Aliyekuwa Mkuu wa Gereza Ukonga, wenzake wakutwa na kesi ya kujibu
Aliyekuwa Mkuu wa Gereza la Ukonga, Josephat Mkama (aliyejifunika shuka) akiwa na aliyekuwa ofisa Tehama wa gereza hilo, Sibuti Nyabuya ( mwenye t-shirt nyeupe) pamoja na mfanyabiashara, Joseph Mpangala (mwenye shati la dark blue) wakitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, baada ya kusomewa hoja za awali katika kesi ya kughushi barua ya msamaha wa Rais kwa wafungwa na kujipatia Sh 45 milioni. Picha na Maktaba
Muktasari:
- Ni kesi wanayodaiwa kughushi barua ya msamaha wa Rais, akionesha imetolewa kwa wafungwa watatu raia wa China na kujipatia Sh45 milioni.
Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemkuta na kesi ya kujibu aliyekuwa Mkuu wa Gereza la Ukonga, Josephat Mkama na wenzake wawili wanaokabiliwa na kesi ya kughushi barua ya msamaha wa Rais kwa wafungwa waliopo gerezani.
Baada ya kukutwa na kesi ya kujibu, washtakiwa hao wataanza kujitetea Juni 8 na 9, 2026 mahakamani hapo.
Uamuzi huo umetolewa leo, Ijumaa Mei 15, 2026, na Hakimu Mkazi Mwandamizi Geofrey Mhini, baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wao.
Mkama na wenzake, Sibuti Nyabuya, aliyekuwa Ofisa Tehama wa Gereza la Ukonga, na mfanyabiashara Joseph Mpangala, wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 25517 ya mwaka 2024.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka manne ambayo ni kuongoza genge la uhalifu, kughushi barua ya msamaha wa Rais kwa wafungwa, kuwasilisha nyaraka ya kughushi na kujipatia Sh45 milioni kwa udanganyifu.
“Mahakama imepitia ushahidi wa mashahidi wanane na vielelezo kadhaa na imeshawishika kuona kuwa washtakiwa wana kesi ya kujibu, hivyo wanatakiwa kujitetea.
“Kwa sababu hiyo, washtakiwa watatakiwa kuanza kujitetea Juni 8 na Juni 9, 2026 mahakamani hapa,” amesema Hakimu Mhini, kisha kuahirisha kesi hadi tarehe hiyo.
Awali, Wakili wa Serikali, Cathbert Mbiling’i, alidai kuwa kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya usikilizwaji, lakini upande wa mashtaka umefunga ushahidi.
Baada ya kutoa taarifa hiyo, Wakili wa utetezi, Eveline Munisi, anayemtetea mshtakiwa Mkama na Mpangala, alidai kuwa wateja wake watajitetea kwa kiapo wao wenyewe bila kuita shahidi mwingine na pia watakuwa na vielelezo.
Kwa upande wake, Wakili Mshana anayemtetea mshtakiwa Nyabuya, alidai kuwa mteja wake atajitetea kwa kiapo yeye mwenyewe bila kuita shahidi mwingine na atakuwa na kielelezo kimoja.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Desemba Mosi, 2022 hadi Januari 30, 2023 jijini Dar es Salaam.
Wanadaiwa kughushi barua ya msamaha wa Rais kwa ajili ya wafungwa watatu raia wa China wenye namba 585/2019 Song Lei, namba 205/2019 Xiu Fu Jie na 206/2016 Haung Quin, waliofungwa katika kesi tofauti kwa makosa ya nyara za Serikali.
Inadaiwa kuwa Machi 18, 2016, wafungwa watatu wenye asili ya China ambao ni mfungwa namba 585/2019 Song Lei, namba 205/2019 Xiu Fu Jie na 206/2016 Haung Quin, walihukumiwa kutumikia adhabu ya kifungo katika Gereza la Ukonga.
Wafungwa hao walihukumiwa vifungo tofauti kila mmoja baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya kukutwa na nyara za Serikali na wote walikuwa hawajuani.
Hata hivyo, Desemba 21, 2022, Mkama ambaye kwa wakati huo alikuwa Mkuu wa Gereza hilo na Nyabuya ambaye alikuwa Ofisa Tehama wa gereza hilo kwa kipindi hicho, walitengeneza nyaraka ya kughushi yenye kichwa cha habari: “Nyongeza ya msamaha kwa wafungwa katika kuadhimisha miaka 61 ya Uhuru.”
Nyaraka hiyo, ambayo ni barua ya Desemba 21, 2022, iliyosainiwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Kaspar Mmuya, ilionesha kuwa wafungwa hao watatu wameongezwa katika idadi ya wafungwa waliopewa msamaha na Rais.