Wanaswa kwa tuhuma kujipatia Sh10 mil za ‘tuma kwa namba hii’

Wakazi 12 wa Ifakara mkoani Morogoro wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisitu, baada ya kusomewa mashtaka 32 yakiwemo ya kujipatia Sh 10milioni kwa nnia ya unganyifu kwa kutuma sms maarufu " tuma pesa kwa namba" pamoja na kutumia laini za simu ambazo za watu wengine bila ridhaa yao. Picha na Hadija Jumanne
Muktasari:
- Mboyo na wenzake wanakabiliwa na mashtaka 32 yakiwemo ya kutakatisha fedha, kutumia ujumbe mfupi kwa watu mbalimbali wakidai kuwa wametuma fedha kimakosa na hivyo wanaomba warejeshewe fedha hizo, huku wakijua ni uongo.
Dar es Salaam. Wakazi 12 wa Ifakara mkoani Morogoro, akiwemo Noel Mboyo (37) maarufu kama Mkono wa Chuma, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashtaka 32 yakiwemo ya kusambaza ujumbe mfupi kwa njia ya mtandao wakitaka fedha, kuongoza genge la uhalifu, kujipatia Sh 10 milioni kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha fedha hizo.
Washtakiwa hao ni Barnaba Gidajuri (45), Rahimu Sangila (20), Ramadhan Mcheni (28), Leonard Mwilenga (23), Mohamed Masalanga (24), Festo Ndizi (27), Richard Masunga (23), Zabron Mkoi (22).
Wengine ni Shafii Mtambo (18), Mussa Lwena (23) na Agrey Razaki (23) ambao wote kwa pamoja wamefikishwa mahakamani hapo leo Mei 28, 2024 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 14185/2024.
Washtakiwa hao wamesomewa mashtaka yao na wakili wa Serikali, Tumaini Mafuru, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swallo.
Katika mashtaka 32 yanayowakabili washtakiwa; mashtaka 20 ni ya kutuma ujumbe mfupi wa sms kwa watu mbalimbali wakitaka fedha; saba ni ya kusambaza ujumbe mfupi wa sms kwa njia ya mtandano; mashtaka mawili ya kujipatia fedha; shtaka moja ni kuongoza genge la uhalifu na jingine ni kutakatisha fedha.
Kabla ya kusomewa mashtaka yao, Hakimu Swallo amesema washtakiwa hawatakiwi kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.
Pia shtaka la kutakatisha fedha linalowakabili washtakiwa hao halina dhamana kwa mujibu wa sheria.
Hakimu Swallo baada ya kueleza hayo, ndipo washtakiwa hao waliposomewa mashtaka yao.
Akiwasomea mashtaka yao, wakili Mafuru amesema katika shtaka la kwanza, washtakiwa wanadaiwa kuongoza genge la uhalifu, tukio wanalodaiwa kulifanya kati ya Januari Mosi hadi Mei 5, 2024, ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Inadaiwa siku hiyo, washtakiwa kwa pamoja walianzisha na kutumia ujumbe mfupi wa maandishi (sms) kwa njia ya mtandano kwa watu mbalimbali na kujipatia Sh10 milioni.
Shtaka la pili ni kusambaza ujumbe mfupi wa maandishi kwa njia ya mtandao linamkabili Gidajuri peke yake, ambapo anadaiwa Januari 4, 2024 katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa nia ya kutenda kosa, mshtakiwa alituma ujumbe uliosema " Uyu mzee Mkuyu ni mganga wa tiba asili anatoa mali bila kafara, cheo, nyota, pete, zindiko, mvuto wa biashara, mapenzi uzazi, kazi, masomo na kesi,"
Inadaiwa kuwa mshtakiwa huyo alituma ujumbe huo kwenda kwenye simu ya mtu mwingine kwa lengo la kutumiwa fedha, wakati akijua kuwa ni kinyume cha sheria.
Shtaka la tatu ni kutuma ujumbe mfupi wa maandishi kwa njia ya mtandao kwenda watu mbalimbali linalomkabili Gidajuri, pekee yake, ambapo anadaiwa kulitenda Februari 4, 2024, ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Inadaiwa siku hiyo, mshtakiwa kwa nia ovu alituma ujumbe uliosomeka kama "Jiunge na chama huru (666) Freemason Tanzania bila kafara za bianadamu badilisha maisha yako, safisha nyota yako wasiliana na Agent kwa namba hizo".
Pia mshtakiwa Gidajuri, Sangila, Mcheni Mwilenga, Masalanga, Ndizi, Masunga, Mkoi, Mboyo na Mtambo wanakabiliwa na mashtaka 20 ya kutumia laini za simu zilizosajiliwa na watu wengine bila ridhaa yao.
Inadaiwa Mei 11, 2024 katika maeneo mbalimbali ya Tanzania, mshtakiwa huyo alitumia laini ya simu iliyosajiliwa na kutumiwa na Reah Rukabanija, Kundi Nkinda, Abbias Matui, Asia Ngalambela na Stephen Lihami, Shida Mwalongo, Ernest Mrotwa, Thadei Nyanyali, Zinduna Gaganda, Maimuna Mwarabu, Merry Mahimbali, Theresia Hamis, Tea Chikalati, Amina Salim, Irene Saidi, Tobiana Kalolo, John Lugendo, Nundu Gulenya, Christina Mandaki na Andrew Kapilimi ambapo washtakiwa hao wanadaiwa kutumia laini hizo bila idhini ya wamiliki wa laini hizo.
Pia, Gidajuri pekee yake anakabiliwa na shtaka la kujipatia Sh105,000 kwa njia ya udanganyifu, kutoka kwa Maria Nangwa, baada ya kujipambanua kuwa yeye ni mganga wa kienyeji atamtibu ugonjwa wa kifafa wakati akijua kuwa ni uongo.
Wakili Mafuru aliendelea kudaiwa kuwa mshtakiwa Sangila, Ndizi, Mkoi, wanakabiliwa na mashtaka saba ya kusambaza ujumbe mfupi wa maandishi kwa njia ya mtandano kwenda kwa watu mbalimbali wakidai kuwa wametuma fedha kimakosa hivyo, wanaomba warejeshewe fedha hizo kwenye laini zao.
Washtakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa yao Mei 5, 2024 huko Ifakara, ambapo inadaiwa kwa nia ovu walisambaza ujumbe uliosomeka kama "Mimi mwenye nyumba yako apa mbona siku zinazidi".
Pia walituma ujumbe uliosomeka kama " Habari za leo, mimi mwenye nyumba yako, mbona kimya na siku zinaenda".
Washtakiwa hao wanadaiwa pia, kutuma ujumbe kwa njia ya sms uliosomeka kama " Umepokea Sh 100,000 kutoka Master card CRDB mnamo 6/5/2024, salio lako jipya ni Tsh 100,032 kupitia simu ya mkononi.
Pia, washtakiwa hao wanadaiwa kutuma ujumbe uliosomeka kama " Imedhibitisha kuwa umepokea Sh300,000 kutoka CRDB bank kwenda kwa Veronica Gamuya mnamo saa 7 mchana, salio lako ni Sh 398,000, wakati wakijua kuwa ni uongo.
Katika shtaka la kuharibu ushahidi, linalomkabili Mboyo pekee yake, inadaiwa Mei 7, 2024 eneo la Viwanja sitini huko Ifakara, kwa nia ya kupoteza ushahidi, alivunja simu ya mkononi aina ya Tecno na kupoteza uhalisia wa simu hiyo na kushindwa kupatikana ushahidi huo.
Katika shtaka la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu linalowakabili washtakiwa wote, Wakili Mafuru alidai kuwa washtakiwa hao wanadaiwa katika tarehe tofati kati ya Januari Mosi, 2024 hadi Mei 5, 2024 katika mikoa tofauti mbalimbali, walijipatia Sh10 milioni kutoka kwa watu mbalimbali, kwa kujitambulisha kuwa fedha hizo walizituma kimakosa kwenye simu zao, hivyo wanatakiwa wazirudishe.
Shtaka la 32 ni la kutakatisha fedha linalowakabili washtakiwa wote, ambapo wanadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Januari mosi hadi Mei 5, 2024 katika mikoa mbalimbali ya Tanzania.
Inadaiwa siku hiyo, washtakiwa kwa nia ovu walijipatia Sh10 milioni wakati wakijua ni udanganyifu.
Washtakiwa baada ya kusomewa mashtaka yao, hawakutakiwa kujibu chochote na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa shauri hilo bado unaendelea.
" Upelelezi wa kesi hii bado unaaendelea, hivyo tunaiomba mahakama yako ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa," alidai wakili Mafuru.
Hakimu Swallo aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 11, 2024 kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na shtaka la kutakatisha fedha linalowakabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria.