Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Maswali magumu utapeli kwa njia simu

Moshi/Dar. Kwa nini laini za simu zimesajiliwa kwa kitambulisho cha Taifa na alama za vidole lakini bado matapeli wanaendelea kutamba? Hili ni miongoni mwa maswali yanayoumiza vichwa vya watu huku ikielezwa kuwa zaidi ya laini 100,000 zimefungwa katika kipindi cha mwaka mmoja.

Baadhi ya Watanzania waliozungumza na gazeti hili wakiwemo wasomi na wanasheria, wametupa lawama kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Jeshi la Polisi, kwa kile walichodai kuzidiwa maarifa na matapeli.

Hata hivyo, TCRA wameeleza namna ambavyo hawalali usiku na mchana kupambana na matapeli hao kwa kushirikiana na Polisi na watoa huduma ambapo kati ya Julai 2022 na Juni 2023, wamefungia namba tambulishi 108,395 zikiwemo za utapeli.

Mamlaka hiyo iliyoanzishwa mwaka 2003, imesema mawakala wanaokiuka kanuni za usajili wa laini, wanaweza kuadhibiwa kwa faini isiyopungua Sh5 milioni au kifungo kisichopungua miezi 12 au vyote kwa pamoja.

Baadhi ya wananchi hao wamedai kuwa huenda baadhi ya wafanyakazi wa baadhi ya kampuni za simu wako kwenye mgawo wa matapeli, wakihoji laini hizo zilisajiliwaje na fedha za utapeli zinatolewaje bila vitambulisho.

Wananchi hao walilitaka Jeshi la Polisi nchini, kama linavyotoa taarifa kwa mbwembwe linapowakamata matapeli wa mtandaoni wakiwamo wale wa ‘Tuma hiyo pesa kwenye namba hii’, vivyo hivyo watoe idadi ya waliofikishwa kortini na kupatikana na hatia.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa baadhi ya mawakala wa usajili wa laini za simu, hushirikiana na matapeli hao wa mtandaoni kwa kuwasajilia laini moja kwa kati ya Sh10,000 na Sh20,000 kwa kutumia majina na vitambulisho vya watu wengine.

Gazeti hili limedokezwa kuwa kinachofanyika ni kwamba mteja anapokwenda kusajili namba yake, wakala mtoa huduma anapomwambia aweke kidole kwenye mashine, humwambia haikusoma hivyo arudie na mara zote anazorudia ni laini mpya imesajiliwa.

Wakala mmoja ambaye aliomba jina lake lisitajwe gazetini, alisema tatizo ni Watanzania hawana utamaduni wa kufuatilia na kuhakiki kujua kitambulisho chake cha Taifa kimesajili laini ngapi anazozitambua kwa kupiga *106#, ili azifute zisizo za kwake.

Mteja anapotumia namba hiyo, humpa fursa ya kuangalia usajili wa laini yake, namba zilizosajiliwa kwa mtandao huo, namba zilizosajiliwa mitandao yote kwa kitambulisho chake cha Nida, kufuta usajili wa laini na kuhakiki na kuongeza namba.

“Lakini kumekuwa na ujumbe huwa kila mteja anatumiwa kwamba atume taarifa za utapeli unaofanyika kwa njia ya simu kwa kutuma ujumbe kwenye namba 15040 lakini hawafanyi hivyo. Akishapokea ujumbe wa kitapeli anaufuta basi,” alisema.

Mbali na hilo, wakala huyo alisema kampuni za simu zimekuwa zikiwatumia wateja wao ujumbe, kuwajulisha kuwa kama ni kupigiwa simu na kitengo cha huduma kwa mteja watapigiwa kwa namba 100, lakini bado wanapokea namba ngeni.

Polisi nao wamekuwa wakituma ujumbe unaosomeka”Usifuate maelekezo kuhusu huduma unazozitumia kutoka kwenye namba usiyoifahamu na kwamba (Halotel, Vodacom, Tigo, Airtel n.k) itawasiliana nawe kwa namba 100 pekee”.


Utapeli unaotikisa nchi

Licha ya jitihada kubwa zinazofanywa na TCRA, Polisi na vyombo vingine kukabiliana na uhalifu ukiwamo utapeli kwa njia ya simu, bado vitendo hivyo vinaendelea kutikisa nchi, licha ya laini za simu kusajiliwa kwa kitambulisho cha Nida na alama za vidole.

Ujumbe mfupi kama “Hiyo hela itume kwenye namba hii” au “Simu yangu imekufa sauti wewe tuma kwenye namba hii” ama “simu yangu imezima charge tuma huku”, zimeendelea kupokelewa na wateja zikitumwa kwa namba tofauti tofauti.

Ujumbe mwingine ni za uganga kuhamasisha utajiri wa haraka haraka ambapo husomeka “Mzee ndio dawa mtaalamu wa tiba asilia kama vile kusafisha mwili mvuto wa biashara na pia kupata mali bila kafara piga namba (zinawekwa namba)”

Baadhi ya ujumbe huo, wanaoutengeneza hujifanya kukosea kosea Kiswahili ili kuonyesha anayeandika ni mzee na kumshawishi mtu aliyetumiwa ujumbe kuwa yeye ana uwezo wa kurejesha mke au mume, kufaulu mitihani au machimbo yateme.

Ujumbe huo husomeka “Nyota imechafuliwa mambo yamebadilika utafutaji mugumu ukipata pesa hazikai mukononi je utatunza siri nikusaidie pesa bila masharti?nipigie au “Mjukuu wangu nimekuandalia dawa ya mvuto wa biashara”

Lakini baadhi ya matapeli hujifanya ni mabosi wa taasisi fulani ambao wamekosea kutuma sms na kujifanya kueleza kuwa “Ile nafasi ya Jeshi nimekupatia ila fanya haraka tuwasiliane,”kiuhalisia watu hujichanganya kutokana na tatizo la ajira lilivyo.

Matapeli wengine hupiga simu kwa kutumia namba za mitandao ya kampuni mbalimbali wakijifanya wanapiga simu kutoka kitengo cha huduma kwa wateja kwamba wanaboresha huduma za miamala au kueleza kuwa amepokea fedha kimakosa.


Wasomi, Wanasheria, wananchi wafunguka

Mtaalamu wa masuala ya uchumi na biashara, Dk Shalom Muzo alisema anachokiona kuna ushirikiano wa karibu kati ya matapeli na baadhi ya wafanyakazi wa kampuni za simu hasa katika usajili wa laini na utoaji wa fedha zilizoibwa kimtandao.

“Mimi nafikiri ipo haja ya kuwa na sheria au kanuni ambazo zitakazopiga faini hizi kampuni za simu. Ikitokea laini ya mtandao X imefanya utapeli kwa Y na hiyo laini imesajiliwa kwa njia haramu kampuni ya simu iwajibike kulipa faini,”alisema.

Wakili Peter Mshikilwa, alisema anachokiona mamlaka husika zimezembea kuchukua hatua kali hasa ikizingatiwa kuwa kuna sheria nzuri za kukabiliana na matukio kama hayo na kwamba uzembe huo ni wa kampuni ya simu na mamlaka za usimamizi.

Kwa upande wake, wakili Elia Kwia alisema inawezekana Jeshi la Polisi halifanyi kazi yake ipasavyo au labda kuna namna nyingine ambayo matapeli wanaweza kusajili laini bila kutumia kidole kwa sababu isingekuwa rahisi kutokamatwa watu hao.

Ansi Mmasi aliyewahi kuwa meneja wa Vodacom alisema kwa mfumo ulivyo ni ngumu kupata laini bila kusajiliwa akasema ujanja unafanywa na baadhi ya wanaosajili laini bila mteja kujua kama kaweka dole lake kwenye komputa na kusajili zaidi ya laini moja.

“Pamoja na elimu ndogo pia, umakini kwa wateja ni mdogo. Mfumo kama mfumo upo makini kwani hata ukitaka kujua laini zako zote zilizosajiliwa kwa kitambulisho chako cha Taifa katika mitandao yote utajua ila wateja kukagua ni changamoto,”alisema.

Mkazi wa Moshi, Renalda Evance alisema anachokiona ni kuwa wapo baadhi ya wafanyakazi katika kampuni za simu wanashirikiana na matapeli kwa kuwa pesa ikiingia kwenye simu na kama ni nyingi, muda huo huo matapeli nao wanapiga simu.

“Ninashauri watu wenye dhamana ya kuajiri na kusimamia wafanyakazi katika kampuni za simu wawe makini sana wakati wa kuajiri lakini waweke pia sheria kali zinazokataza kutoa siri za mteja. Wafukuze mawakala wasio waaminifu,”alisema.

Hata hivyo jitihada za Mwananchi,kumpata Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Camillius Wambura au Msemaji wa jeshi hilo, David Misime kuzungumzia hatua wanazozichukua kukabiliana na utapeli wa mitandao ziligonga mwamba kutoka na simu zao kuita pasi majibu na kutojibu ujumbe waliotumiwa.

Mmoja wa Ofisa wa jeshi hilo ambaye ni mtaalamu wa makosa ya kimtandao, alidokeza kuwa vijana wanaopewa kazi ya kusajili watu wanachangia tatizo hilo kwa kuwa wanasajili bila kufuata taratibu zinazotakiwa

Meneja wa chama cha Akiba na Mikopo kwa Walimu Moshi Vijijini ((MRT-SACCOS), Bosco Simba alisema anachokiona kuna baadhi ya wafanyakazi wa kampuni za simu sio waaminifu na hawasajili laini au kutoa fedha bila kufuata vigezo vilivyowekwa.

Mwandishi wa Habari, Arodia Rweyemamu alisema kiini cha kuendelea kushamiri kwa uwepo wa matapeli ni uwajibikaji hafifu wa TCRA kutokana na kuwepo mifumo dhaifu ya teknolojia ambayo inafanya matapeli wacheze nayo.

Khatibu Shekoloa ambaye ni mfanyabiashara, alisema kuendelea kuwepo kwa matapeli wa mitandaoni wanaotumia simu kutapeli kunatokana na kazi ya usajili wa laini kufanywa kiholela na kupendekeza ziwepo kanuni na vituo rasmi vya usajili.


Kauli ya TCRA

Akijibu maswali ya gazeti hili kuhusiana na changamoto hiyo, Mkurugenzi mkuu wa TCRA, Dk Jabir Bakari alisema mamlaka kwa kushirikiana na Polisi, imeweka jukwaa la kupokea taarifa za utapeli na majaribio ya utapeli kwa kutuma ujumbe namba 15040.

“Hii ni namba ambayo mtumiaji wa huduma za mawasiliano ya simu anaweza kutuma ujumbe wa kutoa taarifa ikiwa amekabiliwa na utapeli kwa njia ya ujumbe mfupi au kwa njia ya kupigiwa kwa sauti,”alisema

Ujumbe huo utalifikia Jeshi la Polisi ambao watafanya ufuatiliaji, mtoa huduma ataifungia laini hiyo inayojaribu kutekeleza utapeli na TCRA itatunza kumbukumbu ya laini za simu zilizofungiwa kwa kujihusisha na utapeli kwa ajili ya maboresho.

Dk Bakari alisema hadi Juni 2023 laini 108,395 zilikuwa zimefungiwa zikiwemo za watu wanaotekeleza utapeli au kufanya majaribio ya utapeli kwa njia ya simu ambazo ziliripotiwa kupotea, kuibwa au kuhusika katika matukio ya kihalifu.

Kuhusu mawakala wasio waaminifu wanaosajili laini na kuwauzia matapeli au wahalifu, Dk Bakari alisema hao wanadhibitiwa kisheria na Kanuni za Usajili wa Laini za Simu za 2023 ambazo zinaweka mahitaji mahsusi kwa mawakala.

“Mahitaji hayo ni pamoja na kuwa na anuani ya makazi au ofisi rasmi, kitambulisho halali cha Taifa, mkataba halali na mtoa huduma, hati safi ya polisi na kitambulisho halali kilichotolewa na mtoa huduma,”alisema mkurugenzi.

 Mawakala wanaokiuka kanuni hizi wanaweza kuadhibiwa kwa faini isiyopungua Sh5 milioni au kifungo cha kipindi kisichopungua miezi 12 au vyote.

Mkurugenzi huyo amewataka wananchi kuwa makini na kuchukua tahadhari wanapotumia huduma za mawasiliano ya simu akisema utapeli kwenye mtandao ni changamoto ambayo inahitaji jitihada za pamoja na wadau wote.

Dk Bakari alidokeza kuwa Oktoba, 2023, TCRA itakuwa na kampeni maalumu ya kuhamasisha matumizi salama ya mtandao yenye kauli mbiu ya “Futa Delete Kabisa”.