Utapeli miamala ya simu tishio

Muktasari:
Wakizungumza kwa njia ya simu na gazeti hili, baadhi ya watumiaji wa simu walisema wamejikuta wakitapeliwa kwa kutoa namba zao za siri.
Dar es Salaam. Wizi wa uhamishaji wa miamala kwenye simu za mkononi umeshika kasi, baada ya kuibuka makundi ya kitapeli, moja likitumia hoja ya kuzimwa simu feki na lingine likitumia mbinu ya kuwapa zawadi wateja wa muda mrefu.
Wakizungumza kwa njia ya simu na gazeti hili, baadhi ya watumiaji wa simu walisema wamejikuta wakitapeliwa kwa kutoa namba zao za siri.
Mwathirika wa utapeli wa njia ya simu, Magdalena Mungai, mkazi wa Vingunguti, jijini Dar es Salaam alisema alifuatwa nyumbani kwake na watu waliojitambulisha wanasajili simu na kumtaka awape taarifa za simu yake ikiwamo namba ili waihuishe (activation) isije ikazimwa.
Alisema, akijua kuwa Juni mosi simu feki zinazimwa alikubali akiamini hao wanatoka kampuni ya Tigo, lakini baada ya siku mbili alibaini kuibiwa Sh200,000.
“Nilikuwa nimetumiwa ada ya mtoto, sasa nataka nikatoe ili nilipe, naambiwa huna salio la kutosha, nilipoangalia salio kweli hakuna pesa,” alisema.
Magdalena alisema alipokwenda ofisi za Tigo, aliambiwa kuwa mtiririko wa miamala unaonyesha kuna mtu alitoa fedha hizo.
Mtembezi Asili ambaye ni mteja wa mtandao wa Tigo alisema alitapeliwa akiwa na wenzake alipokwenda kumtembelea ndugu yake Chanika Kidete, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Alisema huko walikutana na vijana waliojitambulisha wanatoka kampuni ya Tigo, kazi yao ni kutoa zawadi kwa wateja waliokaa na laini kwa zaidi ya mwaka bila kupotea. “Wakasema watatupa zawadi, ila tutaje majina yetu kamili na namba za siri. Walitupa namba fulani siikumbuki vizuri ambayo tunatuma majina na namba zetu za siri.
Baadaye akapiga simu akisema tuongee na ‘customer care’ (mhudumu). Alitumia simu yake halafu akanipa niongee naye. Kweli yule mhudumu alisema anajua jina langu na namba yangu ya siri. Akasema zima simu yako, fungua line ya simu kuna namba zimeandikwa hapo,” aliendelea kusimulia Mtembezi.
Alisema alikubali kutoa laini ya simu yake na kumsomea namba zilizoandikwa, kisha akaambiwa asiwashe simu yake hadi baada ya dakika 45 ndipo atapewa zawadi yake.
“Nilikuwa nimezima simu, kuiwasha nikaona hakuna network (mtandao), nikajiuliza kwa nini, lakini nikajipa moyo kwamba mpaka dakika 45 kama walivyosema,” alisema.
Alisema alipofika ofisini alianza kujishtukia na kuwasimulia wenzake kilichotokea. Wenzake walimwambia huo ni utapeli.
“Wenzangu wakaniambia hapo kweli nitakuwa nimeibiwa. Nikachukua simu ya mwenzangu mmoja nikapiga ‘customer care’ wakapokea na nikawaelezea yote. Wakaniuliza kama line ilikuwa na fedha nikawaambia ilikuwa na Sh1,225,000,” alisema.
“Wakaniambia wameshaiba ila kuna Sh10,500. Akasema wametoa Sh500,000 kwa wakala mmoja, Sh400,000 kwa wakala mwingine, Sh200,000 wamemtumia mtu wa namba nyingine sijui Sh5,000, namba nyingine Sh10,000… kitu kama hicho,” alifafanua Mtembezi.
Alisema mhudumu wa Tigo Pesa alimuambia atoe taarifa kitengo cha Tigo Pesa na asajili upya laini yake.
Naye (Fatuma) ambaye ni mdogo wake Mtembezi alisema wakati matapeli hao wakitoa maelekezo aliwashtukia mapema akasita kutekeleza wanachosema.
“Mimi sikuibiwa ila nilishindwa kumuambia dada. Kuna tapeli mmojawapo aliniomba simu yangu nikamkatalia. Waliposema tutume namba za siri nikatuma za uongo,” alisema.
Alizilaumu kampuni za simu akisema zinahusika na utapeli huo kwa sababu wanajua kila wanachofanya matapeli.
Msemaji wa kampuni ya Tigo, John Wanyancha hakutaka kuzungumzia suala hilo huku akimtaka mwandishi wa habari hizi kumtumia maswali kwa barua pepe ili ajibu Jumatatu.
“Leo hatufanyi kazi, niandikie maswali yako kisha nitumie email, nitakujibu Jumatatu,” alisema Wanyancha.
Hata hivyo, ofisa habari wa Airtel, Jackson Mmbando alisema hana taarifa za utapeli kwa wateja wao zaidi ya matatizo ya kukosea kutuma pesa.
“Tunachojua sisi ni matatizo ya mteja mmoja mmoja; kwamba mteja anaweza kuwa amekosea kutuma pesa mahali tunamsaidia kurudisha, hayo tunayapata sana. Mtu hawezi kuibiwa fedha kwenye simu labda atoe namba yake ya siri,” alisema Mmbando.
Kwa upande wake, Mkuu wa kitengo cha mawasiliano wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano (TCRA), Innocent Mungy alithibitisha kukithiri kwa wizi kwa njia ya simu na mitandao na kusema Jeshi la Polisi ndilo linashughulikia wahalifu hao.
“Utapeli huo umekuwa mkubwa sana siku za hivi karibuni kwa sababu watu wengi hawako makini,” alisema Mungy.
Alisema Polisi ndiyo wenye jukumu la kushughulika na utapeli kwa kupata ushirikiano wa TCRA.
“Sisi TCRA hatushughuliki na utapeli ila tunashirikiana na Jeshi la Polisi kupitia kitengo chao cha Cyber Crime. Tunashirikiana pia na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru); wanaweza kuja kuulizia namba zilizotumika kwenye uhalifu na sisi tutawasaidia kuzipata,” alisema Mungy.
Alisema pia wamekuwa wakitoa elimu kwa watumiaji wa simu na mitandao kuhusu uhalifu huo.