Wanaonyanyasa wanawake wajane, kufanya ukatili jinsia waonywa

Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa (MNEC), Mkoa wa Mbeya, Ndele Mwaselela akizungumza na wajane katika ukumbi wa Mkapa jijini hapa. Picha na Hawa Mathias
Muktasari:
- Matendo haya yamekuwa chanzo kikubwa cha kukosekana kwa haki za msingi kama urithi, elimu, na huduma za afya. Zaidi ya hayo, unyanyasaji huu hudidimiza maendeleo ya wanawake, kuendeleza umasikini, na kuvuruga mshikamano wa kijamii.
Mbeya. Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mbeya kimekemea vikali vitendo vya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji vinavyotendeka dhidi ya wanawake wajane nchini.
Onyo hili limekuja kufuatia kilio cha wajane kwa Serikali, wakidai kuingilia kati kwa dharura ili kudhibiti vitendo hivyo vinavyoathiri kisaikolojia na kuwatatiza kupata msaada wa kisheria.
Kauli hiyo imetolewa na Mwakilishi wa Chama cha Wajane Mkoa wa Mbeya, Kissa Worden, leo Jumanne Juni 24, 2025 wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wajane Duniani ambayo kimkoa yamefanyika katika Ukumbi wa Mkapa jijini hapa.
Kissa amesema kwa muda mrefu baada ya kupoteza wenza wao wamekuwa wakikumbwa na kadhia mbalimbali za kufanyiwa vitendo vya ukatili, kulazimishwa kurithiwa na kunyimwa haki za msingi kwa watoto na hivyo kuathirika kisaikolojia.
"Kwanza tunamshuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuona makundi la wajane na wanawake na kuja na mkakati wa kutengeneza mazingira wezeshi, lakini ombi letu kuanzishwe mfuko wa kuwasaidia na kituo cha elimu ya saikokojia kwa kundi hilo," amesema.

Katika hatua nyingine wameomba Serikali kuja na njia mbadala ya kutoa elimu ili kujua haki zao za msingi na uchumi bora.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa (Mnec), Mkoa wa Mbeya, Ndele Mwaselela amesema Serikali haitaweza kuvumilia wajane wakinyanyasika na kwamba imefungua milango ya kupokea malalamiko.
Amesema dhamira ya kiongozi ni kuleta ustawi wa uchumi kwa wananachi wake na ndio dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan, kuja na mpango wa msaada wa kisheria.
"Lengo ni kuona kama kuna mjane anaporwa mali zake, kunyanyaswa kuwa ni sehemu sahihi ya kukimbilia na siyo kuishi maisha ya shida, lakini niwahakikishe yoyote atakayefanyiwa ukatili atoe taarifa ili tuwashughulikie," amesema.
Mwaselela amesema atasimama na kutetea haki za wakinamama na yoyote atakaye fanyiwa ukatili wa kijinsia awasilishe ofisini kwake.
"Niliona mama yangu akiteseka nitawatetea bure na atakayehusika na vitendo hivyo atamuombea kwa Mungu atete naye kwani mwanamke siyo sehemu ya wasaliti," amesema.
Katika hatua nyingine, Mwaselela amesema kupitia maadhimisho hayo ametoa tahadhari wananchi kuepuka kuwanyanyasa wajane na wanawake huku akiwataka kukuunga mkono Rais Samia.

"Tunaona wapo watu ndani ya chama wamenza kupigana vijembe na kukanyagana kabla ya muda, niwatake kinamama kuwa makini sana chagueni kiongozi ambaye hawatawagawa," amesema.
Kwa upande wake Ofisa Maendeleo Mkoa wa Mbeya, Elikaga Mwalukasa amesema Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kusaidia makundi ya wanawake wakiwepo wajane.
"Tunaendelea kutoa elimu kuhusu masuala mbalimbali ya msaada wa kisheria kwa wajane ikiwepo suala la uwezeshwaji kiuchumi,"amesema.
Mjane Rehema Joel Mkazi wa Mbata jijini hapa, amesema ukosefu elimu bado ni changamoto na kuomba Serikali kuja na mpango mkakati ili kunusuru kundi hilo.