Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kilio cha wajane kuelekea siku yao, Serikali kuja na mwongozo

Muktasari:

  • Takwimu za kidunia zinaonesha kuwa idadi ya wajane ni takriban milioni 258 kati ya hao, wajane 115 milioni wanadhulumiwa, wanafanyiwa ukatili, wanakabiliwa na umaskini na kutengwa na jamii.

Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikiungana na mataifa mengine kuadhimisha siku ya wajane kesho Juni 23, mila kandamizi, umaskini, kukosa uelewa wa kisheria na changamoto za kisaikolojia zimeendelea kuwa kikwazo kwa kundi hilo.

Baadhi ya wajane waliozungumza na Mwananchi wameeleza licha ya jitihada mbalimbali kuendelea kuchukuliwa kuhakikisha kundi hilo linapata haki zinazostahili bado kuna namna linakabiliwa na hali ngumu.

Mmoja wa wajane hao, Anastazia Hebron ambaye ni mkazi wa Mikwambe, Dar es Salaam amesema kinachowasumbua wengi ni kukosa uelewa wa kisheria hivyo kuishia kudhulumiwa au kupoteza mali walizoachiwa na wenza wao.

“Nafikiri kuna haja ya kila mtu kuwa na uelewa hata kidogo wa sheria, wajane wengi wanadhulumiwa na kuishia kuwa wanyonge, binafsi nimepitia changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na kusumbuliwa na familia ya mume wangu lakini nilisimama imara.

“Bahati ilikuwa kwangu kwa sababu nilipata watu wanaojua sheria hivyo walinipa mwongozo ambao kwa kiasi kikubwa umenisaidia kupambania haki yangu na watoto, hili ndilo tunakosa wanawake wengi matokeo yake tunaishia kuwa wanyonge,” amesema.

Kufuatia hilo, Anna anasisitiza watu kutenga muda wa kujifunza vitu muhimu katika sheria mbalimbali ikiwemo zinazohusu mirathi na umiliki wa ardhi ili kuwa na uelewa wa kina.

Kwa upande wake, Rehema Said, mkazi wa Mbagala Kigungi amesema umaskini ndiyo tatizo kubwa linalowakabili wajane hasa waliokuwa tegemezi.

“Wengine hatujaachiwa hizo mali za kugombaniwa, ni umaskini juu ya umaskini, watoto wanakuangalia wewe na huna chochote cha kukuingizia kipato. Hiyo mikopo inayosemwa huwezi kupewa kama huna biashara ya kueleweka. Hii inatufanya tunaishia kuwa ombaomba.

“Natamani kungekuwa na utaratibu kupitia Serikali zetu za mitaa kungekuwa na fungu la kutuwezesha tufanye hata biashara ndogo, isiwe mikopo watenge tu kiasi kidogo mtu upewe ukafanye biashara baada ya hapo utapambana na maisha mwenyewe,”amesema Rehema.

Kwa mujibu wa takwimu za ripoti ya Sensa ya Watu na Makazi mwaka 2022 Tanzania ina idadi ya wajane 1,396,262 sawa na asilimia 4.4 ya wanawake wote nchini.

Hata hivyo, huenda changamoto hizo zikafikia ukomo kufuatia mwongozo ulioandaliwa na Serikali unaolenga kuweka mfumo imara wa uratibu wa wajane katika ngazi ya jamii.

Mwongozo huo utakaozinduliwa kesho Juni 23,2025 wakati wa maadhimisho hayo mkoani Iringa, utasaidia kuachana na mila na desturi kandamizi dhidi ya wajane ikiwemo kunyang’anywa mali, kuozesha watoto wa kike katika umri mdogo vitendo ambavyo vinawaathiri wanawake kifikra, kiuchumi na maendeleo ya kijamii.

Kauli ya Serikali

Kupitia taarifa ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha inawatambua na kuwajali wajane kwa kuweka mazingira bora na wezeshi kwa ajili ya ustawi wa familia zao.

Mojawapo ya hatua hizo ni kuimarisha mifumo ya kulinda haki za wajane kupitia kutungwa kwa Sheria ya Msaada wa Kisheria Na. 1 ya mwaka 2017, ambayo imeongeza utoaji wa huduma za utetezi wa haki za binadamu wakiwemo wajane.

“Vilevile, Sheria ya Ardhi ya Kijiji Na. 5 ya 1999 iliyowawezesha wanawake kumiliki ardhi. Pia tunatekeleza Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia na Kampeni ya Mwanamke na Ardhi zenye lengo la kulinda haki ya upatikanaji wa msaada wa kisheria kwa wananchi wakiwemo wajane kuhakikisha wamepata huduma na elimu kuhusu haki, ardhi, wosia, ndoa, migogoro ya ajira na ukatili wa kijinsia,” imeeleza taarifa hiyo.

Katika taarifa hiyo, Dk Gwajima ameitaka sekta binafsi na wadau mbalimbali kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kuimarisha mazingira wezeshi kwa kundi hilo,  ili waweze kushiriki kikamilifu katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na maendeleo ya kuwezesha nchi kufikia malengo ya maendeleo endelevu.

Amesema maadhimisho ya mwaka huu yataenda sambamba na uzinduzi wa Mwongozo  wa Uratibu wa wajane mwaka 2025.

Undani wa siku ya wajane

Siku ya Kimataifa ya Wajane ambayo huadhimishwa Juni 23  kila mwaka kwa lengo la kukuza hamasa, mshikamano na uelewa ndani ya jamii ili kuendelea kukemea ukiukwaji wa haki na kulinda wajane.

Katika maadhimisho hayo tafakuri ya hali za wajane baada ya kufiwa na wenza wao, kuwaunganisha katika mitandao ya kupata taarifa za fursa za kiuchumi, kijamii na uongozi.

Aidha siku hii hutumika kuelimisha kuhusu haki zao, kupinga ukiukwaji wa haki za binadamu, kama vile kunyimwa urithi, kufukuzwa nyumbani, kulazimishwa kuolewa, kutengwa na kukosa msaada wa kisheria. Pia hutoa fursa ya kutafakari mipango, mikakati, mafanikio na changamoto za wajane kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika kuzikabili.

Kaulimbiu ya maadhimisho mwaka huu ni: “Tuimarishe Fursa za Kiuchumi Kuchochea Maendeleo ya Wajane” ambayo, inasisitiza umuhimu wa kuweka mazingira jumuishi na wezeshi kwa wajane ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kijamii, na hivyo kuboresha hali zao za maisha na kuchangia maendeleo ya Taifa kwa ujumla.