Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Jamii yabebeshwa mzigo kukomesha ukatili, uvunjaji haki za binadamu

New Content Item (2)
New Content Item (2)

Muktasari:

  • Jamii imekuwa ikishuhudia matukio ya ukatili ya kutisha, ikiwemo mauaji, wizi wa watoto na dhuluma dhidi ya wajane, hali inayodhihirisha kuporomoka kwa maadili na kupotea kwa hofu ya Mungu.

Moshi. Jamii imetakiwa kukemea na kuchukua hatua madhubuti kukabiliana na ongezeko la vitendo vya ukatili na uvunjaji wa haki za binadamu vinavyozidi kuripotiwa maeneo mbalimbali nchini, huku chanzo kikuu kikitajwa kuwa ni kuporomoka kwa maadili na kukosa hofu ya Mungu.

New Content Item (1)

Baadhi ya wasaidizi wa kisheria kutoka wilaya za Karatu, Babati, Siha, Hai, Moshi na Rombo, walioshiriki mafunzo  ya kuwajengea uwezo wa kukabiliana na mila na desturi potofu zinazochangia ukatili katika jamii.

Rai hiyo imetolewa leo na Katibu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini, Zebadia Moshi wakati wa mafunzo kwa kamati za wasaidizi wa kisheria kutoka wilaya za Karatu, Babati, Siha, Hai, Moshi na Rombo, yaliyofanyika mjini Moshi, yakilenga kuwajengea uwezo wa kukabiliana na mila na desturi potofu zinazochangia ukatili katika jamii.

Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Idara ya Uwakili na Miradi ya KKKT Dayosisi ya Kaskazini, kwa kushirikiana na Shirika la Norwegian Church Aid (NCA), yaliwakutanisha zaidi ya wasaidizi wa kisheria 80.

Moshi amesema kila siku jamii inashuhudia matukio ya ukatili ya kutisha, ikiwemo mauaji, wizi wa watoto na dhuluma dhidi ya wajane, hali inayodhihirisha kuporomoka kwa maadili na kupotea kwa hofu ya Mungu.

“Suala la kusimamia haki katika jamii tunayoishi ni la muhimu sana kwani jamii imezungukwa na matukio mengi ya ukatili na uvunjaji wa haki. Ni jambo la kusikitisha kwamba hakuna siku inapita bila kusikia mauaji au watu kujeruhiwa, huku wahusika wakiwa hawafahamiki,” amesema Moshi.

Ameongeza kuwa vitendo vya kikatili vimekithiri ambapo pia watoto wanatendewa vitendo visivyo vya kibinadamu huku wanawake wakipata mateso ndani ya familia na wajane kunyimwa haki zao za urithi.

“Watu tumekuwa kama wanyama. Tunapaswa kutafakari kwa kina namna ya kurekebisha hali hii, kwani chanzo kikubwa cha hali hii ni kuporomoka kwa maadili na kuondoka kwa hofu ya Mungu,” amesisitiza.

Amesema: “Niwapongeze kwa namna mlivyobeba jambo hili la kutoa elimu kwenye jamii, kutafuta haki kwa njia ya usuluhishi na kusaidia kuondoa chuki inayojengeka, ambayo hupelekea visasi na mauaji.

Amehimiza utekelezaji wa maelekezo ya mradi huo ili jamii iweze kuishi kwa haki, amani na hatimaye kujiletea maendeleo na kuondokana na umasikini.

Baadhi ya wasaidizi wa kisheria kutoka wilaya za Karatu, Babati, Siha, Hai, Moshi na Rombo, walioshiriki mafunzo  ya kuwajengea uwezo wa kukabiliana na mila na desturi potofu zinazochangia ukatili katika jamii.

Kwa upande wake, Ofisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Kilimanjaro, Pili Bayo amewahimiza wasaidizi wa kisheria waliohudhuria mafunzo hayo kuhakikisha wanazingatia elimu waliyoipata na kufuata sheria na taratibu wanapohudumia wananchi.

Naye Katibu wa Idara ya Uwakili na Miradi wa Dayosisi ya Kaskazini, ambaye pia ni Mratibu wa Miradi ya NCA, Mchungaji Andrew Munisi amewataka wasaidizi wa kisheria kuzingatia weledi wakati wa utekelezaji wa majukumu yao na kuepuka kuwa wanaharakati.

“Nendeni mkafanye kazi yenu kwa kuzingatia weledi. Msiende nje ya mipaka yenu na simameni kama wasaidizi wa kisheria kuleta matokeo chanya kwenye jamii," alisema Mchungaji Munisi.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo, wameomba elimu ya kupambana na ukatili iendelee kutolewa katika maeneo mbalimbali nchini ili kuwafikia watu wengi zaidi na kufanikisha juhudi za kutokomeza vitendo hivyo.