Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kuigiza ukatili kunavyochochea tabia za kikatili

Muktasari:

  • Upo uwezekano wa kuiga tabia za kikatili kwa watu tunaojitambulisha nao. Katika mazingira haya, tabia mbaya za kuumiza watu huanza kama mchezo wa kuigiza.

Dar es Salaam. Ukitafakari namna tunavyozungumzia maumivu ya watu, namna tunavyochukulia hisia zao, unaona tulivyo na tatizo kubwa la ukatili katika jamii. Kwa mfano, unaweza kusikia mtu akibeza na kufanyia mzaha maumivu ya mtu, kwa kisingizo kuwa mtu huyo amejitakia.

“Mbona hakuumia? Huyu, kwa ushenzi alioufanya, alitakiwa kuumizwa zaidi. Mngemkomesha zaidi.”

Unaona tunavyofikiri? Tunahalalisha maumivu ya mtu kwa kigezo cha yale aliyoyafanya. Matukio ya wananchi kujichukulia sheria mkono, mathalani, kuua wahalifu ni ushahidi kuwa tunaamini mtu akishakosea, anastahili kuumizwa, kuteswa na hata kuuawa.

Ukisikiliza mazungumzo kwenye vijiwe na mitandao ya kijamii, unaweza kuona namna tulivyo jamii inayobeza masaibu wanayopitia watu tusiowapenda. Hatuoni aibu kutamka maneno makali kama, “Hana adabu kabisa. Ungemuua kabisa yule. Mnamuacha anaondoka akitembea?”

Wakati mwingine matamshi haya hutolewa kama michapo na maoni ya kufurahisha genge kuonesha ushabiki wa michezo, dini na siasa.. Makala haya,  yanaangazia namna maigizo haya ya kukosa huruma kwa watu yanavyoongeza uwezekano wa kugeuka ukatili na unyama.

Ingawa unaweza kujiona una haki ya kubeza masaibu wanayopitia wenzako, mizaha kama hii ikikutana na mazingira fulani fulani hugeuka ukweli wa kitabia.

Utafiti

Mwaka 1971, Philip Zimbardo, mshunuzi na mwalimu wa Chuo Kikuu cha Stanford, alifanya utafiti maarufu kama “Stanford Prison Experiment” akilenga kuchunguza nguvu ya mazingira kwenye tabia.

Zimbardo alitengeneza gereza la kuigiza hapo chuoni likiwa na seli, mahali mfungwa angekaa mwenyewe, mahali pa wanyapara kuishi, mahali wafungwa wangetoka na kuteswa na wanyapara. Washiriki walifanyiwa mchujo wa haiba kuona kama ni watu wenye utimamu wa tabia na hisia. 

Kwa njia ya nasibu (random assignment) wanafunzi 24 wa kiume walitawanywa kwenye majukumu wengine kuwa wafungwa (waliovalishwa jezi bangabanga na vibandiko vya namba) na wengine wakawa wanyapara wa gereza (walivaa sare, wakapewa marungu na miwani nyeusi kuashiria mamlaka). 

Sharti kubwa kwa washiriki lilikuwa kuigiza tabia zinazoendana na jukumu walilopewa. Utafiti ulilengwa kukamilika baada ya wiki mbili lakini ulikatishwa baada ya siku sita kufuatia athari kubwa kihisia zilizojitokeza.

Matokeo

Igizo lile likageuka kuwa uhalisia wa gereza la Stanford. Wanyapara ghafla waligeuka madikteta kweli, wababe, wasio na soni wala hawa, wasiojali hisia za wafungwa, wakiwanyanyasa kwa amri na mateso makubwa.

Wafungwa nao ghafla maigizo yakageuka ukweli, wakaonesha dalili zote za sonona, ile tabia ya ‘fanya-lolote-na-sijali’ (helplessness) na wengine waligeuka kuwa waasi dhidi ya wanyapara. Baadhi ya wafungwa walipitia ukatili mkubwa wa kihisia.

Philip Zimbardo alihitimisha kuwa mazingira na hali tunazolazimika kupitia kama sehemu ya majukumu yetu, yana nguvu kubwa ya ‘kuunda’ tabia mpya zinazoweza kuzidi hata nguvu ya nasaba katika tabia.

Mazingira ya gereza yaliyowapa wanyapara uwezo wa kuonesha wana nguvu dhidi ya wenzao, kwamba wanaweza kufanya chochote na hakuna kitu wale wafungwa wangefanya, yaliwageuza watu hawa waliokuwa wema mwanzoni kuwa wakatili kweli, wenye tabia zisizo na utu wala ubinadamu.

 Kadhalika, mazingira hayo hayo ya gereza yaliyowaweka wafungwa kwenye upande wa ‘wanyonge’ yaliwafanya wajifunze kukubali kutii, kupitia madhila ya sonona, na hata kuchochea uasi, kwa maana ya kutaka kushindana na wanyapara wa gereza.

Tafsiri

Ukatili katika jamii, mara nyingi, ni matokeo ya mashindano ya tabaka linalotaka kulinda mamlaka yake na tabaka linalolazimishwa kutambua mamlaka hayo. Unapokuwa na pande mbili zenye nguvu na maslahi tofauti, kwa mfano, unachochea tabia za kikatili kwa namna mbili.

Kwanza, upande unaotaka kuonesha uwezo wake wa kuamuru, mabavu na nguvu za kuamua mustakabali wa wengine unajifunza tabia mpya ya ukatili dhidi ya wenzao. 

Upande wa pili usiokuwa na nguvu (wafungwa) unaokumbushwa umuhimu wa kutii, kufuata na kuheshimu nao unajifunza tabia za kupingana na mamlaka kama namna ya kujitetea, na hilo linaposhindikana upande huu huishia kujifunza unyonge na kujiaminisha kuwa hawana lolote wanaloweza kufanya kujitetea na nguvu za upande wa pili. Kwa msingi huo, chanzo cha tabia za ovyo katika jamii ni watu fulani kutaka kuthibitisha mamlaka yao dhidi ya wengine.

Tunachojifunza

Ukishaanza kujiona una nguvu dhidi ya mwenzako, una uhalali wa kubeza maumivu yake kwa sababu zozote zile, wewe tayari umeshakuwa muovu. Uovu, kwa kawaida,  unaanza na kujiona una haki ya kumuonea mwingine ikiwa ni pamoja na kubeza maumivu yake.

Upo uwezekano wa kuiga tabia za kikatili kwa watu tunaojitambulisha nao. Katika mazingira haya, tabia mbaya za kuumiza watu huanza kama mchezo wa kuigiza. Kamwe usibeze maumivu ya mtu kwa kujifariji kuwa unachofanya ni mzaha wa siasa, michezo au dini.

Pia, mazingira yanayokuza tofauti za kimamlaka baina ya watu kuanzia kwenye ngazi ya familia, yanaongeza uwezekano wa watu kujifunza tabia hatari kupitia majukumu yanayolenga kuthibitisha tofauti hizo za kimamlaka. Kujijengea matabaka kwa mfano tabaka la wenye nguvu na tabaka la wanyonge, kunahamasisha tabia za kikatili.

Hili lina maana kubwa katika malezi. Fikiria namna mtoto anavyoweza kujifunza ubabe kutoka kwa mzazi wake anayetumia mabavu kama mbinu ya kumrekebisha.

 Fikiria athari ya mamlaka makubwa ya mzazi yasiyodhibitiwa na hatari yake kwa tabia ya mtoto. Kuna umuhimu wa kuwa na mifumo madhubuti inayowafanya wazazi kutumia nafasi zao kuwalinda ustawi wa watoto na tishio lolote dhidi ya utu na ubinadamu wao.