Wanaodaiwa kusafirisha Heroine waiangukia mahakama

Muktasari:
Linda alikamatwa Aprili 17, 2019, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam (JNIA), akisafirisha dawa za kulevya aina ya Heroine ndani ya mabegi mawili yenye rangi ya udongo na nyeusi.
Dar es Salaam. Wakili wa Utetezi katika kesi ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin zenye uzito wa kilo 19, inayowabili raia watatu kutoka nchini za Lativia na Nigeria, Elipatra Ali, ameiomba Mahakama ielekeze upande wa mashtaka wakamilishe kusajili nyaraka muhimu Mahakama Kuu.
Wakili Ali ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Desemba 6 wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.
Washtakiwa katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi nipamoaja na Linda Mazure na Martins Plavins raia wa Lativia na Henry Ozoemena, raia wa Nigeria.
"Kesi hii ni ya muda mrefu, naomba Mahakama iwaelekeze upande wa mashtaka wawasilishe taarifa muhimu Mahakama Kuu ili kesi hii iweze kuendelea kwa hatua nyingine kwa sababu wateja wangu wanaendelea kusota rumande, bila kujua hatima yao," amedai Wakili Ally.
Awali, wakili wa Serikali, Adolf Verandumi, amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Rhoda Ngimilanga kuwa kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake bado haujakamilika.
Hakimu Ngimilanga baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote, aliutaka upande wa mashtaka kukamilisha mapema nyaraka hizo ili kesi iweze kuendelea kwa kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika.
Baada ya kueleza hayo, Hakimu Ngimilanga ameirisha kesi hiyo hadi Januari 15, 2023 itakapotajwa na washtakiwa wapo gerezani kutokana na shtaka la kusafirisha dawa halina dhamana kwa mujibu wa sheria.
April 7, 2021 washtakiwa hao walisomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo (Commital Proceedings) baada ya upelelezi wake kukamilisha.
Siku hiyo, upande wa mashtaka uliiele Mahakama hiyo kuwa wanatarajia kuwa na mashahidi 18 na vielelezo 6, ambavyo vitatolewa Mahakama Kuu, Divesheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu uchumi.
Washtakiwa hao baada ya kusomewa maelezo hayo, kesi yao ilihamishiwa Mahakama Kuu wakisubiria kupangiwa tarehe kwa ajili ya kuanza kusikilizwa.
Hata hivyo, mapema mwaka huu, washtakiwa hao waliridishwa Mahakama ya Kisutu na kufitiwa mashtaka yao na kisha kufunguliwa kesi nyingine yenye mashtaka kama hayo.
Huo ni utaratibu wa kawaida kwa upande wa mashtaka kufuta kesi na kuwafungulia nyingine iwapo watabaini kuna kasoro za kisheria katika kesi husika.
Katika mashtaka yao, Linda alikamatwa Aprili 17, 2019, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam (JNIA), akisafirisha dawa za kulevya ndani ya mabegi mawili yenye rangi ya blauni na nyeusi.
Akiwa JNIA, eneo la kuondokea ndege, alipitisha mabegi yake kwenye mashine ya kukagulia mizigo na ndipo mkaguzi alipoyatilia shaka baada ya kuona vitu visivyo vya kawaida kupitia mashine hiyo.
Baada ya mabegi hayo kupita Linda alijitokeza kuyachukua na ndipo mlinzi alipomtaka asubiri kwanza na baadaye aliamuliwa kufungua mabegi hayo ili yakaguliwe tena.
Linda alifanya hivyo na kutoa vitu vyote ikiwemo nguo zake kisha mabegi hayo yakiwa matupu yalipitishwa tena katika mashine na mashine iliendelea kubaini kuwepo vitu vingine na ndio ilipoamliwa mabegi hayo kuchanwa na kukutwa na kiasi hicho cha heroin.
April 19, 2019 alikamatwa Plavins eneo la Kariakoo Dar es Salaam na alikiri kumsafirisha Linda kutoka Lativia kuja Tanzania kuchukua dawa hizo za kulevya na walikuwa wakiishi wote King's Hotel.
Muda mfupi baadaye, alikamatwa, Ozoemena na katika mahojiano na jeshi la polisi alikiri kumpatia Linda bengi moja lilikuwa na dawa za kulevya aina ya heroin zenye uzito wa kg 15, wakati walipokutana na Plavins hotelini.
Mbali shtaka la kusafirisha dawa za kulevya, Ozoemena anakabiliwa na shtaka la kuishi nchini bila kuwa na kibali kwani aliingia nchini Julai mosi, 2017 na wakati anakamatwa kibali chake cha matembezi kilikuwa kimeisha muda mrefu.