Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwamposa: Pasaka ni baraka, tuombee amani uchaguzi unapokaribia

Muktasari:

  • Mtume Mwamposa amesema Pasaka maana yake ni wokovu, uponyaji, ushindi, maangamizo na amani

Dar es Salaam. Mtume Boniface Mwamposa wa Kanisa la Inuka Uangaze ametoa wito kwa Watanzania kuliombea Taifa liwe na amani kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, 2025.

Amesema Pasaka maana yake ni wokovu, uponyaji, ushindi, maangamizo na amani, hivyo katika Taifa la Tanzania kitu pekee cha kulilinda ni amani.

Amesema hayo leo Aprili 20, 2025 kwenye ibada maalumu ya Pasaka iliyofanyika Kawe, jijini Dar es Salaam yalipo makao makuu ya kanisa hilo.

"Tutaendelea kuliombea Taifa, kila mmoja ainue Taifa kwa maombi, Yesu anaitwa mfalme wa amani na ukiona tumekaa hivi na kusherehekea kufufuka kwa Yesu basi Mungu ametupa amani," amesema.

Amesema kuna watu hawawezi kukaa kwa pamoja kusali kwa sababu hawana amani, hivyo amewataka waumini kufanya maombi ili Mungu awape amani kwenye familia zao.

Mwamposa amesema amani huwa inatembea, inaweza kukaa inaweza kuondoka na Yesu aliwaambia wana wa amani wakiingia nyumba yoyote waseme amani iwepo ndani ya nyumba hiyo na akiwepo mwana wa amani ndani lazima amani itakaa, asipokuwepo itaondoka kwa maana inatembea na inahitaji kiti cha kukaa.

Kwa mujibu wa Mwamposa, kipindi cha uchaguzi kinakuwa na mambo mengi na adui ndipo anapofungulia malango ya aina mbalimbali ya makabila na dini, hivyo ametaka wawe sehemu ya amani katika Taifa.

"Tunamshukuru Mungu kwa Taifa letu naendelea kuliombea amani na tukaendelee kuilinda amani na Mungu atatupa Neema. Tuendelee kufanya maombi hadi pale uchaguzi utakapomalizikia ili kuendelea kudumisha amani iliyopo," amesema.

Kwa upande wao waumini wamesema leo ni siku yao maalumu kwa ajili ya kufunguliwa mioyo yao ili kuishi kwa amani.

"Kwa wale wenye jicho lingine na fikra nyingine wanaweza kuona Mungu alivyomtumia Mtume kutueleza namna ya kuishi kwa amani na kuepuka yale ambayo siyo yetu tunatakiwa tuachane nayo," amesema Johnson Saku, muumini wa kanisa hilo.

Amesema kuna watu wapo kwa ajili ya kuharibu amani za watu kwenye familia ili kuwe na mifarakano, akieleza hayo ni mapepo yanayojiinua kwa njia mbalimbali ili kuangamiza nyumba zenye amani.

Mkazi wa Gongo la Mboto, Christina Paulo amesema mahubiri yanaeleza maisha halisi wanayoishi, akisema adui amekuwa akijiinua kuharibu amani iliyopo.