Wanaodaiwa kughushi fomu ya mirathi waomba kufutiwa kesi
Mshtakiwa Seleman Said na Betha Laurence, wanaokabiliwa na mashtaka ya kughushi fomu ya mirathi, wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Picha na Hadija Jumanne
Muktasari:
- Washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa yao kati ya Aprili 18, 2008, Desemba 1, 2009 na Agosti 21, 2015, jijini Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Upande wa utetezi katika kesi inayomkabili mfanyabiashara, Seleman Said, na Betha Laurence, umeiomba Mahakama iwafutie kesi na kuwaachia huru wateja wao kwa madai kuwa Jamhuri haionyeshi nia ya kuendelea na shauri hilo.
Said na Laurence wanakabiliwa na mashtaka 16, likiwemo la kughushi na kutakatisha fedha.
Mawakili wa washtakiwa hao, Ally Jamal akishirikiana na Adii Kiiza, wametoa maelezo hayo leo Julai 28, 2026, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, kesi hiyo ilipotajwa.
Wametoa ombi hilo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Rahimu Mushi, baada ya wakili wa Serikali, Godfrey Olugwey, kuiomba mahakama hiyo iwape ahirisho fupi ili waweze kuwaleta washtakiwa wengine kutoka Wizara ya Ardhi kwa ajili ya kuunganishwa katika kesi hiyo.
Alidai tayari wameshapeleka hati za wito, hivyo wanaamini kikao kijacho watafikishwa mahakamani.
Ndipo wakili Jamal, pamoja na mambo mengine, alidai kuwa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai inataka upelelezi ukamilike ndipo washtakiwa wafikishwe mahakamani, hasa kwa makosa yasiyo makubwa kama yanayowakabili wateja wake.
Alidai upande wa mashtaka haujatoa sababu ya msingi ya kutowafikisha mahakamani washtakiwa waliobaki, hivyo wateja wao hawapaswi kuwajibika kwa makosa ya watu wengine.
"Sheria ya jinai inataka upelelezi ukamilike kwanza ndipo kesi ifunguliwe. Kesi hii ilipaswa ifunguliwe na kusikilizwa mara moja. Washtakiwa wengine wamepatikana au la, si jukumu la washtakiwa," alidai wakili Jamal.
"Kwa kuwa upande wa mashtaka hauna nia ya kuendelea na kesi, tunaomba iondolewe ili, wakiwa tayari, watawafungulia upya mashtaka yao. Kinachoonekana hapa haki haitendeki," aliongeza.
Akijibu hoja za upande wa utetezi, wakili Olugwey alidai kuwa tayari wameshapeleka barua ya wito Wizara ya Ardhi na wanachosubiri ni watu hao kufikishwa mahakamani ili waunganishwe na wenzao.
Hakimu Mushi, baada ya kusikiliza hoja za pande zote, aliutaka upande wa mashtaka kwamba tarehe ijayo waletwe mahakamani washtakiwa waliobaki au waendelee na kesi dhidi ya washtakiwa waliopo mahakamani.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 11, 2026, kwa ajili ya kutajwa. Mshtakiwa Said amerudishwa rumande kwa sababu anakabiliwa na shtaka la kutakatisha fedha, ambalo halina dhamana kwa mujibu wa sheria.
Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Juni 5, 2026, na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka 16.
Kati ya mashtaka hayo, sita ni ya kughushi, sita ni ya kuwasilisha nyaraka za uongo, moja ni la kushiriki kufanya ukaguzi wa nyaraka hizo na kujipatia usajili wa ardhi, pamoja na shtaka la kutakatisha fedha linalomkabili mshtakiwa Said pekee.
Katika kesi ya msingi, Said na Betha wanakabiliwa na mashtaka sita ya pamoja ya kughushi nyaraka, tukio wanalodaiwa kulitenda Aprili 18, 2008, jijini Dar es Salaam.
Inadaiwa walighushi mkataba wa mauziano kwa lengo la kuonyesha kuwa Seleman Said amenunua kiwanja namba 212, eneo la Kinondoni, kwa thamani ya Sh20 milioni, wakijua si kweli.
Pia wanadaiwa kughushi kiapo kinachoonyesha kuwa Ramadhani Mussa, Rehema Mussa, Mwanahamisi Mussa na wenzao waliridhia kumuuzia kiwanja hicho.
Nyaraka nyingine wanazodaiwa kughushi ni fomu za mirathi namba 1, 2, 3 na 4 zilizomhusu marehemu Mussa Kondo Majenga.
Pia, Said anakabiliwa na mashtaka mengine sita ya kuwasilisha nyaraka hizo za kughushi kwa Ofisa Ardhi wa Manispaa ya Kinondoni, Romanus Sanda.
Ilidaiwa kuwa Said, akiwa na maofisa wengine wa ardhi, alishiriki ukaguzi wa nyaraka hizo za kughushi zilizotumika kusajili ardhi na kutoa hati ya ardhi namba 1003 kwa jina lake.
Vilevile, Said anadaiwa kuwa Juni 27, 2008, akiwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, iliyopo Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, alijipatia usajili wa hati ya kumiliki ardhi namba 105525 kutoka kwa Msajili wa Ardhi akijifanya alinunua ardhi hiyo kutoka kwa Moshi Majenga, akijua si kweli.
Said pia anadaiwa kuwa kati ya Desemba 1, 2009 na Agosti 21, 2015, katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Ardhi, alitoa ushahidi wa uongo katika shauri la ardhi namba 62 la mwaka 2019 kwamba alinunua ardhi hiyo kutoka kwa Moshi Majenga, wakati akijua si kweli.
Pia, Said anakabiliwa na shtaka la kutakatisha fedha, akidaiwa kuwa Agosti 1, 2008, alijipatia ardhi hiyo huku akijua ilitokana na kosa tangulizi la kughushi.