Wanane wafa, sita wajeruhiwa ajalini Kigoma

Kigoma. Watu wanane wamefariki dunia akiwemo mtoto wa umri wa mwaka mmoja na nusu na wengine sita wamejeruhiwa katika ajali iliyohusisha magari mawili katika Barabara ya Kibondo-Kakonko mkoani Kigoma.
Ajali hiyo iliyotokea jana Desemba 23, 2023 saa 11:30 jioni katika Kijiji cha Mumkungwa, Kata ya Misenzero, ilihusisha gari aina ya Toyota Probox lililokuwa na abiria na jingine la Kampuni Chiko inayojenga barabara.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye amesema leo Jumapili Desemba 24, 2023 kuwa majeruhi wapo katika Hospitali ya Wilaya ya Kibondo kwa matibabu.
Amesema baada ya uchunguzi, majeruhi watatu kati ya sita wameumia zaidi, hivyo watapewa rufaa kwenda Hospitali ya Kanda, Bugando iliyopo mkoani Mwanza na watatu wanaendelea na matibabu hospitalini hapo.
“Nitoe wito kwa watumiaji wa vyombo vya moto, wahakikishe wanachukua tahadhari wanapokuwa barabarani kwa kipindi hiki cha msimu wa sikukuu, kwani ni jambo la kila mmoja wetu tukishirikiana kutokomeza ama kupunguza ajali, ambazo sababu ni uzembe wa madereva,”amesema Andengenye.
Anden genye amewataja watu waliopoteza kuwa maisha ni pamoja na dereva wa gari ndogo maarufu mchomoko, Hamisi Chaurembo, Bernadina Reuben, Maduha Asukile, Ntinganiza Bihezako, Vedastus Paulo na wengine hawajatambulika.
Mkuu wa mkoa amesema majeruhi sita ni pamoja na dereva Chiko, Flavianus Felician (28), Juma Said (27), Daniel Samwel (33), Silvanus Muhigwa (43), Sara Bundala (20) na Dorice Mafumbo (22).
Miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kibondo na chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi na dereva wa Probox kutaka kupita gari iliyokuwa mbele yake kwenye kona.