Makosa ya kibinadamu, uzembe vyachangia ajali barabarani

Muktasari:
- Makosa ya kibinadamu yametajwa kuwa chanzo cha ajali zinazojitokeza mara kwa mara hasa katika msimu wa kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka
Dar es Salaam. Mkuu wa Kikosi cha Usalama wa Barabarani nchini, Kamanda Ramadhani Ng’anzi amesemaa makosa ya kibinadamu yanayojitokeza mara kwa mara ni miongoni mwa sababu za ajali za barabarani.
Amesema hayo wakati akichangia mjadala wa Mwananchi Space jana uliokuwa na mada ya ‘Nini suluhisho kukithiri kwa ajali kila mwisho wa mwaka?’
“Binadamu kama alivyo yeye mwenyewe anakuwa chanzo kikuu cha ajali barabarani, kwanza ni uzembe wa kutofuatilia vitu au kutofanya vinavyotakiwa kufanywa na vile anavyokatazwa anavyovifanya,” amesema Kamanda Nga’anzi.
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, jumla ya ajali 46 zilizoripotiwa kati ya Desemba mosi na 12 mwaka huu, vimesababisha vifo vya 46 huku 59 wakijeruhiwa
Kamanda Ng’anzi amesema sababu nyingine ya ajali za barabarani ni mwendokasi unaobabisha dereva kushindwa kufanya uamuzi wa haraka pindi linapotokea jambo la ghafla au dharura.
“Vitu vingine ni watu kuendesha magari wakiwa na kiwango kikubwa cha ulevi, wakati sheria inatakataza kuwa dereva wa magari ya umma kuwa na kiwango chochote cha pombe ndani ya damu yake,” amesema Kamanda Ng’anzi.
Kuhusu Sheria ya Usalama Barabarani, amesema wamepeleka marekebisho kuiongeza meno ili wakosaji wapate adhabu watakayojutia.
Awali, akifungua mjaladala huo, mwandishi wa Gazeti la Mwananchi, Tuzo Mapunda, amesema miongoni mwa vichochezi vya ajali za mwisho wa mwaka ni magari binafsi kutembea umbali mrefu huku dereva mmoja, tofauti na usafiri wa umma.
“Watu wengi hawana uzoefu wa kuendesha gari kwa mwendo mrefu, mwisho wa siku wanachoka na kusababisha ajali. Lakini kisababisha kingine ni baadhi ya watu kupuuza sheria za usalama barabarani.
“Chanzo ni kingine ni makosa ya kibinadamu hasa uzembe wa madereva wa kutotii kanuni zilizowekwa, utakuta mtu anakunywa pombe kabla ya kuanza safari hali inayosababisha kutofanya uamuzi sahihi barabarani,” amesema.
Gervas Michael amesema miongoni mwa sababu za ajali ni utoaji wa leseni za udereva, akisema kuna shida hasa wale wa wanaondesha magari ya abiria.
“Nilikuwa nashauri hili la kusababisha ajali kwa uzembe, endapo dereva akibainika basi anyang’anywe leseni na asipewe tena kutokana na ukubwa wa tatizo baada ya trafiki kupima,” amesema Michael