Wanafunzi vyuo vikuu kuacha masomo kwamshtua mbunge, aitaja bodi ya mikopo
Muktasari:
- Mbunge wa Ngara (CCM), Ndaisaba Ruhoro ameitaka Serikali ichunguze kwa haraka wanafunzi wa vyuo vikuu walioacha masomo kwa kukosa mikopo na kuwasaidia wamalize masomo yao.
Dodoma. Mbunge wa Ngara (CCM), Ndaisaba Ruhoro ameitaka Serikali kufanya uchunguzi wa haraka kuwabaini wanafunzi wa vyuo vikuu walioacha masomo kutokana na kukosa mikopo na kuwasaidia wamalize masomo yao.
Amesema hayo jana Jumatano Aprili 3, 2024 wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zake kwa mwaka 2024/25.
Ameipongeza Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) na Serikali kwa kuongeza bajeti ya mikopo ya elimu ya juu, lakini kuna kundi la Watanzania ambao hawamalizi elimu ya vyuo vikuu kama ilivyo kwa elimu ya msingi na sekondari nchini.
Amesema hivi sasa kuna mdondoko wa wanafunzi wa vyuo vikuu na kwamba wabunge wengi wanaombwa kuwasomesha wanafunzi walio vyuo vikuu.
“Ukiuliza ile habari unaambiwa mtoto alikosa mkopo na baada ya kukosa kuna wazazi wanauza mifugo mwenye ng’ombe anauza, mwenye kuezua nyumba anaezua. Kwa bahati mbaya wazazi wengi hawatoboi miaka mitatu ama minne,”amesema.
Amesema matokeo yake unakuta mwananchi wa kijijini ameuza mali zake, lakini watoto hawajamaliza vyuo vikuu wanarudi nyumbani.
Ndaisaba ameomba Serikali kufanya uchunguzi wa haraka kuwabaini wanafunzi walioshindwa kumaliza vyuo vikuu na kushauri HESLB kuwapa mikopo wanafunzi hao, ili wamalize vyuo.
Amesema lipo kundi kubwa lenye changamoto hiyo na kwamba jana kuna wazazi sita walifika nyumbani kwake kuomba msaada wa ada kwa watoto wao walioko vyuoni.
“Hii ni kero kubwa kwa wabunge wengi kwa sababu wazazi wanahisi sisi tuna mifuko tunaweza kuchukua fedha ya kuwasaidia watoto wao wakamaliza vyuo vikuu. Sasa kundi hili naomba lihudumiwe, litafutwe linajulikana,”amesema.
Amesema wapo wanaoandika barua ya kushindwa kuendelea na masomo na hivyo kurudi nyumbani kukaa kwa kukosa mikopo ya kuendelea na masomo.
Amewataka Serikali kwenda katika vyuo vikuu kuwakusanya wanafunzi walioacha masomo kutokana na kukosa mkopo na kuwasaidia, ili waweze kumaliza masomo yao.
“Naomba hili jambo mlipe kipaumbele kwa sababu watu wanalalamika na kuna kundi limeachwa, naomba Watanzania hawa wasaidiwe,” amesema.