Wanafunzi 'feki' 17 wanaswa wakifanya mitihani chuo kikuu

Moja ya jengo la Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT).

Muktasari:

  • Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT) kimesema watuhumiwa wanatoka vyuo vingine, pia wapo wafanyakazi nje ya chuo.

Dar es Salaam. Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kimewakamata watu 17 wakijaribu kuwafanyia mitihani wanafunzi wa chuo hicho.

Waliokamatwa imeelezwa walikuwa na vitambulisho vya kughushi na tiketi ya ukumbi wa mitihani.

Kwa mujibu wa OUT watuhumiwa wamekatwa kuanzia Juni 18, 2024 katika vituo vya mitihani vya Ilala na Kinondoni.

Watuhumiwa hao imeelezwa wapo mikononi mwa Jeshi la Polisi.

Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Elifas Bisanda ameeleza hayo kupitia taarifa iliyotolewa na Idara ya Mawasiliano OUT leo Juni 28, 2024.

Profesa Bisanda amesema chuo kilianza mitihani Juni 3 hadi 24, na wanafunzi  10,417 waliandika mitihani katika vituo 53, ambavyo vimesambaa nchi nzima.

"Katika kipindi cha wiki tatu za mitihani, kwa umakini wa mifumo yetu, wasimamizi wa mitihani waliwakamata mamluki wapatao 17, hususani katika vituo vya Ilala na Kinondoni, Dar es Salaam. Matukio mengi yalibainika kuanzia Juni 18," amesema Profesa huyo.

Amesema kitendo cha watu hao kughushi vitambulisho vya chuo na tiketi ya ukumbi wa mitihani ni vitendo vya jinai, hivyo sheria ichukue mkondo wake. 

Amesema waliokamatwa siyo wa chuo hicho, bali ni kutoka vyuo vingine na wengine ni wafanyakazi katika fani walizosomea.

Mmoja wa wanafunzi wa chuo hicho mwaka wa tatu (jina linahifadhiwa) amesema ameshuhudia tukio la kijana mmoja aliyekamatwa na msimamizi kwenye chumba cha mtihani, aliyejaribu kukimbia.

"Tuliona purukushani huyo kijana alipokonywa kitambulisho alipopata upenyo akataka kukimbia, huyo angepata nafasi angetokea dirishani maana wasimamizi wanne walimshika kumzuia asikimbie hatukuelezwa kitu bali msimamizi alituambia endeleeni na mitihani," amesema.

Kuhusu hatua zitakazochukuliwa kwa  waliowatuma, Profesa Bisanda amesema chuo kina sheria na kanuni za mitihani ambazo zitatumika kuwashughulikia.

"Mamlaka za chuo zitawahoji wahusika na wakikutwa na hatia, basi wataadhibiwa kulingana na kanuni," amesema.

Kwa waliofikishwa Polisi, amesema hataridhika kuambiwa wanaendelea na upelelezi, kwani maofisa wa Usalama wa Taifa walishuhudia matukio hayo hivyo hayahitaji upelelezi zaidi.

Amesema taarifa ataifikisha makao makuu ya Jeshi la Polisi, Ofisi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi na Ofisi ya Rais kwa ajili ya ufuatiliaji.

Ili kukomesha vitendo vya namna hiyo, Profesa Bisanda amesema OUT ipo kwenye maandalizi ya kuwasajili wanafunzi wote kwa alama za vidole, na kumhakiki kila mtahiniwa kwa mashine maalumu za utambuzi wa alama za vidole katika vituo vyote vya mitihani.


Usalama wa mitihani 

Profesa Bisanda amesema OUT kimejijengea sifa kimataifa, kwa kuwa na mfumo madhubuti wa usalama wa mitihani.

"Chuo kimeweza kutumia wataalamu wake wa Tehama, kujenga mfumo wa mitihani, ambao ni vigumu sana mtihani kuvuja. Hata mwalimu anayefundisha somo fulani, hajui wanafunzi wake wataulizwa maswali gani. Anakutana na maswali hayo, wanafunzi wakishamaliza kuandika mtihani, na ndipo anaandaa utaratibu wa kuusahihisha," amesema.