Mkenda ataka vyuo vikuu kujikita kwenye tafiti gunduzi

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda akiwa na wajumbe wa Baraza jipya la Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (Out) 2023/2026
Muktasari:
- Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, ametoa wito kwa vyuo vikuu kuzingatia ufanyaji wa tafiti zenye tija ili kuchochea na kuleta ushindani katika gunduzi mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Dar es Salaam. Ilikuchochea na kuleta ushindani katika gunduzi mbalimbali, vyuo vikuu nchini vimetakiwa kuzingatia ufanyaji wa tafiti zenye tija, kwani havipimwi kwa wingi wa wanafunzi, ufanyaji wa tafiti zenye kuleta gunduzi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa baraza jipya la Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (Out) la 2023/2026 jijini Dodoma, leo Jumanne Oktoba 10, 2023; Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema ni vema chuo kikuu kiwe chemchemu ya kuvumbua na kutafuta majibu ya matatizo ya wananchi.
“Chuo Kikuu ni mahali pa kuzalisha wataalamu na wabobezi ambao wakitoka wanakwenda kufanya kazi za kutoa huduma kwa wananchi na kukuza uchumi kupitia sekta mbalimbali,” amesema Profesa Mkenda na kuongeza;
“Tafiti zinazofanywa na vyuo vyetu ni vyema zikashindanishwa kimataifa ili ziweze kuwa na viwango vya ubora zaidi katika nyanja za kimataifa, hii itavifanya vyuo vyetu viwe na uwezo wa kufanya kazi na watu wa mataifa mbalimbali duniani,” amesema Profesa Mkenda.
Amesema kuwa hivi karibuni wizara hiyo imetoa tuzo na fedha kwa watafiti ambao wamechapisha matokeo ya tafiti zao katika majarida ya kimataifa kama motisha, lakini pia kuwafanya watafiti wa Tanzania kushindana Kimataifa.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mwenyekiti wa Baraza hilo, Profesa Joseph Kuzilwa, amemuhakikishia Profesa Mkenda kuwa baraza lililoteuliwa ni la watu wenye taaluma na ujuzi wa kutosha kuweza kulisongesha mbele gurudumu la chuo hicho.
“Timu hii ya wajumbe itakuwa ni chachu kubwa katika kuchangia ufanisi wa baraza kwenye kusimamia chuo kwa mujibu wa majukumu yaliyoainishwa katika hati idhini ya chuo ya mwaka 2007, sheria ya vyuo vikuu ya mwaka 2005 na waraka namba moja wa msajili wa hazina wa mwaka 2023,” amesema Profesa Kuzilwa.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo hicho Profesa Elifas Bisanda, amesema baraza hilo limepata fursa ya kupata mafunzo ya siku tatu ambapo wawezeshaji watatoa mada mbalimbali zitakazowawezesha wajumbe kujenga uwezo zaidi ili waweze kufanya kazi na kutimiza wajibu wao vizuri.
“Utendaji wa baraza hili utapimwa na ofisi ya msajili wa hazina kila mwisho wa mwaka, ndiyo maana tumekaa pamoja ili wajumbe waweze kujua vizuri wajibu, taratibu, haki na mamlaka waliyonayo ili waweze kufanya kazi kwa kukidhi matakwa ya sheria na kanuni zilizopo kuhusu utendaji wa bodi na mabaraza yaliyoko chini ya serikali.” amesema Profesa Bisanda.