Prime
Hizi hapa njia za kufanya mshahara utoshe
Muktasari:
- Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa asilimia 93 ya watu wanaofanikiwa katika maisha ni wale wanaoishi kwenye bajeti walizojiwekea.
Dar es Salaam. Wakati gharama za maisha na mahitaji ya kila siku vikiendelea kupanda, mishahara ya watu wengi imeendelea kuonekana midogo kutokana na kubeba majukumu mengi zaidi.
Kodi ya nyumba, usafiri, chakula, ada za watoto, huduma za afya, bando la intaneti na malipo ya mikopo ni miongoni mwa matumizi yanayogombea kipato kilekile cha mwezi, ambacho wakati mwingine hakiongezeki kwa kipindi kirefu, licha ya kupanda kwa gharama hizo za maisha.
Wataalamu wa fedha wanasema changamoto hiyo inaweza kupunguzwa kwa kuandaa bajeti kulingana na kipato cha mtu husika, hatua ambayo kwa wengi ni ngumum lakini inaweza kuwasaidia kutumia vizuri kile wanachopata, kufanya mshahara ukidhi mahitaji na kuepuka madeni yasiyokuwa ya lazima.
Mkufunzi wa biashara na bajeti, Charles Mtega anasema tafiti zinaonyesha kuwa asilimia 93 ya watu wanaofanikiwa maishani ni wale wanaoishi kwa kufuata bajeti walizojiwekea kwa sababu huwa na malengo ya matumizi yao.
Anasema miongoni mwa sababu zinazowafanya watu washindwe kufuata bajeti walizojiwekea, hasa mwanzoni mwa mwaka, ni matamanio ya matumizi na tabia ya kutembea na fedha nyingi mfukoni.
Hali hiyo huwafanya baadhi ya watu kutumia fedha ambazo walikuwa tayari wamezitenga kwa ajili ya majukumu mengine.
"Mtu ameweka bajeti lakini anataka kutembea na fedha. Ili kukabiliana na hali hiyo ni vyema kuhakikisha unakuwa na kiwango maalumu cha misaada unayotoa, kujua makundi ya watu wanaokuzunguka na kujizuia kuiga matumizi ya marafiki. Hilo litakusaidia kutunza fedha," anasema.
Anasema ili mtu afanikiwe ni lazima aishi chini ya kile anachokipata na si juu ya kipato chake, jambo ambalo linawezekana kwa kupanga bajeti kulingana na mapato ya kila mwezi.
Mfano wa bajeti
Mtega anasema mtu asiye na bajeti anaweza kuingiza Sh6 milioni lakini matumizi yake yakafikia Sh7 milioni, huku mwenye bajeti akiwa na uwezo wa kupokea Sh800,000, akatumia Sh600,000 na kutunza Sh200,000 kama akiba.
"Bajeti humsaidia mtu kuwa na nidhamu ya matumizi muhimu na kuepuka kutumia fedha nje ya mipango yake," anasema.
Anatoa mfano wa mtu mwenye kipato cha Sh450,000 kwa mwezi, akisema fedha hizo zinaweza kukidhi mahitaji muhimu na kumwezesha kuweka akiba ya Sh40,000.
Anaeleza katika bajeti hiyo, Sh50,000 inaweza kutengwa kwa kodi, Sh150,000 kwa chakula, Sh60,000 kwa usafiri, Sh20,000 kwa umeme na maji, Sh20,000 kwa mawasiliano, Sh40,000 kwa sadaka na michango, Sh20,000 kwa matumizi ya dharura na Sh40,000 kwa akiba au mtaji.
Hata hivyo, amesema: "Bajeti hii inawezekana zaidi kwa mtu anayeishi kwenye maeneo yenye kodi ndogo," anasema.
Kwa anayepata Sh700,000 baada ya makato, Mtega anashauri kutenga Sh70,000 kwa sadaka, Sh135,000 kwa chakula, Sh80,000 kwa kodi, Sh15,000 kwa umeme na maji, Sh20,000 kwa mawasiliano, Sh30,000 kwa usafiri, Sh110,000 kwa starehe, Sh60,000 kwa matumizi binafsi, Sh40,000 kwa akiba ya bima, Sh50,000 kwa akiba ya dharura na Sh50,000 kwa akiba ya malengo.
Kuepuka mikopo
Kwa upande wake Mtaalamu wa elimu ya fedha, Ladislaus Louitas, anasema kuishi kwa bajeti humsaidia mtu kuepuka mikopo isiyokuwa ya lazima, ambayo mara nyingi hutafutwa kuziba pengo lililosababishwa na matumizi yasiyopangwa.
"Mtoto anaweza kuumwa akahitaji dawa ya Sh3,000 tu. Kwa sababu hukuwa na bajeti, unaanza kuhangaika kukopa. Tayari hilo ni deni ambalo halikuwa na ulazima. Kama ungekuwa umeweka hata Sh20,000 kwa dharura usingepata shida," anasema.
Anasema watu wengi wanaishi kwa mazoea badala ya kupanga matumizi yao.
"Bajeti itakupunguzia aibu ndogondogo za kuomba kiwango kidogo cha fedha ambacho unadhani mtu hawezi kukunyima, halafu akakwambia hana. Unaweza kuanza kumchukia ukidhani ni mchoyo, wakati wewe ulikuwa na uwezo wa kutunza fedha zako," anasema.
Anaeleza watu wasiokuwa na bajeti hata kulipa madeni huwa ni changamoto kwa sababu fedha zote huishia kwenye matumizi ambayo hayakuwa yamepangwa, hivyo kukosekana fungu maalumu la kulipa madeni.
Tatizo liko wapi?
Baadhi ya wananchi wanasema kinachoharibu bajeti zao ni kushindwa kudhibiti matamanio ya kununua vitu ambavyo havikuwa kwenye mipango yao, zikiwemo vocha (bando), nguo na mahitaji ya nyumbani.
Katika hilo, Mkazi wa Tabata, Shany Marwa amesema kwa sasa matumizi ya intaneti yamekuwa sehemu ya maisha ya kila siku.
"Kwa sasa simu ndiyo kila kitu. Ikiisha salio ni vigumu kukaa bila kuwa mtandaoni kwa sababu hata namna ya kuwasiliana, wengi wamehama kutoka kupiga simu za kawaida na kutumia WhatsApp. Hivyo kuwa na data limekuwa jambo muhimu sana," anasema.
Anasema changamoto nyingine ni tabia ya kununua vifurushi vya muda mfupi vinavyoisha haraka.
"Unanunua bando la siku tatu, ndani ya saa tatu limeisha. Unanunua bando la wiki moja, ndani ya siku moja limeisha. Unakuta fedha unayotumia ni nyingi, lakini si wengi wanaoweza kutenga Sh30,000 kwa kifurushi kikubwa cha mwezi," anasema.
Kwa upande wake, Mariam Juma anasema kusaidia ndugu na kufanya ununuzi wa vitu vya nyumbani ni miongoni mwa sababu zinazovuruga bajeti.
"Ukipigiwa simu unaona kabisa jambo hilo liko ndani ya uwezo wako, inabidi uangalie namna ya kutoa akiba usaidie. Kuna namna unaumia, lakini utafanyaje?" anasema.
Anasema ununuzi wa mahitaji ya watoto nayo huwafanya wengi kutumia fedha nje ya bajeti walizokuwa wamejiwekea.