Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waliotumia vyeti feki usaili JKT wanaswa Morogoro

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Fotunatus Musilimu akionesha baadhi ya vyeti vya kuzaliwa na vya kumaliza darasa la saba vilivyoghushiwa na vijana wawili na kuvipeleka kwenye usaili wa kujiunga na JKT. Picha Hamida Shariff

Muktasari:

Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linawashikilia vijana wawili kwa tuhuma za kughushi vyeti vya kuzaliwa pamoja na vya kuhitimu darasa la saba ambavyo waliviwasilisha kwenye usaili wa kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Morogoro. Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linawashikilia vijana wawili kwa tuhuma za kughushi vyeti vya kuzaliwa pamoja na vya kuhitimu darasa la saba ambavyo waliviwasilisha kwenye usaili wa kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Vijana hao ni, Donald Mayunga (18), mkazi wa Manispaa ya Morogoro na Hashim Hemed (18) mkazi wa Kijiji Dar es Salaam wamenaswa wakati wa usaili uliokuwa ukifanyika Bwalo la JKT Umwema Manispaa ya Morogoro.

Pia, jeshi la polisi linamshikilia mmiliki wa steshenari Mary Banzi (54), mkazi wa Kilakala Manispaa ya Morogoro kwa tuhuma za kushirikiana na vijana hao kughushi vyeti hivyo.

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Wakili Albert Msando ambaye alikuwa akisimamia usaili huo amesema Septemba 5, 2022 akiwa na kamati yake ya ulinzi na usalama ya wilaya vijana hao waliingia kwenye usaili na baada ya kuwauliza maswali na kukagua vyeti vyao aligindulika vyeti hivyo vimeghushiwa saini.

"Kwanza tulianza kumgundua Donald, alipoingia tu nikaanza kumuuliza umri wake na maswali mengine ambayo wakati anajibu nilimuona kama ameanza kutojiamini na kijasho chembamba kikaanza kumtoka.”

“Hali ile ilinipa wasiwasi mimi pamoja na wajumbe wangu wa kamati ya ulinzi wa usalama, nikaamua kuanza kuchunguza vizuri vyeti vyake na ndipo nilipogundua cheti kile lilitolewa mwaka 2004 lakini saini iliyokuwepo kwenye cheti ni ya msajili ambaye alianza kazi mwaka 2013," amesema Wakili Msando.

Amesema wakati anakagua cheti cha kuhitimu shule ya msingi pia aligundua cheti hicho kimeghushiwa, aliagiza kijana huyo akamatwe kwa ajili ya kuhojiwa ili kubaini uhalali wa vyeti hivyo.

"Wakati Donald anakwenda kuhojiwa nje ya chumba cha usaili nilitoka nje na kuwatangazia vijana waliokuja kwenye ule usaili kama kuna mwenye cheti au nyaraka yoyote ya kughushi asiingie kwenye chumba cha usaili na aondoke haraka,” amesema

“Lakini cha kusikitisha huyu kijana Hashim aliingia akiwa na vyeti vya kuzaliwa na vya kumaliza darasa la saba vya kughushi ambavyo navyo baada ya kuvikagua tukagundua namba za usajili wa vyeti hivi pamoja na saini zinafanana," amesema Msando.

Kutokana na hali hiyo, Msando amesema vijana hao walichukuliwa na kupelekwa polisi kwa ajili na mahojiano zaidi ambapo katika mahojiano hayo waliweza kumtaja Mary Banzi ndio aliyewatengenezea vyeti hivyo.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Fotunatus Muslim amesema baada ya kumkamata mmiliki wa steshenari polisi walikwenda kumpekuwa na kumkuta akiwa na vyeti 16 vya kuzaliwa, vyeti vinne vya darasa la saba na vyeti 13 vya kuhitimu kidato cha nne vikiwa na majina ya watu na vingine vikiwa havijaandikwa majina.

Amesema mmiliki huyo wa steshenari alikamatwa akiwa na mihuri 10 bandia ikiwemo mhuri wa msajili wa vizazi na vifo, afisa elimu mkoa wa Ruvuma, afisa elimu mkoa wa Kilimanjaro, Afisa elimu Wilaya ya Kongwa na wa mwalimu mkuu shule ya msingi Malali B.

Kufuatia tukio hilo, kamanda Musilimu amesema kuwa uchunguzi unaendelea kubaini mtandao huo wa watu wanaohusika na vitendo hivyo vya kughushi nyaraka na vyeti ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria huku akisema watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani mara baada ya uchunguzi kukamilika.