Waliokata nguzo ya Tanesco wakidai kutumwa na Mungu watupwa jela

Muktasari:
- Licha ya kuhukumiwa adhabu ya kulipa faini au kifungo cha miezi sita jela, mshtakiwa asema mahakama haina mamlaka ya kutoa hukumu kwa sababu mwenye haki ya kutoa adhabu ni Mungu pekee kwani alisikia sauti ya Mungu ikimwambia wakate nguzo hiyo.
Mufindi. Mahakama ya Wilaya ya Mufindi imewatia hatiani wanandugu watatu, katika kesi ya jinai, waliokuwa wakikabiliwa na shtaka la uharibifu wa mali kwa kuvunja nguzo ya umeme ya Shirika la Umeme (Tanesco), kwa madai ya kutumwa na Mungu.
Waliotiwa hatiani kwa kosa hilo, katika kesi hiyo ya jinai namba 11416 ya mwaka 2025 ni Emma Makombe (30), Shujaa Makombe (27) na Ruby Makombe (32) wote ni ndugu wa familia moja na wakazi wa Kijiji cha Nzivi, wilayani Mufindi mkoani Iringa.
Kutokana na hatia hiyo, mahakama hiyo imewahukumu adhabu ya kulipa faini ya Sh500,000 kila mmoja au kutumikia kifungo cha miezi sita Jela.

Hata hivyo, hawakuweza kulipa faini hiyo, hivyo wamepelekwa jela kuanza kutumikia adhabu ya kifungo mpaka pale watakapofanikiwa kulipa.
Wanafamilia hao walipandishwa kizimbani Jumatatu Mei 13, 2025 na kusomewa shtaka hilo na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Twide Mangula, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Benedict Nkomola.
Akiwasomea shtaka hilo, Wakili Mangula amesema kuwa Mei 6, 2025 katika Kijiji cha Nzivi wilayani Mufindi mkoani Iringa, washtakiwa hao kwa pamoja waliharibu nguzo ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) iliyopo karibu na nyumba yao kwa madai kwamba wametumwa na Mungu.
Wakili Mangula amesema kuwa walitenda kosa hilo la uhabirifu wa mali kinyume na kifungu cha 326 (1) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura 16, Marejeo ya Mwaka 2022.

Washtakiwa hao baada ya kusomewa shtaka hilo na kuulizwa na Hakimu Nkomola iwapo ni kweli walitenda kosa hilo au la, wote mmoja baada ya mwingine wamekiri kuwa ni kweli, huku wakidai kuwa walisikia sauti ya Mungu akiwaamuru kukata nguzo hiyo.
Kutokana na kukiri kwao kosa, ndipo Mahakama ikawatia hatiani kwa kosa hilo na kuwahukumu adhabu hiyo.
“Kwa kuwa washtakiwa baada ya kusomewa shtaka wamekiri kutenda kosa hilo, mahakama hii inawatia hatiani washtakiwa Emma Makombe, Shujaa Makombe, na Ruby Makombe kama walivyoshtakiwa," amesema Hakimu Nkomola wakati akisoma hukumu hiyo.
Kabla ya kutoa adhabu Hakimu Nkomola alitoa nafasi kwa pande zote, upande wa mashtaka kama wana kumbukumbu za nyuma za makosa yoyote ya jinai na washtakiwa kuomba shufaa (utetezi kupunguziwa adhabu).
Wakili Mangula ameieleza Mahakama kuwa hawana kumbukumbu za nyuma za makosa ya jinai kwa washtakiwa, lakini ameiomba Mahakana itoe adhabu kali kwa washtakiwa hao ili liwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.
“Niombe mahakama yako itoe adhabu kwa kuzingatia kifungu 326 (1) cha sheria ya kanuni ya adhabu sura 16 Marejeo ya Mwaka 2022 kwa washtakiwa hawa ili iwe fundisho kwa wengine," amesema Wakili Mangula.
Hata hivyo, washtakiwa kwa upande wao wote walisema kuwa mahakama haina mamlaka ya kutoa hukumu kwa sababu mwenye haki ya kutoa adhabu ni Mungu pekee kwani walisikia sauti ya Mungu ikiwambia wakate nguzo hiyo.
“Mahakama haina haki ya kutoa adhabu kwani Mungu pekee ndio mwenye mamlaka ya kutoa adhabu kwa wanadamu sisi tuliongozwa na Mungu kwamba umeme usiwepo kwenye eneo hili,” amesema Emma, huku na wengine nao wakitoa kauli hiyo hiyo, kila mmoja alipopewa nafasi hiyo.
Akizungumza na Mwananchi baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo mkazi wa Tanangozi, Manispaa ya Iringa, Blandina Kinemeu amesema kuwa amefika mahakamani hapo baada ya kusikia ndugu zake hao wameshtakiwa kwa kosa la kukutaa nguzo ya umeme ambayo ni mali ya Serikali.

Amesema kuwa ndugu zake hao wanadai kuwa walikata nguzo hiyo kwa sababu imani yao hairuhusu kuwa na umeme, huku akisema kwamba nguzo hiyo iliwekwa bila wao kushirikishwa katika jambo hilo.
“Baada ya kuona nguzo imewekwa walilala asubuhi yake wakadai kwamba wamepata kibali kutoka kwa Mungu kukata nguzo hiyo kutokana na imani yao namna ambavyo inawaambia,” amefafanua Kinemeu.
Kuhusu imani yao amesema ndugu zake hao hawana kanisa lolote ambalo wanakwenda kuabudu, lakini ibada zao wanazifanyia nyumbani kwao wakiwa wote hao watatu.
“Sisi kama familia tumeshangaa kuona hali hii inatokea kwa sababu zamani hawakuwa hivi. Tumeona baada ya mmoja wao Emma kwenda kufanya kazi Dar es Salaam alivyorudi kutoka huko ndipo wakaanza kuwa na imani hii kwa madai kuwa ametumwa na Mungu.” amesema Blandina.