Prime
Waliohukumiwa kunyongwa kwa mauaji ya mtalii Serengeti, meneja waachiwa huru

Muktasari:
- Kesi dhidi ya wawili hao na wengine ambao waliachiwa huru na Mahakama Kuu ya Tanzania iliyoketi Serengeti, walikuwa wakikanusha mashitaka hayo hadi Novemba 16, 2020 walipotiwa hatiani na kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa.
Mwanza. Mussa Daniel na Machenes Mniko waliohukumiwa adhabu ya kifo kwa madai ya kuvamia kambi ya watalii na kuwapora vitu mbalimbali na kuua watu wawili akiwemo mtalii Breckelman Eric, wameachiwa huru na mahakama.
Katika tukio hilo lililotokea Juni 20, 2012 saa 3:45 usiku katika kambi ya wageni ya Ikoma Tented Camp iliyopo kijiji cha Rubanda Wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara, watu hao walidaiwa kumuua pia meneja wa kambi hiyo, Renatus Robert.
Kesi dhidi ya wawili hao na wengine ambao waliachiwa huru na Mahakama Kuu ya Tanzania iliyoketi Serengeti, walikuwa wakikanusha mashitaka hayo hadi Novemba 16, 2020 walipotiwa hatiani na kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa.
Hata hivyo, walikata rufaa kupinga hukumu hiyo, kupitia rufaa namba 169 ya mwaka 2021 na baada ya kusikiliza sababu za rufaa, jopo la majaji watatu walikubaliana na sababu zao na kuamuru waachiliwe huru kutoka gerezani.
Ushahidi wa awali uliowatia hatiani ulidai kuwa siku ya tukio, watu wanne wakiwa na bunduki aina ya SMG na mapanga, walivamia kambi hiyo na kuwaua Eric na Robert kwa kuwapiga risasi kisha kupora vitu mbalimbali vya watalii.
Upelelezi ulifanyika ambapo watuhumiwa wanne walikamatwa ambapo Juni 25, 2012, makachero wa Jeshi la Polisi walimkamata mrufani wa kwanza, Mussa Daniel akiwa na fedha za kigeni zikiwemo Dola za Canada na Marekani na Euro.
Ushahidi unaeleza baada ya kukamatwa, alipelekwa Polisi na kuandika maelezo ya onyo ambapo ilidaiwa aliwataja washirika wengine akiwemo mrufani wa pili, Mniko ambapo Juni 27, 2012 aliwapeleka nyumbani kwa Mniko.
Huko ilidaiwa polisi walifanikiwa kukamata vitu mbalimbali vilivyoshukiwa kuporwa kwa watalii na wakisaidiwa na mkewe na kaka wa mrufani, walikamata kompyuta mkakato, simu, mabegi, memory card na vitu vingine.
Pia ilidaiwa polisi walikamata bunduki mbili, magazine moja na risasi sita ambapo bunduki aina ya SMG namba 10989 na namba IL4398L vyote vilitolewa mahakamani na kupokelewa kama kielelezo wakati wa usikilizwaji shauri hilo.
Halikadhalika upande wa mashitaka ulikabidhi maelezo ya mashahidi wawili, Steven Sebeki ambaye wakati kesi inasikilizwa alikuwa ameshafariki na Michael Sulzer, mtalii na raia wa Ujerumani ambaye alitambua vitu walivyoporwa.
Walivyojitetea kortini
Katika utetezi wake wakati kesi hiyo iliposikilizwa mbele ya Jaji Joachim Tiganga, mshitakiwa wa kwanza alikanusha kufanya tukio hilo lakini akaenda mbali na kuwakata washitakiwa wenzake akiwamo mshitakiwa wa pili, Machenes Mniko.
Alieleza kuwa alikuwa ameshitakiwa katika kesi nyingine ya jinai ambayo aliachiwa huru na akalalamikia kuteswa na polisi na akadai ni kutokana na mateso hayo, aliamua kuandika maelezo ya onyo na kukiri ili kuepuka kifo.
Kwa upande wake, mshitakiwa wa pili, naye alikanusha tuhuma dhidi yake na kueleza kuwa alikamatwa nchini Kenya Julai 10,2012 alipokuwa akiishi tangu mwaka 2009 baada ya kutoroka gerezani hapa nchini alikokuwa amefungwa.
Kama ilivyokuwa kwa mshitakiwa wa kwanza, naye alieleza namna alivyoteswa na polisi na baadae kupewa karatasi ambazo alizisaini na ili kuthibitisha uwepo wa mateso hayo, alitoa fomu ya polisi namba 3 (PF3) iliyomsaidia kutibiwa.
Baada ya kusikiliza ushahidi wa Jamhuri na ule wa utetezi wa washitakiwa, Jaji Tiganga aliwatia hatiani na kuwahukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa lakini wakakata rufaa kupinga hukumu hiyo wakiegemea katika hoja sita.
Hoja ya kwanza ni kuwa mahakama ilikosea kisheria pale ilipoegemea kanuni kuwa anayekutwa na mali iliyoibwa ndiye mtenda kosa na kupokea vitu vilivyotambuliwa na wamiliki wake (watalii) bila kufuata sheria ya ushahidi.
Halikadhalika walidai mnyororo wa kuhamisha vielelezo (chain of custody) ulivunjika, mahakama ilikosea kwa kutozingatia utetezi wao na kwamba wao ni waathirika wa ukamataji wa mali usiofuata kanuni wala kuzingatia sheria.
Pia wadai kutiwa kwao hatiani kulifanyika kimakosa kwa kuegemea maelezo ya ungamo (extra judicial statement) za warufani ambazo walidai zilipatikana na kupokelewa mahakamani kinyume cha sheria na shitaka halikuthibitishwa.
Hukumu ya jopo la majaji
Katika hukumu yao waliyoitoa Desemba 17, 2024, Rehema Kerefu, Abraham Mwampashi na Dk Eliezer Feleshi walisema baada ya kuchambua sababu za rufaa, wamekubaliana na sababu namba 1, 4, 5 na 6 kuwa zina mashiko.
Hoja ambazo mahakama imeziona zina mashiko ni pamoja na madai mahakama ilikosea kisheria pale ilipoegemea kanuni anayekutwa na mali iliyoibwa ndiye mtenda kosa na kupokea vitu vilivyotambuliwa na wamiliki wake (watalii) bila kufuata sheria ya ushahidi.
Majaji hao walisema kama Jaji aliyesikiliza kesi hiyo angechambua kwa kina kanuni inayosimamia suala hilo, asingefikia katika hitimisho kuwa upande wa Jamhuri ulikuwa umethibitisha kosa hilo pasipo kuacha mashaka yoyote.
Hoja nyingine ambayo mahakama imeizingatia ni kuwa warufani hao ni waathirika wa ukamataji wa mali usiofuata kanuni wala kuzingatia sheria zinazosimamia makosa ya Jinai.
Pia wamekubali kuwa kutiwa kwao hatiani kulifanyika kimakosa kwa kuegemea maelezo ya ungamo (extra judicial statement) za warufani ambayo walidai yalipatikana bila uhiyari na kupokelewa na mahakama kinyume cha sheria.
Ni kwa msingi huo, majaji hao walisema upande wa mashitaka haukuwa umethibitisha shitaka dhidi ya warufani, hivyo kubatilisha kutiwa kwao hatiani na adhabu waliyopewa na kuamuru waachiliwe mara moja kutoka gerezani.