Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waliofariki ajali ya mtumbwi Nyumba ya mungu watambuliwa

Muktasari:

  • Miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mawenzi kabl ya kuzikwa jumatatu Julai 27, huku manusura mmoja akiendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya TPC kutokana na mshtuko.

Moshi. Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limetaja majina ya watu watano wa familia moja waliopoteza maisha baada ya mtumbwi waliokuwa wakisafiria kupinduka katika Bwawa la Nyumba ya Mungu, wilayani Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Ajali hiyo ilitokea jana Alhamisi Julai 23, 2026, katika eneo la Mikocheni, Kata ya Arusha Chini, baada ya mtumbwi waliokuwa wakisafiria waumini wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) Chemchemi, kukumbwa na upepo mkali uliosababisha mawimbi makubwa na hatimaye kupinduka.

Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa, Julai 24, 2026, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro, Jeremia Mkomagi amesema waliofariki dunia ni pamoja na Maria Andrea, Yustina Lazaro, Raima Andrea, Happy Andrea na Kelvini Andrea.

"Mtumbwi ulipinduka baada ya kukumbwa na mawimbi makubwa yaliyosababishwa na upepo mkali. Wananchi waliokuwa karibu na eneo la tukio walishirikiana na Jeshi la Polisi pamoja na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kufanya operesheni ya uokoaji. Watu wanane waliokolewa na miili mitano ilipatikana," amesema Mkomagi.

Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro wakishirikiana na wananchi kuushusha mwili wa mmoja wa waliofariki dunia kufuatia ajali ya mtumbwi iliyotokea katika Bwawa la Nyumba ya Mungu, Kata ya Arusha Chini wilayani Moshi.

Amewataja walionusurika kuwa ni Eliza Kiula, Stella Eza, Aziza Kadoda, Elda Mfuru, Sophia Godi, Malta John, Careen Andrea na Ebenezer Kadoda.

Baba wa mume wa mmoja wa marehemu, mzee Lawrence Ngonyani amesema msiba huo umeiacha familia katika majonzi makubwa baada ya kupoteza watu watano kwa wakati mmoja.

Amesema mwanaye amepoteza mke wake, watoto wao watatu pamoja na mdogo wa mke wake.

"Tulipokea taarifa hizi kwa uchungu mkubwa. Kupoteza watu watano wa familia moja ni pigo zito sana. Sisi tuliobaki hatuna la kufanya zaidi ya kumtegemea Mungu," amesema.

Kwa mujibu wa Mzee Ngonyani, watoto waliofariki dunia walikuwa na umri wa miaka 12, 10 na mitatu.

Amesema mazishi ya watu hao yanatarajiwa kufanyika Jumatatu, Julai 27, 2026 katika Kijiji cha Chemchemi, Kata ya Arusha Chini, Wilaya ya Moshi.


Safari ilivyogeuka majonzi

Akisimulia kilichotokea, Mchungaji wa Kanisa la TAG Chemchemi, Silvanus Haule amesema  safari hiyo ilianza baada ya ibada ya asubuhi, waumini walikuwa wakielekea kwenye kongamano la Idara ya Wanawake lililokuwa likifanyika katika Kanisa la TAG Mikocheni Ndogo.

Amesema awali waumini walielekezwa kutumia kivuko kilichopo eneo hilo, lakini mmoja wa wakazi alijitolea kuwavusha kwa mtumbwi hadi Mikocheni Kubwa.

Baadhi ya abiria walimwomba mwendesha mtumbwi awapeleke hadi Mikocheni Ndogo kwa kuwa eneo hilo lilikuwa karibu na mahali kongamano lilipokuwa likifanyika.

"Walipokuwa njiani, upepo mkali ulivuma na mawimbi yakaanza kuuingiza maji mtumbwi. Nahodha aliwaambia washike mtumbwi huku akiogelea kwenda kuomba msaada. Kabla waokoaji hawajafika, wanawake wawili na watoto watatu walikuwa tayari wameachia mtumbwi na kuzama," amesema Haule.

Amebainisha kuwa wanawake hao wawili walikuwa ndugu, huku watoto watatu waliofariki wakiwa ni wa mmoja wao.


Serikali yatoa tahadhari

Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava amesema Serikali imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za ajali hiyo na kutoa pole kwa familia zilizopoteza wapendwa wao.

Amewataka wananchi kuzingatia tahadhari wanapotumia vyombo vya usafiri majini, akisema licha ya kuwepo kwa njia ya nchi kavu kuelekea eneo husika, waumini hao walichagua njia ya maji kwa kuwa ilikuwa fupi.

"Ni bora kutumia njia salama hata kama ni ndefu kuliko kutumia njia ya mkato ambayo usalama wake haujathibitishwa, hasa wakati hali ya hewa siyo nzuri," amesema.

Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro wakishirikiana na wananchi wakiwa wamebeba mwili wa mmoja wa waliofariki dunia kufuatia ajali ya mtumbwi iliyotokea katika Bwawa la Nyumba ya Mungu, Kata ya Arusha Chini wilayani Moshi.

Ameongeza kuwa pamoja na mvua kupungua, kiwango cha maji katika Bwawa la Nyumba ya Mungu bado ni kikubwa na upepo unaendelea kuvuma kwa nguvu, hivyo wananchi wanapaswa kuzingatia tahadhari zinazotolewa na mamlaka husika.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya TPC, Timizaeli Sumuni amesema hospitali hiyo ilimpokea mmoja wa manusura wa ajali hiyo, mwanamke mwenye umri wa kati ya miaka 48 na 50.

Amesema manusura huyo hakupata majeraha ya mwili, lakini alipata mshtuko kutokana na tukio hilo.

"Hakuwa na majeraha yoyote, lakini alipata mshtuko mkubwa kutokana na ajali. Pia alimeza maji kiasi, hata hivyo aliokolewa baada ya kusukumwa na upepo hadi eneo lenye kina kifupi," alisema.

Miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi, ikisubiri kukamilika kwa taratibu za kipolisi kabla ya kukabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya mazishi.