Watano familia moja wafariki dunia ajali ya mtumbwi wakielekea kanisani
Moshi. Majonzi na simanzi vimetanda katika Kijiji cha Chemchem, Kata ya Arusha Chini, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, baada ya watu watano wa familia moja, wakiwemo wanawake wawili na watoto watatu, kufariki dunia kufuatia mtumbwi waliokuwa wakisafiria kupinduka katika Bwawa la Nyumba ya Mungu.
Tukio hilo limetokea leo Julai 23, 2026 majira ya mchana wakati waumini wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) Chemchem walipokuwa wakielekea Kitongoji cha Mikocheni 'B' (Mikocheni Ndogo) kuhudhuria kongamano la Idara ya Wanawake wa kanisa hilo.
Waliofariki ni dada wawili wa familia moja pamoja na watoto watatu wa mmoja wao, wasichana wawili na mvulana mmoja. Mtoto mmoja wa familia hiyo na abiria wengine sita wamenusurika, huku baadhi yao wakipelekwa Hospitali ya TPC kwa matibabu.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro, Jeremia Mkomagi, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo, akisema miili mitano imeopolewa majini na kukabidhiwa Jeshi la Polisi, huku uchunguzi ukiendelea kubaini chanzo cha ajali pamoja na idadi kamili ya manusura na majeruhi.
"Tumetoa miili mitano majini na kuikabidhi Jeshi la Polisi kwa taratibu nyingine. Uchunguzi unaendelea ili kubaini chanzo halisi cha ajali pamoja na kutambua majina ya waliofariki na majeruhi," amesema Mkomagi.
Amesema hadi sasa haijafahamika kilichosababisha mtumbwi huo kupinduka, huku uchunguzi ukiendelea kubaini kama ulikuwa umebeba watu wengi kuliko uwezo wake au kama kulikuwa na sababu nyingine.
Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro wakishirikiana na wananchi kuushusha mwili wa mmoja wa waliofariki dunia kufuatia ajali ya mtumbwi iliyotokea katika Bwawa la Nyumba ya Mungu, Kata ya Arusha Chini wilayani Moshi.
Pia amesema taarifa kuhusu nahodha wa mtumbwi huo bado zinafanyiwa kazi kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi.
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu, Diwani wa Kata ya Arusha Chini, Leonard Waziri amesema taarifa alizozipokea zinaeleza kuwa waumini hao walitoka Kijiji cha Chemchem wakielekea Mikocheni Ndogo kwa ajili ya kongamano la kanisa.
Amesema waumini hao awali kabla ya safari walikuwa na uchaguzi wa kutumia barabara ya kawaida au kuvuka kupitia Bwawa la Nyumba ya Mungu kwa mtumbwi, lakini waliamua kutumia njia ya maji.
"Kati ya abiria waliokuwamo kwenye mtumbwi, watano wamefariki na saba wameokolewa. Kilichotokea katikati ya safari kitafahamika zaidi kupitia ushuhuda wa walionusurika," amesema Waziri.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kijiji cha Chemchem, Alex Joseph Mgaya, taarifa za ajali zilimfikia majira ya saa nane mchana, zikieleza kuwa mtumbwi uliokuwa umewabeba waumini hao ulizama walipokuwa wakielekea kongamano la wanawake wa TAG Mikocheni Ndogo.
Mgaya amesema upepo mkali uliovuma katika bwawa hilo ulisababisha mawimbi kuingia ndani ya mtumbwi na hatimaye kupinduka.
"Katika tukio hilo wanawake wawili na watoto watatu walifariki papo hapo. Walionusurika walipelekwa Hospitali ya TPC, ambapo wawili wameruhusiwa na mmoja bado anaendelea na matibabu," amesema.
Mchungaji wa Kanisa la TAG Chemchem, Silvanus Haule, amesema safari hiyo ilianza asubuhi baada ya ibada kanisani, ambapo waumini walijipanga kuelekea kwenye kongamano lililokuwa linafanyika katika kanisa jingine lililopo Mikocheni Ndogo.
Amesema awali walikuwa wameelekezwa watembee hadi kivukoni kabla ya kuvuka, lakini mmoja wa wakazi alijitolea kuwapeleka kwa mtumbwi hadi Mikocheni Kubwa.
Hata hivyo, amesema baadhi ya abiria walimuomba nahodha awaongezee safari hadi Mikocheni Ndogo, ambako ndiko kongamano la wanawake lilitarajiwa kufanyika kwa kuwa ilikuwa karibu.
Amesema walipokuwa wakielekea huko, upepo mkali ulivuma na mawimbi kuanza kuujaza maji mtumbwi huo kabla ya kupinduka.
"Baada ya upepo mkali, mwendesha mtumbwi (nahodha) aliwaambia washike mtumbwi huku akijaribu kuogelea kuelekea ufukweni kuomba msaada. Kabla waokoaji hawajafika, wanawake wawili na watoto watatu walikuwa tayari wameachia mtumbwi na kuzama," amesema.
Mchungaji huyo amesema waliopoteza maisha wote ni wa familia moja, akieleza kuwa wanawake hao walikuwa ndugu, huku watoto watatu waliokuwa wamefariki wakiwa ni watoto wa mmoja wao.
Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro wakishirikiana na wananchi wakiwa wamebeba mwili wa mmoja wa waliofariki dunia kufuatia ajali ya mtumbwi iliyotokea katika Bwawa la Nyumba ya Mungu, Kata ya Arusha Chini wilayani Moshi.
Amesema manusura wengi wameanza kurejea nyumbani baada ya kupatiwa matibabu, huku mtu mmoja akiendelea kupatiwa matibabu Hospitali ya TPC akilalamikia maumivu ya kichwa kutokana na mshtuko alioupata baada ya ajali hiyo.
Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linaendelea na uchunguzi wa ajali hiyo, huku miili ya marehemu ikiwa imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mawenzi kwa taratibu nyingine za kipolisi kabla ya kukabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya mazishi.