Walimu Mbeya kupelekwa Dubai, vigezo hivi hapa

Muktasari:
- Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Homera amesema Dubai ndio sehemu nzuri kwa mapumziko akieleza kuwa ofa hiyo itahusisha walimu wa shule za Serikali huku za binafsi kamati itakaa kujadili zawadi
Mbeya. Kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera kuwapeleka walimu 10 wa shule za msingi na sekondari Dubai kwa watakaofanikisha ufaulu mwakani, imeonekana kuwaamsha walimu kila mmoja akiahidi kufundisha kwa bidii ili kupata nafasi hiyo.
Akizungumza leo Julai 16 katika kikao cha tathimini ya elimu mkoani humo kilichohusisha wadau wa sekta hiyo ikiwa ni kupongeza matokeo mazuri ya kidato ch sita yaliyotangazwa hivi karibuni, Homera amesema watatoa ofa kwa walimu 10 kwenda Dubai.
Amesema kutokana na matokeo mazuri yaliyopatikana mwaka huu, Dubai ndio sehemu nzuri kwa mapumziko akieleza kuwa ofa hiyo itahusisha walimu wa shule za Serikali huku za binafsi kamati itakaa kujadili zawadi.
Amesema kwa sasa Mbeya ipo katika ramani nzuri kielimu, inazidiwa na mkoa mmoja tu (hajautaja) akieleza kuwa mkakati ni kushika nafasi ya kwanza akiwatia moyo walimu kuwa inawezekana.
"Wakati nafika hapa Mbeya tulikuwa nafasi hazijulikani, lakini kwa sasa matokeo yetu hayana sifuli, tuna daraja la kwanza 4,047, la pili 2726 daraja la tatu 487 na nne ni tano, niwapongeze walimu kwa kazi nzuri.
"Niagize kila halmashauri yenye uwezo inaweza kuwapa zawadi shule zilizofanya vizuri na mwakani walimu 10 ikiwa watano shule za msingi na watano sekondari tutawapeleka Dubai katika hoteli ya nyota tano wakirudi wawe wamebadilika kwa kuongea Kiingereza," amesema Homera.
Amesema kutokana na umuhimu wa walimu, ameelekeza ofisi zote mkoani humo kutowapanga foleni pale wanapofika kuhitaji huduma yoyote, lakini kutonyimwa likizo na kuwapa fursa kujiendeleza kielimu kwa kuzingatia muongozo wa elimu nchini.
Homera amesema Serikali ya awamu ya sita imetoa Sh17 bilioni kwa ajili ya miundombinu ya elimu, akiwataka watendaji kukamilisha miradi yote hasa madarasa yaliyo katika ujenzi kukamilika kwa wakati.
"Nielekeze kuwapo kwa chakula shuleni kwa ajili ya wanafunzi, wazazi wachangie huduma hii kwa mustakabari wa matokeo mazuri, tupambane kuacha alama katika maeneo yetu kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan anayeidhinisha fedha hizi,"amesema Homera.
Pia, amewataka walimu kujitambua akieleza kuwa wakati wakiendelea kung’ang'ania matokeo mazuri, vivyo hivyo wasijisahau katika maendeleo yao binafsi kwa kuwekeza kwa ajili ya maisha yao ya baadaye.
Wakizungumzia kauli hiyo, baadhi ya walimu wa shule za msingi na sekondari mkoani humo, wamesema kila mmoja anatamani kwenda Dubai, hivyo itakuwa ni vita kali kuwania nafasi hiyo.
Baraka Mwangunda, Mwalimu wa Shule ya Msingi Ikuti jijini humo, amesema hatua hiyo inaenda kuamsha upya ari na morali katika majukumu yao kwa kila mmoja kupambania nafasi ya safari hiyo.
"Sidhani kama kuna ambaye hapendi safari ya Dubai, binafsi naenda kujipanga kuona namna ya kuongeza juhudi ili katika somo langu nifaurishe zaidi nisubiri kamati itakachoamua," amesema Mwangunda.
Naye Mwalimu Irene Bukuku wa Shule ya Msingi Igale, amesema matarajio yake ni kuongeza bidii katika kusimamia na kufundisha.
"Kikubwa ni ushirikiano kuanzia wazazi hadi wakuu wa idara, sasa zile mbinu tulizotumia kupata ufaulu huu tukiongeza na hii motisha ya Dubai kitaeleweka," amesema Irene.
Shadrack Mwaibambe, Mwalimu wa Shule ya Sekondari Lubaga wilayani Kyela amesema pamoja na motisha hiyo kwenda kuwaongezea ushindani, lakini huduma ya chakula shuleni kwa walimu na wanafunzi ni muhimu sana.
"Twende kazini, matokeo yatajibu na kuamua nani aende na nani abaki, lakini tumeipokea vyema ofa hii na itatuongezea hamasa kubwa katika majukumu yetu, niombe huduma ya chakula iwe kwa mwanafunzi na mwalimu," amesema Mwaibambe.
Akitoa salamu kwa niaba ya madiwani, Meya wa Jiji la Mbeya Dourmohamed Issa amesema ili kuhakikisha ufaulu unaendelea mkoani humo, lazima huduma ya chakula shuleni iwahusishe pia walimu.
"Haitawezekana mwanafunzi ashibe halafu mwalimu ana njaa, hayo madini hayatapatikana, lazima tunapowapa chakula wanafunzi na walimu nao wapate ili kurahisisha kazi," amesema meya huyo.
Mwenyekiti wa Umoja wa Walimu Wakuu kwa Shule za Sekondari Mkoa wa Mbeya (Taosa), Francis Mwakihaba amesema matokeo mazuri katika mkoa huo yametokana na uongozi imara uliopo na ushirikiano.
Mmoja wa wananchi jijini hapa, Yusuph John amesema zawadi hiyo kwa walimu itaongeza hamasa kwao katika kuongeza juhudi katika ufundishaji akieleza kuwa huenda ikawa njia sahihi ya kuongeza ushindani.
"Mtu akifanya vizuri kupongeza siyo dhambi, japokuwa ahadi hiyo itekelezwe na huenda kila shule ikaja na mkakati wa kupambana kupata nafasi hiyo, sisi wazazi tunatamani kuona watoto wetu wakifaulu" amesema John.