Walimu mbaroni wakidaiwa kufanyisha wanafunzi wa sekondari mitihani ya la saba

Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Wilbroad Mutafungwa akizungumza na Waandishi wa Habari leo Ijumaa Septemba 22, 2023. Picha na Mgongo Kaitira

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linawashikilia walimu wanne kwa tuhuma za kuwafanyisha mitihani ya darasa la saba wanafunzi watatu wa sekondari katika Shule ya Msingi Igulumuki Wilaya ya Sengerema mkoani humo.

Mwanza. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linawashikilia walimu wanne kwa tuhuma za kuwafanyisha mitihani ya darasa la saba wanafunzi watatu wa sekondari katika Shule ya Msingi Igulumuki Wilaya ya Sengerema mkoani humo.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Ijumaa Septemba 22, 2023; Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amewataja walimu wanaoshikiliwa ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Sima wilayani humo na Msimamizi Mkuu wa Mitihani katika shule ya Msingi Igulumuki, Maiko Sheusi (35).

Wengine ni mwalimu wa Shule ya Sekondari Kilabela ambaye ni msimamizi wa mtihani mkondo namba 2, Musa Mwashihava (38), Mwalimu wa Shule ya Sekondari Buzilasoga, Bonasi Balozi (33) na Mwalimu wa Taaluma wa Shule ya Msingi Igulumuki, Azizi Mohamed (36).

"Walimu hawa wanatuhumiwa kwa kosa la udanganyifu wa mitihani ya darasa la saba kwa kuwachukua wanafunzi wa Sekondari na kuwafanyisha mitihani hiyo kwa niaba ya wanafunzi wa darasa la saba,” amesema Mutafungwa

Mutafungwa amesema wanafunzi wanaoshikiliwa wote wana miaka 14 wanaosoma shule ya Sekondari Sima Kata ya Igukumuki wilayani humo wakidaiwa kuingizwa kwenye chumba cha mtihani kwa ajili ya kufanya mitihani hiyo kwa niaba ya wanafunzi wengine.

Amesema tukio hilo lililotokea Septemba 13, Mwaka huu, baada ya Kamati ya Mitihani ya Wilaya ya Sengerema kutembelea na kukagua namna mitihani hiyo inavyofanyika na kubaini udanganyifu huo ambapo mkondo namba mbili na namba tatu wa shule hiyo ilibainika kuwa na wanafunzi wa Sekondari wakifanya mitihani hiyo.

"Watuhumiwa wote wamehojiwa kwa kina na watafikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo baada ya upelelezi kukamilika. Tunaendelea kuimarisha ulinzi maeneo yote na hatutasita kuchukua hatua kali za kisheria kwa wahalifu na wadanganyifu wa aina yoyote," amesema Kamanda huyo

Katika hatua nyingine, Jeshi hilo limeanza uchunguzi wa Kampuni ya Alliance Global in Motion ambayo inadaiwa kufungua Ofisi katika jengo la Rock City Mall wilayani Ilemela mkoani Mwanza huku ikituhumiwa kufanya utapeli dhidi ya vijana 150 kwa kuwatoza fedha kwa ahadi ya kuwawezesha kufanya biashara ya tiba lishe kwa njia ya mtandao.

"Tulianza uhunguzi wa kampuni hiyo Septemba 19 mwaka huu baada ya kupata taarifa hizo kutoka kwa wananchi kwa kuwahoji watu mbalimbali wakiwemo wanachama 46 kati yao mabinti wawili wa kampuni hiyo kutoka mikoa mbalimbali,"amesema

Amesema jeshi hilo linaendelea kufuatilia uhalali wa kampuni hiyo pamoja na shughuli inazozifanya kwa mujibu wa sheria na katika uchunguzi huo litashirikiana kwa ukaribu na tasisi nyingine za Serikali.