Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Walimu Dar ‘wakunwa’ na mafanikio kielimu

Muktasari:

  • Umoja wa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania Bara (Tapsha) Wilaya ya Ilala,  umesema unatambua mchango wa Rais Samia Suluhu Hassan kielimu na utahakikisha watoto wote wanaoanza shule wanamaliza na kufaulu

Dar es Salaam. Walimu wanaounda Umoja wa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania Bara (Tapsha) Wilaya ya Ilala, wamefurahishwa na ufaulu wa asilimia 98.7 wa wanafunzi wa darasa la saba  katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na kusema watahakikisha watoto wanaoanza shule wanamaliza na kufaulu.

 Pia, wamesema wanatambua mchango wa Rais Samia Suluhu Hassan kielimu kwa kufanya maboresho mbalimbali ikiwamo miundombinu ya shule.

Maazimio hayo yametangazwa jijini Dar es Salaam Desemba 8, 2023 kupitia risala ya umoja huo kwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo katika mkutano uliokuwa na kauli mbiu ya, “Yamewezekana yasiyowezekana katika elimu nchini.”

Hata hivyo, Tapsha imebainisha changamoto kadhaa zikiwamo upungufu wa walimu kwa baadhi ya shule mpya, uchakavu wa majengo, upungufu wa madawati, ukosefu wa meza na viti vya walimu na kuchelewa kwa malipo ya nauli za likizo kwa walimu.

Mwenyekiti wa Tapsha ya Ilala Shule za Msingi za Serikali, Godrick Rutayungururwa amesema mchango wa Rais Samia katika elimu, utatambuliwa kwa tuzo maalumu.

Mwenyekiti wa Tapsha Ilala, Shule za Msingi Binafsi, Jefta Chaulo amesema mchango wa Rais Samia katika elimu, unadhihirishwa na kupungua kwa idadi ya wanafunzi wasiomudu Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) katika shule zao, jambo linalowafanya kuazimia utoaji wa tuzo kwa kiongozi huyo wa nchi.

Akizungumza katika mkutano huo Mpogolo  ambaye ni mkuu wa wilaya hiyo, amewapongeza walimu hao kwa ufaulu wa wanafunzi akisema kwa miaka minne mfululizo, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imekuwa ikiongoza kwa ufaulu wa wanafunzi wanaomaliza darasa la saba.

“Hata mwaka huu ufaulu umeongezeka kwa kiwango kikubwa mpaka kupata zaidi ya asilimia 97.8," amesema Mpogolo.

Pia, ameupongeza umoja huo kwa usimamizi mzuri wa miradi inayoendelea kutekelezwa katika ngazi za chini.

“Ninawasihi, kuna fedha nyingi ambazo Rais anazipeleka katika halmashauri za utekelezaji wa miradi kwa hiyo na ninyi ndiyo wasimamizi, mkaisimamie vizuri na lazima itekelezwe kwa ubora unaotakiwa,” amesema.

Mpogolo amesema walimu wana thamani kubwa kwao kutokana na mafanikio wanayoendelea kuyapata huku akitolea mfano wa Septemba, mwaka huu.

 "Wakati wa likizo tulikuwa na kazi ya ukusanyaji wa takwimu za wafanyabiashara katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, tuliwatumia walimu katika kazi hiyo.”

Amesema halmashauri hiyo imefanikiwa kuongeza mapato yake kutoka Sh6 bilioni kwa mwezi, hadi Sh10 bilioni na kwa mwaka wanakusudia kukusanya Sh120 bilioni, huku sehemu ya fedha hizo zikitengeneza viti na meza kwa shule za sekondari 17,600 na madawati kwa shule za msingi 20,000.

Pia, amewaomba waendelee kumwombea Rais Samia kwa kuwa amefanya mambo makubwa katika wilaya hiyo, ikiwamo kuwapatia zaidi ya Sh15 bilioni kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya elimu msingi, kugharamia elimu bure na mitihani pamoja na ununuzi wa vitabu vya kiada na ziada.