Walimu watakiwa kwenda na mabadiliko ya sera, mitaala

Muktasari:
Waalimu wametakiwa kwenda na mabadiliko ya sera na mitaala ya elimu ili waweze kufundisha elimu ya ujuzi itakayo wawezesha wanafunzi wanaohitimu kujitegemea kwa kujiajiri badala ya kusubiri ajira za Serikali zisizoendana na wingi wa wahitimu.
Geita. Waalimu wametakiwa kwenda na mabadiliko ya sera na mitaala ya elimu ili wafundishe elimu ya ujuzi itakayo wawezesha wanafunzi wanaohitimu kujitegemea kwa kujiajiri badala ya kusubiri ajira za Serikali ambazo ni chache zisizoendana na wingi wa wahitimu.
Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Said Nkumba ameyasema hayo wakati wa mahafali ya 10 ya wahitimu 87 wa kidato cha nne katika shule za Sekondari za Waja zilizopo mjini Geita akidai mabadiliko ya mitaala yamelenga kutoa fursa za elimu na mafunzo kwa kuzingatia njia mbalimbali za ufunzaji zitakazo endana na mazingira ya sasa.
Aidha amesema ni wakati sasa shule kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundisha ili kukuza vipaji vya watoto sanjari na kufundisha elimu ya kujitegemea na ile ya ujasiriamali itakayowawezesha wahitimu kujiajiri na kupunguza changamoto ya ajira nchini.
“Serikali imeendelea kuboresha sera na mitaala ili kuhakikisha wanafunzi wanaomaliza wanaweza kujiajiri na kujitegemea. Sera za elimu kwa muda mrefu zilikuwa zikiwafanya watoto wanapomaliza wabaki kuwa tegemezi hawawezi kujiajiri lakini mabadiliko ya sasa ya mitaala yatawezesha mtoto kujiajiri”amesema Nkumba
Akizungumzia ujenzi wa vyuo vya ufundi vinavyojengwa kila Wilaya amesema, vyuo hivyo vitawezesha watoto kujifunza stadi za maisha na kujiajiri na kwamba tofauti na wimbi kubwa la wanafunzi waliokuwa wakihitimu kidato cha nne kubaki nyumbani baada ya kufeli sasa wataweza kujiunga kwenye vyuo na kupunguza utegemezi.
Mkurugenzi wa taasisi za Waja, Chacha Wambura amesema elimu inayotolewa sasa haimsaidii mwanafunzi kujitegemea lakini uboreshwaji wa mitaala unaofanywa na Serikali utaleta suluhisho linalomuwezesha mwanafunzi kujitegemea na kupunguza utegemezi.
Akiwaasa wanafunzi waliohitimu kidato cha nne, Wambura amewataka wanafunzi hao kuendelea kuwa na nidhamu na kutokubali kutawaliwa na mitandao ya kijamii badala yake waweke malengo ili kutimiza ndoto zao.
Mkuu wa shule ya wasichana ya Waja, Glory Ottaru amesema shule hiyo imefanikiwa kuandaa wanafunzi na kuzifanya shule za Waja kuwa kinara wa ufaulu ndani na nje ya Mkoa wa Geita.
Ottaru amesema shule hizo hufadhili wanafunzi wanaofanya vizuri katika matokeo yao kwa lengo la kuiunga mkono Serikali na kumuwezesha mtoto wa kitanzania kupata elimu ambapo kuanzia mwaka 2014 watoto 547 wamefadhiliwa.