Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ufaulu wa D, E wawaibua wadau, wawataja walimu

Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani nchini (Necta). Dk Said Mohammed akitangaza matokeo ya mitihani ya darasa la saba ya mwaka 2023 jijini Dar es salaam, Kushoto ni Naibu Katibu Mtendaji Angela Kitali. Picha na Said Khamis

Dar es Salaam. Wakati Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) likisema ufaulu wa wahitimu wa darasa la saba umeongezeka kwa asilimia 0.96, jumla ya watahiniwa 263,336 waliofanya mtihani huo mwaka huu wamepata alama D na E.

Kulingana na maelezo ya baraza hilo, alama D inaashiria ‘inaridhisha’ huku alama E ikimaanisha ‘hairidhishi’, na makundi haya yanakamata mkia katika viwango vya ufaulu vya taasisi hiyo inayosimamia mitihani ya Taifa ya shule za msingi na sekondari nchini.

Kati ya wanafunzi wenye ufaulu huo, wavulana ni 122,333 sawa na asilimia 46.5 ya waliopata madaraja hayo mawili, huku wasichana wakiwa 141,003, sawa na asilimia 53.5.

Licha ya idadi ya watahiniwa waliopata wastani wa D na E mwaka 2023 kupungua kwa asilimia 4.1 ikilinganishwa na 274,671 mwaka 2022, bado wadau wa elimu wanapata wasiwasi wa ubora wa elimu, huku wakishauri maboresho zaidi.

Akitangaza matokeo hayo, Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Said Mohamed alisema ufaulu umeongezeka kidogo kutoka asilimia 79.62 mwaka 2022 hadi asilimia 80.58 mwaka 2023.

Akishauri namna sahihi ya kuongeza ubora wa elimu nchini ili kuondokana na madaraja hayo hafifu, Dk Zubeda Mussa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema walimu wawezeshwe ili waendane na mabadiliko.

“Walimu wanapaswa kupigwa msasa kwa kufanyiwa semina za mara kwa mara ili kuendana na mabadiliko ambayo hawakuyapata kipindi wako vyuoni,” alishauri Dk Zubeda.

Hoja ya Dk Zubeda iliungwa mkono na Suzan Lyimo, ambaye ni mdau wa elimu na Spika wa Bunge la Wananchi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), aliyesema ili kuboresha elimu na kupunguza idadi ya wenye ufaulu huo wa chini, mazingira ya walimu yaboreshwe ili wafanye kazi kwa bidii.

“Cha kufanya hapo ni kuboresha mazingira ya walimu, kwanza wanapaswa kuboreshewa masilahi kwa sababu wao ndio kila kitu, ndio wanazalisha watu wa kila aina kama marubani, madaktari na wahandisi.

“Hakuna watu wanaowajali (walimu) ndio maana wanajiendea tu. Tukiboresha mazingiria ya walimu hata wanafunzi watafaulu kama zamani,” aliongeza.
Akiendelea kushauri namna ya kukwamua ubora wa elimu na ufaulu, Dk Zubeda alisema Serikali iendelee kuboresha maeneo yenye mahitaji ya kimiundombinu na kitaaluma.

Akizungumzia suala la ufaulu kuongezeka huku kukiwa na takwimu zisizoridhisha kwa baadhi ya masomo, Mtafiti wa Elimu, Muhanyi Nkoronko alisema Serikali inapaswa kuangalia namna ya kuruhusu walimu kusoma masomo maalumu ili ipate wataalamu waliobobea.

“Waruhusiwe walimu watakaoenda kusoma somo kama hisabati pekee au Kiingereza ili wakafundishe kwa umahiri zaidi,” alishauri.
Kwa upande wake Lyimo alisema ongezeko la ufaulu halijafika hata asilimia moja, hivyo “halina maana kubwa na bado kuna tatizo la upimaji wa mitihani kwa wanafunzi.”

“Ufaulu wa Tanzania hauangalii mwanafunzi kwa miaka yote alifanya nini, bali unaangalia siku ya mtihani amejibu nini. Inawezekana ameamka vizuri na mtihani ni wa kuchagua hakuna njia, anaweza akaotea akafaulu lakini akaenda sekondari akawa hajui kusoma wala kuandika,” alisema.

Aidha, Nkoronko alisema tafsiri ya kusema ufaulu umeongezeka ni kupanda kwa madaraja ya ufaulu ukilinganisha na mwaka jana.

“Kiujumla kama shule ilikuwa na idadi ileile ya wanafunzi mwaka jana na ilikuwa na wastani wa C, na mwaka huu kwa idadi hiyohiyo imepata alama B hapo tunaona ongezeko la ufaulu.

“Kwa hiyo tunapima idadi ya wanafunzi waliotoka daraja moja kwenda jingine na shule kutoka daraja moja kwenda jingine,” aliongeza.

Nkoronko alisema kuongezeka kwa ufaulu kumetokana na uboreshwaji wa taaluma na uwekezaji uliofanywa na Serikali.

Kwa upande wake Lyimo, alisema njia nzuri ya kuwatahini wanafunzi ni kuangalia kazi alizofanya mwaka mzima zimpe kiasi fulani cha alama, kisha mtihani wa mwisho pia uwe na alama zake.

Lakini alisema Serikali haifanyi hivyo, kitu alichodai kinamfanya mwanafunzi afaulu akiwa hana ubora.

Kupitia mtandao wa Instagram wa gazeti hili, @unclestey alisema tatizo linaanzia kwa walimu na namna ya upatikanaji wao.

“Ukiona hivyo hata upande wa walimu pana shida kubwa, kumbuka hawa waliopata D ndio hao hao walimu wajao watakaofundisha somo hilo,” alisema.
 

Wasichana na E, D

Akizungumzia matokeo kuonyesha wasichana wanaongoza kwa kupata madaraja E na D, Mhadhiri wa UDSM, Dk George Kahangwa alisema kuna sababu za kimazingira na kifamilia zinazomkwamisha msichana kielimu.

“Mara nyingi katika madarasa ya awali watoto wa kike hufanya vizuri sana, lakini wakianza kufika darasa la saba, anaanza kupewa majukumu ya kiutu uzima kama kulea wadogo zake, jambo ambalo linayumbisha ufaulu wao,” alisema.

Dk Kahangwa alisema zipo jamii nyingine ambazo zinawalazimisha watoto wa kike wafeli kusudi wakaolewe au kufanya kazi za ndani.

“Matokeo haya kama Taifa yanatwambia nini cha kufanya kwa watoto wa kike, ni kwamba, kwa jumla tunapaswa tuendelee kuwekeza kwenye elimu. Hata ambao hawajafaulu wawezeshwe kupata elimu ya ufundi au vipaji walivyonavyo,” alisema.

 

Kurudia mtihani

Wakati huohuo, Baraza limefuta matokeo yote ya watahiniwa 31 nchini waliofanya mtihani ambao wamebainika kufanya udanganyifu.

Vilevile Dk Mohamed ameongeza kuwa Baraza limefungia vituo viwili vya mtihani ambavyo ni Twibhoki na Graiyaki vya halmashauri ya Serengeti mkoani Mara.

"Vituo hivyo vimethibitika kupanga kufanya udanganyifu katika mtihani na vimefungiwa kwa mujibu wa kifungu 4(8) cha kanuni za mtihani mwaka 2016 mpaka hapo Necta itakapojiridhisha kuwa ni salama kwa uendeshaji wa mitihani ya Taifa," alibainisha.

Aidha, Dk Mohamed alisema baraza limezuia matokeo ya watahiniwa 360 ambao walipata matatizo ya kiafya na kushindwa kufanya mtihani kwa masomo yote au idadi kubwa ya masomo.

"Watahiniwa husika wamepewa fursa ya kurudia kufanya mtihani huo mwaka 2024 kwa mujibu wa kifungu cha 32(1) cha kanuni za mitihani.

Katika matokeo hayo, ufaulu wa wastani A, B na C mwaka 2023 umeongezeka hadi kufikia wanafunzi milioni 1.09 kutoka wanafunzi milioni 1.07 mwaka 2022.