Walimu 919 wafukuzwa kazi kwa utovu wa nidhamu

Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC),  Paulina Nkwama

Muktasari:

  • Jumla ya walimu 919 wamefukuzwa kazi katika kipindi cha Machi, 2021 hadi Septemba mwaka 2022 kutokana na makosa mbalimbali ya kinidhamu huku kosa la utoro likiongoza kwa asilimia 68.9 ya makosa yote.

Dodoma. Jumla ya walimu 919 walifukuzwa kazi katika kipindi cha Machi, 2021 hadi Septemba mwaka 2022 kutokana na makosa mbalimbali ya kinidhamu ikiwemo utoro kazini.

Makosa mengine ni kughushi vyeti, mahusiano ya kimapenzi kati ya walimu na wanafunzi, ukaidi, ubadhirifu na ulevi.

Katibu wa Tume ya Utumishi Walimu (TSC), Paulina Nkwama ameyasema hayo leo Alhamis, Oktoba 27, 2022 wakati akizungumzia utekelezaji wa taasisi na vipaumbele vya mwaka 2022/2023.

Nkwama amesema walimu 1,952 walifunguliwa mashauri ya kinidhamu na kati ya mashauri yaliyofunguliwa 1,362 (sawa na asilimia 69.8) yalihusu utoro.

Amesema mashauri 260 (asilimia 13.3) yalihusu kughushi vyeti, 119 (asilimia 6.1) yalihusu mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi, 98 (asilimia 5) yalihusu ukaidi, 66 (asilimia 3.4) yalihusu ulevi huku 16 (asilimia 0.8) yalihusu ubadhirifu na 31 (asilimia 1.6) yalihusu makosa mengineyo.

Amesema katika mashauri 1,642 yaliyoamuliwa na tume hiyo walimu 919 sawa na asilimia 56 ya adhabu zilizotelewa walifukuzwa kazi.

Amesema walimu 234 sawa na asilimia 14.3 hawakupatikana na hatia na walimu 115 (asilimia 7) ya adhabu zilizotolewa walishushwa cheo, 89 (asilimia 5.4) walikatwa mshahara kwa asilimia 15 kwa muda wa miaka mitatu.

Amesema walimu 143 (asilimia 8.7) walipewa adhabu ya karipio, 59 (asilimia 3.6) walipewa adhabu ya onyo na 77 (asilimia 4.7) walipewa adhabu ya kufidia hasara.

Amesema mashauri 310 yapo katika hatua mbalimbali za kuyahitimisha.

Kwa upande wa vipaumbele katika mwaka wa fedha 2022/2023, Nkwama amevitaja baadhi ya vipaumbele vya tume hiyo ni kusimamia utumishi na maendeleo ya walimu kwa kudumisha maadili na nidhamu kwa walimu.

Ametaja kipaumbele kingine ni kuhakikisha walimu wenye sifa ya kupandishwa vyeo na kubadilishiwa kazi wanapata huduma hiyo kwa wakati baada ya kibali kutolewa na mamlaka husika na ukamilishaji wa muundo wa maendeleo ya utumishi na mishahara wa tume.

Pia ametaja vipaumbele vingine ni kuanza kutumia mfumo wa kielektroniki wa usimamizi wa masuala ya utumishi wa walimu kwa majaribio na kuendelea kutoa elimu kwa watumiaji wa mfumo huo kuanzia ngazi ya shule.