Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wakulima ufuta Lindi waiangukia Serikali

Ofisa uendeshaji biashara ya soko la bidhaa Tanzania (TMX), Mahamu Kadikilo akiwaelekeza wakulima jinsi wanunuzi wanavyoshindana  bei ya ununuzi wa ufuta. Picha na Bahati Mwatesa

Muktasari:

  • Wakulima hao wanataka ruzuku ya pembejeo kama inavyofanyika kwenye zao la korosho, ikiwemo sumu ya kuulia magugu pamoja na dawa.

Lindi. Wakulima wa ufuta Mkoani Lindi wameiomba Serikali kuwapatia ruzuku ya pembejeo kwa ajili ya zao hilo.

Wakulima hao wanataka ruzuku ya pembejeo kama inavyofanyika kwenye zao la korosho, ikiwemo sumu ya kuulia magugu pamoja na dawa.

Akizungumza leo, Julai 24, 2024, mkulima Ahmad Mkupa kutoka Kijiji cha Mnolela, Halmashauri ya Mtama, amesema zao la ufuta halina ruzuku, na wameiomba Serikali kuwapatia sumu ya kuulia magugu pamoja na dawa ya kuulia wadudu, pamoja na mbegu ya ufuta wanasubiri iwajibu.

"Sisi wakulima wa ufuta, kilio chetu kikubwa ni kuiomba Serikali itusaidie kwa ruzuku ya pembejeo kwenye zao hili, kwa kutupatia sumu ya kuulia magugu, dawa ya kuulia wadudu pamoja na mbegu," amesema Mkupa.

Licha ya kutaka ruzuku ya pembejeo katika zao la ufuta, wakulima hao wameishukuru Serikali kwa jitihada kubwa wanazofanya kuleta mfumo wa uendeshaji biashara la soko la bidhaa Tanzania (TMX), ambao kwa sasa wanaona matunda yake.

Shukuru Mazome kutoka Kijiji cha Nangano, Wilaya ya Liwale, amesema kuwa awali walikuwa hawauelewi mfumo wa TMX, lakini siku zinavyozidi kwenda wamekuwa wakiuelewa, na kusema kuwa umesaidia bei kutoshuka kama kwenye mfumo wa zamani.

"Huu mfumo, wakulima wengi tulikuwa hatuelewi, ila sasa hivi tumeshaelewa. Kwanza bei hazijashuka sana, ingekuwa mfumo wa boksi sasa hivi ufuta ungekuwa hadi Sh.2000. Tunaishukuru Serikali kwa kuleta huu mfumo, ni mfumo mzuri sana," amesema Mazome.

Sharifa Mzuwele kutoka Kijiji cha Likunja, Wilaya ya Ruangwa, amesema kuwa mfumo wa TMX umesababisha hata wanaume zao kushindwa kuwaibia fedha, kwa sababu mnada unapoendeshwa wanakuwepo na wao wenyewe kuangalia bei inayotolewa na wanunuzi.

"Zamani mnada wa boksi, wanunuzi walikuwa wanaambiana waongeze bei gani, lakini sasa hivi kila mtu anaomba kwa bei yake na hawajuani. Mimi niishukuru Serikali kwa kuleta mfumo huu wa TMX lakini pia kuleta mizani ya kidigitali, unapoenda kupima unaonesha kabisa kilo zako," amesema Mzuwele.

Ofisa Uendeshaji wa Biashara la Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), Mahama Kadikilo, amesema kuwa kupanda kwa bei ya zao la ufuta kunatokana na wanunuzi kushindana kila mmoja kutaka kupata mzigo, hali inayoongeza tija kwa wakulima kuuza kwa bei za juu na kuwapa moyo wa kuendelea kulima.

"Mfumo huu unaushindani mkubwa. Wanunuzi wanavyoshindana bei inachochea kuongeza uchumi kwa mkulima mmoja mmoja pamoja na kuongeza pato kwa mkoa na Taifa kiujumla," amesema Kadikilo.

"Wakati tunaanza tulipata changamoto kubwa ya mtandao, lakini hadi sasa minada inaendelea vizuri na bei zinaendelea kupanda kila wakati," ameongeza.