Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wakulima nchini wahimizwa kulima mazao ya asili

Dk Stephan Nindi, Naibu Katibu wa Wizara ya Kilimo.

Muktasari:

  • Wakulima zaidi ya 16,000 nchini wanatarajia kunufaika na mradi huo kutoka katika shirika la hisani ya watu wa Uswisi la SwissAid.

Dar es Salaam. Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayeshughulikia masuala ya maendeleo ya  mazao, usalama wa chakula pamoja na ushirika, Dk Stephen Nindi ametoa wito kwa wakulima kuyakumbuka mazao ya asili ambayo kwa sasa yanaonekana kusahaulika nchini.

Nindi ameyasema hayo Julai 8, 2025 wakati wa ufunguzi wa awamu ya pili ya mradi wa Crops 4HD II unaolenga kuboresha na kufufua mbegu na mazao ya asili ambayo yamesahaulika kwa muda mrefu kama vile njugu mawe, mchicha, mgagani, mbegu za maboga pamoja na ulezi.

"Tumeona kupitia utajiri mkubwa wa uwepo wa mbegu na mazao haya ya asili katika mkoa wa Lindi na Mtwara wameweza kujipatia kipato, huduma bora ya afya. Mradi huu ukisaidiwa na miradi mingine imeweza kupunguza uhaba wa chakula kutoka asilimia 49 mpaka 29 ni mradi ambao una matokeo makubwa,"amesema.

Amesema Serikali ikishirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ikiwemo SwissAid, walitekeleza mradi wa kwanza ambao ulikuwa na lengo la kufufua matumizi mbalimbali wakianzia Lindi na Mtwara lakini baadaye utaalamu huu utaenezwa sehemu mbalimbali nchini.

"Awamu ya kwanza iliangazia katika kupata takwimu za msingi na kujua hali halisi ya  mbegu za mazao hayo upo kwa kiasi gani katika mikoa yetu Lindi na Mtwara. Ambayo imeonesha kuna mazao mengi na mbegu nyingi za asili na ambayo yanafanya vizuri lakini matumizi yake hayakuwa makubwa sana.

"Awamu ya pili ya mradi huu italenga katika kuhakikisha matokeo chanya ambayo tuliyapata Lindi na Mtwara yaendelezwe kwa wilaya nyingine ndani ya mikoa hiyohiyo. Lakini pia katika mikoa mingine hapa nchini ambapo kuna utajiri wa hizi mbegu zetu  za asili na ambazo tumekuwa hatuzitumii kwa muda mrefu kwa hiyo wenzetu wa SwissAid wataongoza jopo la wadau wa kimaendeleo katika kuhakikisha tunaongeza utambuzi pia  kwa ajili ya kuimariSha afya na kupata kipato,"amesema

Aidha wakulima zaidi ya 16,000 nchini wanatarajia kunufaika na mradi huo kutoka katika shirika la hisani ya watu wa Uswisi la SwissAid.

Kwa upande wake Ofisa Miradi Mwandamizi na Mratibu wa Crops 4HD kutoka SwissAid,  Veronica Masawe amesema mradi huo una malengo ya kuongeza usalama wa chakula na lishe, kuongeza ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi, kuhifadhi na kuhakikisha kuna matumizi makubwa ya mbegu za asili hususan za mazao yaliyosahaulika na yasiyopewa kipaumbele

"Kupitia mradi huu tumeweza  kuanzisha benki za mbegu za wakulima 15. Kupitia benki hizo wakulima wameweza kubadilisha mbegu na kuwa na uhakika wa kuotesha, pia tumeweza kufikia zaidi ya wakulima 8,000 ambao wamefundishwa mbinu  za ukulima ekolojia hivyo wameweza kupambana na mabadiliko ya tabianchi na kuongeza uzalishaji wa mazao yao.”

"Kwenye awamu ya pili tunaenda kufanya kazi na zaidi ya wakulima 16,000 ambao tutafanya nao katika uzalishaji wa mazao ya kilimo hai, kuongeza benki za mbegu na uhai wa haya mazao lakini pia tutafanya kazi na watafiti ili zipatikane mbegu nzuri,"amesema.