Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wakopaji mtandaoni wanavyodhalilishwa

Muktasari:

  • Unaweza kusema mikopo hiyo ni zaidi ya ile iliyopachikwa jina la “Kausha damu” kwa kuwa ina riba kubwa ambayo haiwekwi wazi kwa wakopaji.

Dar es Salaam. “Dawa ya deni kulipa,” ni msemo unaotumiwa na watu wengi wanaodai fedha zao wakimaanisha ili kumalizana ni lazima mdaiwa alipe kile alichokopeshwa.

Mbali na msemo huo, hivi sasa watu hukumbushwa kulipa deni kwa njia ya ujumbe mfupi (sms) kwenye simu ya mhusika na kupitia watu wengine, ambao mkopaji anawasiliana nao mara kwa mara, haijalishi ndugu wala rafiki zake.

Kutokana na watu wengi kuwa uhitaji fedha, kumekuwepo na aplikesheni  nyingi mtandaoni za mikopo ya ‘chapchap’ na kila moja ikiwa na kiwango chake, lakini zote zikinadi ni mkopo nafuu na wa haraka bila masharti.

Unaweza kusema mikopo hiyo ni zaidi ya kausha damu kwa kuwa imekuwa na riba kubwa ambayo haiwekwi wazi kwa wakopaji hadi pale anapokuwa amechukua fedha.

Kutokana na utaratibu huo, wakopaji wenye tabia ta ama ya kutolipa au kuchelewesha marejesho, wanadhalilishwa kwa ujumbe mfupi wa madeni kutumwa kwa watu ambao namba zao hukutwa kwenye simu ya mkopaji.

Ujumbe huo umekuwa ukisomeka: “Ndugu wa karibu/jamaa /rafiki/jirani wa (jina la mkopaji  na namba za simu)… aliyechukua mkopo kwa njia ya mtandao kupitia Application ya … unafahamishwa kuwa mtu huyu amekiuka makubalianao kwa kutolipa deni siku husika ya marejesho na kutopokea simu za ofisi, hivyo tutamchukulia hatua kwa kosa hilo.

“Unaombwa kumpigia simu muhusika na kumjulisha kuwa ana masaa mawili ya kulipa deni kabla hatua kali hazijachuliwa dhidi yake. Fanya hivyo kuepuka usumbufu.”

Ujumbe huu ni kinyume na kanuni za ukusanyaji madeni kwa mujibu wa Toleo la Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha 2019 ibara ya 56, kifungu cha 1, (c,d)  kinachokataza “kumtisha au kutumia nguvu au njia zisizo halali katika kukusanya au kufuatilia deni; pia kutotumia lugha ya fedheha au isiyofaa.”

Vilevile, kuna tatizo jingine la kudukua taarifa za mteja na kutafuta namba za simu alizozihifadhi kwenye simu yake na kuzitumia ujumbe wa vitisho.


Kudukua hatua ya mwisho

Mmoja wa viongozi wa kampuni moja inayotoa mikopo kwa njia ya mtandao ambaye hakutaka jina lake litajwe, anasema kudukua taarifa za mteja wao ikiwamo kuchukua namba za watu wake wa karibu, ni hatua ya mwisho baada ya kufanya jitihada za kumtafuta kwa mfumo wa kawaida kushindikana.

“Ikitokea mteja amekuwa sugu tunaangalia faili lake kuna namba mbili anaziandika za wadhamini tukiwatafuta hawapatikani au ni wasumbufu, tuna tumia mfumo wetu uliounganishwa na namba za mhusika na unawezesha kuona hadi namba za watu wake wa karibu anaowasililiana nao mara kwa mara, kisha tunawatumia ujumbe,” amesema.

Pia, amesema kwa sheria ya kampuni yao kufanya marejesho mwisho ni saa 05:00 asubuhi lakini muda huo hawajauweka wazi kwenye mitandao yao, lakini wanaochukua mikopo wanaelezwa sharti hilo kabla ya kupewa fedha.

“Tumeshindwa kuweka wazi kwenye mitandao kwa sababu mifumo yetu ina changamoto na bado tunajaribu kuangalia teknolojia ya kutuwezesha kila mmoja aone ili ukikopa fedha zirudi kwa wakati tuwakopeshe wengine.”

Amesema wamekuwa wakiwasisitiza wateja wao kufanya marejesho mapema na kuwa wanapochukua wanakubali lakini wakati wa kurejesha wamekuwa wakitoa visingizio vingi ikiwamo kudai wamefiwa au wanauguza.

“Muda ukifika kampuni huwa inahitaji fedha zake bila kujali mteja anapitia katika hali gani au kapatwa na msiba, tunachohitaji malipo yetu tupewe kwa wakati,”amesema kiongozi huyo.


Waliotumiwa ujumbe

Akizungumza na Mwananchi, Mkazi wa Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam, Ramadhan Rajab ambaye alitumiwa ujumbe wa namna hiyo amesema alipopata ujumbe alimtafuta muhusika na kumuuliza na yeye alikiri kudaiwa.

“Nilipomtafuta muhusika akakubali anadaiwa, nilimuuliza ameshapigiwa simu na watu wangapi, alisema ni wengi na walijua wanaofanya hivyo ni matapeli au yeye ameibiwa simu,” anasema Rajabu.

Amekitaka Serikali isimamie utaratibu wa kuendesha hizo biashara akisema kwa sasa zinafanyika kiholela na kuwapa uhuru wa wahusika kuwachanganya wananchi.

Ashura Omary, mkazi wa Tabata, Dar es Salaam anasema ametumiwa ujumbe wa wadaiwa zaidi ya watatu na alipojaribu kuuliza endapo aliwekwa kuwa mdhamini walikataa na kushangaa wakopeshaji walijuaje namba za watu na kuwatumia ujumbe.

"Mara ya kwanza kuona ujumbe nikajua ni matapeli wanafanaya kama zile sms nyingine, nikatumiwa tena kwa jina la mtu mwingine nikapuuza, nimekaa kidogo ikaingia nyingine ikabidi niwapigie wanaotajwa wakaniambia wamekopa mtandaoni na wamechelewa kulipa kwa hiyo watu wanatumiwa ujumbe," anasema Ashura.


Wakopaji walonga

Jackson Kalongo, dereva wa bajaj Buza alisema wakati anakopa hakujua kama wanatuma ujumbe kwa watu pindi anapochelewesha rejesho.

“Nimekopa Sh100, 000 nimeshalipa Sh40,000 nikapitiliza kulipa, wakawa wanapiga simu kila nikiwaelewesha hawanielewi, mwisho nikaamua kutopokea simu zao. Cha ajabu napigiwa simu na watu tofauti kuwa nadaiwa,” amesema Jackson.

Jackson amesema kitendo hicho kimemdhalilisha kwa kuwa  hakuwa na lengo la kutokulipa, lakini wamefanya asilipe kabisa kwa sababu imemkosesha baadhi ya kazi kwa kutoonekana mwaminifu.

Sabrina Jabir, mkazi wa Magomeni aliwataka watu kutoingia kwenye aplikesheni za mikopo hata kama wana shida kwa kuwa zinafedhehesha hadi kwa watu ambao unawaheshimu.

“Sina hamu na mikopo ya mitandao wametuma sms hadi kwa wakwe zangu, naonekana mdaiwa sugu na sijui namba za hao watu wametoa wapi wakati sijawapa namba,” anasema Sabrina.

Anasema utaratibu wanaotumia si mzuri kwa kuwa wanapoomba mkopo hakuna sehemu ya kuandika wadhamini, hivyo anaamini kuwa ni makubaliano ya wao wenyewe.

Grace Kazonda, mkazi wa Mtongani, Dar es Salaam anasema alipopigiwa simu ya kulipa deni aliwaambia kuwa atalipa ingawa amepitiliza siku moja na wao walimwambia watamkomesha.

“Unaweza waambia nimepitiliza siku moja nitawalipa baada ya siku mbili wao wanasema ngoja tukuaibishe, niliwajibu kama mnaona hilo linawapa ufumbuzi, basi endeleeni nitawafurahisha,” alima Grace.

Alisema baada ya kutumwa ujumbe kwa ndugu zake aliwaambia kuwa ameibiwa simu kwa hiyo wezi wameamua kutuma ujumbe huo kwa watu ili kujipatia pesa.


Kauli ya TCRA

Alipoulizwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Mawasiliano (TCRA), Dk Jabiri Bakari amesema wanaopaswa kuulizwa kuhusu suala hilo ni Benki Kuu ya Tanzania kwa sababu wana mifumo yao ya kifedha. 

"BoT kila mara tunawaeleza unapoona Tigo Pesa au M Pesa, Halopesa wale wanapewa leseni na kusimamiwa na Benki Kuu.

"Kama unavyoona sisi kwenye Interneti ukimfuata tigo ana leseni tatu kati ya hizo mbili ni za kwetu kwenye miundombinu na mifumo, lakini zinazohusu fedha zinasimamiwa na Benki Kuu na siku za hivi karibuni walitoa matangazo mengi kuhusu hiyo mikopo na matatizo yanayojitokeza," amesema Dk Jabiri.


BoT haina taarifa

Akizungumza na Mwananchi kuhusu mikopo hiyo, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba anasema hana taarifa na hajapata uthibitisho wa nani alikopa kwa nani na taarifa zake zimetolewa kwa mtu gani.

Anasema suala la mkopo linahusisha mkopeshaji na mkopaji, hivyo taarifa zote za mkopo zinatakiwa kutunzwa kwa kipindi cha makubaliano.

“Mtu akivunja makubaliano kunakuwa na adhabu kwenye riba ikiwa ni hatua ya kumtaka awe na uchungu wa kurejesha, lakini kuna wakopaji wengine wanakuwa wakaidi na katika ufuatiliaji kila mtu anatumia mbinu mbalimbali,” amesema Tutuba.

Pia, amesema kwa sasa hawajaona taarifa rasmi kuhusu nani ametumiwa taarifa hizo, lakini inategemea mkopaji ameambiwa mara ngapi na mkopeshaji na ikitokea amepitiliza kuna hatua zinachukuliwa ikiwamo kumtangaza kwenye vyombo vya habari.

Tutuba amesema wanatangaza kwenye vyombo vya habari kuonyesha mkopaji si mwaminifu, hivyo anawataarifu wakopeshaji wengine wanaotaka kumkopesha  wajue ni mtu huyo ni hatari.

“Mtu asipolipa mkopo kutangazwa ni kawaida, ndiyo maana hata Serikali ilifungua jukwaa kwenye mtandao kuna orodha ya wakopaji kuzisaidia benki kujua historia ya mkopaji,” amesema.

Hata hivyo, alisema wakipata uthibitisho wa kujua mkopaji alichukua kiasi gani, alipitiliza kwa muda gani na walipeana mkopo kwa makubaliano gani, wataliangalia na kulichambua zaidi.