Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

VIDEO: ‘Kausha damu’ inavyokausha mpaka lishe kwa familia

Muktasari:

  • Wakopaji wa mikopo umiza ya mitaani ni kina mama ambao ndiyo waandaaji wa vyakula majumbani. Wanapokosa pesa za kurejesha mikopo hiyo, hutumia za chakula walizoachiwa na wame zao kulipia, kisha kuilisha familia kinachopatikana kutokana na pesa iliyobaki. Hali hiyo imeelezwa kuifanya familia kukosa lishe na kuongeza udumavu.

Dar es Salaam. Tanzania ikipambana na tatizo la utapiamlo na udumavu kwa watoto, umasikini wa kipato umetajwa kuwa miongoni mwa sababu za familia kukosa mlo unaotakiwa kukidhi lishe.

Hali ya umasikini imesababisha baadhi ya wanawake kujiingiza kwenye mikopo inayotajwa kuwa na masharti magumu maarufu ‘Kausha damu’ hivyo kujikuta wakiongeza changamoto zaidi hasa ya lishe katika familia.

Miongoni mwa wengi ni wanawake watatu waliozungumza na Mwananchi hivi karibuni.

Upendo Swai, anayeishi Mtaa wa Sabasaba, Kwa Aziz Ally wilayani Temeke anasema alichukua mkopo kuongeza mtaji wa biashara ya sabuni na dawa ya kuondoa madoa, pia kuwatunza marafiki zake waliompa zawadi kwenye sherehe alizokuwa ameandaa.

“Nilishiriki mikopo ya kausha damu, ukichukua Sh50,000 unatakiwa kila siku urejeshe Sh2,000. Ikitokea siku umekosa, wanakupiga faini na kama utaendelea kushindwa wanakuja kukufilisi vitu vyako vikiwamo vya ndani,” amesema.

Kwa kulipa Sh2,000 kwa siku maana yake kwa mwezi atakuwa amerudisha Sh62,000.

Katika mikopo hiyo, baadhi ya wakopeshaji huchukua mali za wakopaji endapo wanashindwa kumaliza deni kwa wakati.

“Kwenye mkataba wao kama umeandika kabati au televisheni au samani za ndani, ambazo endapo utashindwa kulipa mkopo huo wanakuja kuvichukua,” amesema.

Ameendelea, “Ilifika mahali nakosa hela ya kuwapikia chakula watoto na mume wangu. Mara nyingi naachiwa Sh10,000, natoa Sh2,000 ya kausha damu, natoa michango ya jamii, mwisho nakuta nina hela kidogo tu ya kuandaa chakula. Siwezi kutumia hela ya biashara zangu maana bado mtaji ni mdogo,” amesema.

Pamoja na ugumu wa masharti unaotajwa na wakopaji, baadhi yao pia wanatumia vibaya mikopo hiyo.

“Sisi wanawake tuna tabia ya kupeana. Ukienda kwa shoga yako lazima na yeye aje na nisipomlipa linakuwa deni, hivyo ni lazima niende kausha damu nikakope ili nilipe hilo deni, mume wangu anatoka saa 11.00 asubuhi, anarudi usiku, kwa hiyo hapa katikati hajui kinachoendelea.”

“Mchana tunapitisha bila kula, watoto wakienda shule wanashindia mihogo huko, halafu usiku ndiyo naandaa chakula, na mume akija anakuta chakula kizuri hajui kama mchana kila mmoja alijijua mwenyewe kuhusu mlo,” amesema.

Hata hivyo, Upendo amesema aliachana na mikopo hiyo baada ya kuona hali ya lishe katika familia yake inayumba na hapati maendeleo yoyote.

Maelezo kama hayo ameyatoa Fatuma Ally anayeishi mtaa huo. Amesema analazimika kukopa kutokana na ugumu wa maisha.

“Niliwahi kushiriki mikopo kausha damu kutokana na ugumu wa maisha, nina baba na mama wananitegemea maana nimeshakuwa  mkubwa na umeolewa. Mume mwenyewe hela hana.”

“Kwa siku mume ananiachia Sh10,000 ya matumizi, kuna watoto kwenda shule, walimu wenyewe wanataka hela, mara utaambiwa kuna mitihani, kuna hela ya mlinzi, kwa hiyo unajikuta watoto wanaondoka na Sh3,000, unabaki na Sh7,000.

“Hapo unaambiwa baba anaumwa, ukimwambia mume, anakwambia hana hela, unapoenda kuwauliza marafiki zako wanakwambia nenda mahali utapata hela, ndipo hapo kausha damu, unakopa. Kwa hiyo, nilipokopa nikapeleka kumtibu baba yangu, kulipa ni kila siku,” ameeleza.

Amesema, “Nikishatoa Sh3,000 ya watoto kwenda shule kila siku, natoa Sh2,000 marejesho mkopo wa kausha damu, itabaki Sh5,000. Haiwezi kutosha kuwapa chakula watoto wakirudi shule, hivyo watakula mihogo. Hapo atakayekula zaidi ni baba kwa sababu ndiye mtafutaji.

Fatuma amesema baada ya kukamilisha marejesho ya mkopo wa kwanza kwa mbinde na baba yake akawa amepona, akaingiwa na tamaa, akakopa tena.

Hata hivyo, amesema aliamua kuachana na mikopo hiyo baada ya kuona inamyumbisha hasa kwa malezi ya watoto.

Kwa upande wake, Latifa Ungani, ambaye haishi na mume bali analea watoto wake wawili amesema aliingia kwenye madeni ya mikopo hiyo kukidhi gharama za maisha.

“Kuna wakati nilichukua mkopo ikaniwia vigumu kulipa, ikafika mahali ikawa naogopa kurudi nyumbani. Nikiondoka asubuhi mtoto anaenda shule na mwingine naondoka naye, tunarudi usiku, na wakati mwingine hatuli mchana,” amesema.

Edward John anayesoma darasa la tano katika Shule ya Msingi Mtoni Sabasaba wilayani Temeke amesema kila akiondoka asubuhi na mdogo wake, wanapewa Sh2,000 ya kula shuleni.

“Tukirudi nyumbani mchana, tumeshakula mihogo, mama anasema tusubiri chakula cha jioni ndio tunakula. Kuna wakati tunakuta chakula na siku nyingine hatuli hadi jioni,” amesema.

Mwanaisha Ally mkazi wa Gongolamboto ameeleza kuwa mtindo wa kupeana fedha katika vikundi vyao ndiyo ulioyumbisha familia yake katika lishe.

“Sisi tuna kikundi hapa mtaani, huwa tunapeana fedha, kila siku Sh2,000 ambazo baadaye anapewa mtu mmoja. Usipotoa, unapigwa faini na kama utaendelea hivyo wanakutoa, hivyo ni lazima nitumie hela niliyopewa na mume kuhakikisha nalipa.

“Wakati mwingine najinyima, sili mchana ili kupata hiyo hela, kwa sababu nikiwa na shida, hiki kikundi kinanisaidia,” amesema.

Amefafanua kuwa kama binadamu ana kila sababu ya kujichanganya na wanawake wenzake kwenye hivyo vikundi. “Siwezi kuishi kama nipo kisiwani, lazima nijichanganye na wenzangu kwani nikiwa nina shida ndiyo wananisaidia, kwenye kurejesha nikikopa hapo ndiyo huwa najuta, ila huwa vinanisaidia sana.

Naye Monica Mchamba anayeishi Kinondoni Moscow, amesema alilazimika kukopa ‘Kausha damu’ ili kuongezea mtaji wake wa biashara ya genge.

“Tatizo ni marejesho kila siku, kwa mfano unakopa Sh100,000 unatakiwa ulipe Sh5,000 kila siku, wakati biashara yenyewe inapanda na kushuka. Hapo ni lazima upunguze hela ya chakula cha siku ulipe madeni, lakini yote kwa yote tunapambana ili tuishi.”

“Ukisema ukae bila kukopa hata watoto hawatasoma shule nzuri, changamoto ni kukosa dhamana kama wenzetu waliopo makazini na kwingineko ndiyo maana tunanyonywa na hawa wakopeshaji na hatuna namna lazima twende kwao maana hatutambuliki kwenye mabenki,”amesema Monica.


Wasemavyo wanaume

Salim Mkeni anayeishi Kurasini wilayani Temeke amesema aligundua kuwa mkewe amekopa mikopo hiyo, baada ya hali ya lishe kwa watoto kuwa ngumu, licha ya kumwachia fedha.

“Hali ya maisha ni ngumu, kwa hiyo siku nyingine naacha Sh10,000 siku nyingine chini ya hapo. Nikirudi usiku nakuta chakula kimepikwa tunakula wote na watoto.

“Siku nyingine nikiwahi kurudi mchana nakuta hajapika kitu chochote, nikiuliza, anasema hela haitoshi, yaani maana yake hapo hata watoto hawajala. Nilipofuatilia zaidi nikagundua nikiacha hela ya chakula anaigawa ili apate na ya kupeleka kwenye  marejesho ya mkopo, ilibidi tu nimsaidie kuumaliza, vinginevyo hali ingekuwa mbaya,” amesema.

Ferouz Kakozi ambaye ni mjasiriamali anayeuza mashuka na sabuni kutoka Kigoma, ameeleza jinsi alivyomkopesha bidhaa zake mwanamke mmoja aliyekuwa kwenye janga la mikopo hiyo na hatimaye kujikuta kwenye hasara, kwani hakulipwa.

“Kuna mteja mmoja alikuja kwangu akanikopa shuka niliyokuwa nauza Sh80,000 na marejesho ni miezi miwili, nikampa. Akanipa Sh10,000 ya mwanzo.

“Baadaye akanifuata tena, akasema ile nyumba anayokaa kuna mtu mwingine anahitaji shuka. Nikamwambia mtu mwingine sitampa labda umdhamini wewe, akakubali kudhamini, nikampa,” amesema.

Amesema tangu wakati huo alihangaika kumtafuta bila mafanikio, lakini alikuja kugundua kuwa mwanamke huyo anasumbuliwa na madeni na alikuwa hapokei simu. 

Baada ya kuanza kupoteza matumaini, amesema alimtafuta mumewe na kumweleza kuhusu deni hilo.

“Mumewe aliniambia kuwa mkewe ametoweka nyumbani, kwa sababu ya kukimbia madeni hayo. Akasema ameshamsaidia mkewe kulipa madeni lakini ni mengi kiasi kwamba hata lishe kwa watoto imekuwa mbaya kwa sababu kila hela anayoiona anawaza madeni anasahau hata umuhimu wa kula,” amesema. 

Baada ya mahangaiko ya muda mrefu, Kakozi amesema alikwenda kushitaki mahakamani na alishinda kesi.

“Kuna siku nilikwenda kwake ili nichukue vitu vya ndani, huwezi kuamini hali niliyoikuta ilikuwa ngumu. Ana watoto wanne halafu wamekonda na bado ana mimba, ndani hakuna hata kitanda na hicho chumba wamepanga.

“Ilifika kipindi mimi ilibidi nisamehe lile deni, yaani ile hela yote imepotea,” amesema.


Serikali ya Mtaa

Amani Mbutu, mjumbe wa Mtaa wa Sabasaba jijini Dar es Salaam, amesema tatizo ni wanawake kukosa elimu ya mikopo.

“Wanawake wengi wakishakopa wanapeleka fedha kutunza rafiki zao kwenye sherehe za kuzaliwa, na wanaofaidika ni wale wenye kawaida ya kwenda kwenye sherehe za wenzao na kupeleka alichonacho.

“Anaweza kwenda kwa shoga yake akamtuza Sh200,000 na siku shoga yake akija anamtuza Sh300,000 au Sh400,000, ina maana yule aliyetunzwa awali na yeye anarudisha mara mbili au moja na nusu,” amesema. 

Kuhusu utaratibu wa kuchukua mikopo, Mbutu amesema wao kama Serikali za Mitaa hutoa barua za utambulisho.

“Kesi tunazopata pale Serikali ya Mtaa ni watu kushindwa kulipa madeni, hivyo waliomkopesha wanaenda kumfilisi au kuchukua vitu vilivyowekwa dhamana.

“Tunachojua ni kwamba mtu anapoenda kukopa, mkataba unaeleza akishindwa kulipa, dhamana itachukuliwa ili mkopeshaji arejeshe deni. Hata benki ndivyo ilivyo, mtu akishindwa kulipa wanaangalia dhamana,” amesema.


Watoa mikopo

Akizungumzia malalamiko kuhusu mikopo hiyo, George Mawala wa Carvas Micro-Credit Company Ltd amesema hakuna unyanyasaji wowote kwa wakopaji bila kujali ni wanawake au wanaume, kwa kuwa mikopo inafuata utaratibu wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT). 

“Hakuna unyanyasaji wala malalamiko yoyote kwa sababu kwanza riba zetu ni ndogo ambayo ni asilimia 3.5 na inapungua kwa kadiri anavyolipa marejesho mengi zaidi,” amesema.

Hata hivyo, amesema wanawake ambao ndiyo walengwa wa mikopo hiyo hawatekelezi malengo waliyokusudia. 

“Unakuta mwanamke amechukua mkopo wa Sh100,000 au Sh200,000 kwa ajili ya biashara lakini hapeleki kwenye biashara, bali anatumia kwa mambo mengine halafu anategemea biashara ndiyo irejeshe mkopo.

“Ndiyo maana wapo wanawake unaweza hata ukampa Sh1 milioni bila riba, lakini atachukua ataenda kulipa ada, ataenda kununua vitu vya nyumbani hapeleki kwenye biashara.”
 

“Siku ukija kumkumbusha kurudisha, inabidi aitoe tena kwenye biashara ili alipe deni. Hiyo ndiyo changamoto na hapo ndiyo wanalalama kuonewa,” amesema.

Kuhusu kuwatembelea wakopaji nyumbani na kukagua mali zilizopo, amesema ni ulinzi wa mkopo.

“Kwetu mdhamini tunayemkubali ni mwenye makazi ya kudumu, haturuhusu mume amdhamini mkopaji, ila tutamjulisha kuwa mkeo amekopa hapa. Haturuhusu mume awe mdhamini, kwa sababu ikitokea wamehama maana yake watahama wote bila kulipa deni,” amesema.

Kwa upande mwingine, mmoja wa wakopeshaji ambaye hakutaka kuandikwa jina lake wala la kampuni yake, amesema ili ujiepushe na  malalamiko ya wakopaji wanawachuja.

“Sisi hatukopeshi kila mtu, tunaangalia mwenye biashara na tunaitathmini ili kujua tumkopesheje,” amesema. mkopeshaji huyo mwenye ofisi yake Mtoni kwa Aziz Ali wilayani Temeke.

Ameendelea kusema kuwa , “Huwa tunatoa elimu kwa wakopaji na tunaangalia ili wajue malengo ya kukopa na endapo mtu atashindwa kulipa mkopo, tunampa muda zaidi. Tatizo baadhi ya wakopaji hasa wanawake wanapochukua hela, wanakwenda kutuza wenzao kwenye sherehe.”


Kauli ya BoT

Gavana wa Beki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba amekiri benki hiyo kusikia malalamiko ya wananchi kuhusu mikopo hiyo, akisema kwa sasa wamechukua hatua ya kutoa elimu kwa wakopeshaji, halmashauri kupitia Ofisi ya Rais (Tamisemi) na wakopaji.

Ametaja makundi manne ya mikopo, ambapo mikopo hiyo midogo ipo kundi la pili na la kwanza ni mikopo ya benki.

Kundi la tatu ni la vyama vya ushirika wa kuweka na kukopa (Sacco’s) na kundi la nne ni la vikundi vya kijamii (Vicoba).

“Ni kweli tumesikia hayo malalamiko ya wakopeshaji na wengine wanaita mikopo kausha damu na wengine mikopo umiza.

“Sheria yetu imetungwa mwaka 2018, lakini mikopo imekuwepo miaka mingi kabla hata Yesu Kristo hajazaliwa, ndiyo maana utasikia huyu alipewa talanta akazizika chini ya ardhi na mengineyo.

“Sisi Benki Kuu tumekuwa tukitoa elimu, kwanza kwa wakopeshaji kukata leseni na pia waweke wazi masharti na vigezo vyao. Halafu hivyo vigezo visiwe vigumu kwa wakopaji, hata kama tuko kwenye uchumi wa soko huria, visilete taharuki,” amesema Tutuba.

Amesema miongoni juhudi za kutoa elimu ni ujumbe wa simu unaosambazwa kwa wananchi ili waelewe mikopo hiyo.

“Kopa kwenye taasisi yenye leseni ya Benki Kuu ya Tanzania kuepuka usumbufu. Zingatia malengo ya mkopo, elewa mkataba na ubaki na nakala iliyosainiwa,” unasomeka ujumbe huo.


Lishe

Kutokana na maelezo ya wananchi hao, ni wazi kuwa idadi kubwa ya watu wanakosa lishe bora kwa siku kutokana na changamoto za maisha.

Akieleza kuhusu mwongozo huo, Ofisa lishe mwandamizi mtafiti wa TFNC, Maria Ngilisho amesema mtu anatakiwa kula makundi sita kwa siku, hapo maana yake mtu ale mara tatu kwa siku.

“Mtu akila hivyo kuna nishati lishe anayotakiwa kula ifike 2,300 (calories).

“Kwa siku nzima inatakiwa ale asilimia 36 ya wanga, asilimia 10 ya vyakula vya asili ya nyama, asilimia 18 vyakula ya vyamii ya kunde, maharage karanga na mbegu, asilimia 17 mbogamboga, asilimia 17 matunda na asilimia 2 mafuta ambayo yanapikia chakula,” amesema.


Utafiti

Hayo yanajiri wakati utafiti huo unaoitwa ‘Mgawanyo wa Jinsia katika ulaji wa Chakula kwa Kaya Tanzania’ uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Jamii (ESRF) mwaka 2022 kwa Wilaya ya Temeke (Dar es Salaam) kuonyesha uwezekano wa wanawake kukosa lishe bora kutokana na umaskini wa kipato, hadhi ya kijamii ya chini, ukosefu wa elimu ya uzazi.

Utafiti huo pia umebaini kuwa wanawake ndio wenye uamuzi wa chakula kipi kinunuliwe, kipikweje na ratiba ya kula. Hata hivyo, jukumu la kutoa fedha za chakula limebaki kwa wanaume, wakisaidiwa na wake zao.

“Wanaume wengi wamejiajiri kwenye biashara ndogondogo na vibarua kwenye sekta zisizo rasmi, hivyo hawana uwezo wa kuacha fedha za kutosha mahitaji ya familia.”

Katika eneo hilo utafiti umebaini kutokueleweka kwa tofauti ya lishe kulingana na makundi wakiwamo wajawazito, ambapo imeelezwa, tofauti na watoto na wagonjwa wanaopata lishe bora, wengine (wanawake, wanaume) hula chakula sawa.

“Nyumba nyingi hula milo mwili, mmoja asubuhi na mwingine jioni, bila kujali hali zao kama watoto, wajawazito, watu wote wanakula milo miwili,” unasema utafiti.

Utafiti huohuo umeeleza kuwa wanawake wenye vipato vya chini wako hatarini kukosa lishe bora kwa kujiingiza kwenye mikopo inayowalazimisha kuwajibika kuilipa hata kwa fedha wanazotakiwa kuandalia chakula.

Unataja Benki za jamii vijijini (Vicoba) kuwa miongoni mwa sababu za wanawake wengi kujikuta njiapanda na hatimaye kuzinyima lishe familia zao.

Kulingana na utafiti, ili kupata mikopo, wanachama wanatakiwa kununua hisa fulani (kwa mfumo wa michango ya fedha) ambayo inagharimu hadi Sh2, 000 kwa hisa. Kiasi cha mkopo kinachotolewa kinategemea idadi ya hisa zinazomilikiwa na watu binafsi.

“Hata hivyo, wanawake wengi wanashiriki katika Vicoba hivyo wanalazimika kutafuta fedha zaidi ili kulipa michango yao ya kawaida na au kurudisha mikopo yao.

“Matokeo yake wanakimbilia kupunguza mgawo wa bajeti ya kaya kwa chakula ambacho kwa upande mwingine huathiri uwezo wa kaya kununua na kupata milo ya kutosha,” unasema utafiti huo.

Kulingana na utafiti huo, karibu wanaume wote hutoa kati ya Sh5,000 hadi Sh10,000 na hata kidogo zaidi hivyo, wanawake wanapaswa kufikiria kwa kina jinsi ya kutumia pesa hiyo na kuamua ni nini kinaweza kupikwa kwa kutumia pesa kidogo iliyobaki.

“Inaumiza sana, hasa katika familia kubwa zenye watu 10 kwa mfano. Kilo moja ya mchele sasa inauzwa kwa bei ya wastani ya 2,500 na unahitaji angalau kilo 2.5 za mchele ambazo hufanya Sh6,250.

Utafiti unahitimisha kwa kuita serikali na wadau wasio wa serikali kushughulikia tofauti za kijinsia na sababu za kitamaduni za kijamii katika kubuni, kutekeleza, kufuatilia na kutathmini mipango inayolenga jamii kama hizo.