Madiwani Simanjiro walia na mikopo umiza, wataka ya asilimia 10 irejeshwe

Muktasari:
- Kutokana na Serikali kusitisha mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri, baadhi ya wananchi wilayani Simanjiro mkoani Manyara wamejitosa kwenye mikopo umiza na kusababisha kulipishwa riba kubwa
Simanjiro. Madiwani wilayani hapa, wameiomba Serikali kurejesha mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri ili kuinusuru jamii kujiunga na mikopo umiza na kausha damu inayowatoza riba kubwa.
Mikopo ya asilimia 10 inayotokana na mapato ya ndani ya halmashauri ilikuwa inatolewa kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu ila hivi sasa imesitishwa na Serikali.
Diwani wa viti maalumu wa Tarafa ya Moipo, Paulina Makeseni, akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani leo Januari 2, 2024 amesema hivi sasa jamii imejiingiza kwenye mikopo umiza na kausha damu inayowaumiza.
Makeseni ameiomba Serikali kurejesha mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ili kuinusuru jamii kwani wamejiingiza kwenye taasisi za fedha zinazotoa mikopo kwa riba kubwa.
Diwani wa kata ya Endiamtu, Lucas Zacharia amesema hivi sasa jamii inapitia kipindi kigumu, kwani fedha za mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ilikuwa inawasaidia.
Amesema baada ya mikopo hiyo kusitishwa hivi sasa jamii hasa wanawake wamejiingiza kwenye mikopo umiza na kausha damu inayowaumiza kiuchumi.
"Hizi taasisi za fedha zimesababisha wananchi wangu kuingia kwenye tafrani, kwani wengine wamenyang'anywa samani za ndani walizoweka dhamana na kuchukua mikopo hiyo," amesema Zacharia.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Gracian Max Makota amesema bado Serikali haijarejesha mpango wa utoaji mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani.
Makota amesema endapo mpango huo ukirejeshwa viongozi wa kisiasa wanapaswa kuwapa msukumo waliokopa warejeshe, ili wengine waweze kupata fursa hiyo.
Amesema mtu mwenye akili timamu akichukua mkopo anapaswa kurejesha na siyo kutetewa ili asirejeshe, jambo ambalo siyo sahihi hivyo wajirekebishe.
"Kuhusu hilo suala la taasisi za fedha kutoa mikopo na kunyang'anya vitu walivyoweka dhamana ikiwemo TV au chochote, tumefuatilia na wamekanusha kukamata hivyo vitu," amesema Makota.