Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wakili Mpoki kufungua kesi nane kupinga kusimamishwa

Wakili mwandamizi wa kujitegemea, Mpole Mpoki akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mpango wake wa kukata rufaa kupingwa kusimamishwa kwake kuwa wakili alipokuwa akizungumza  jijini Dar es salaam.Kushoto ni Rais mstaafu wa TLS Dkt Nshala Rugemeleza. Picha na Said Khamis

Muktasari:

  • Wakili Mpole Mpoki amesimamishwa uwakili Novemba 20, 2023 na Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Mawakili, Jaji Ntime Kilekamajenga kwa kile kilichoelezwa na Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) kuwa alikuwa akiweka mapingamizi jambo ambalo kamati ililikataa.

Dar es Salaam. Wakili Mpole Mpoki aliyefutiwa uwakili kwa miezi sita, anakusudia kufungua kesi nane ikiwemo ya kikatiba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki kupinga kusimamishwa kufanya kazi hiyo.

Mpoki amesimamishwa uwakili Novemba 20, 2023 na Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Mawakili, Jaji Ntime Kilekamajenga kwa kile kilichoeleza na Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) kuwa alikuwa akiweka mapingamizi, jambo ambalo kamati ililikataa.

Alisimamishwa uwakili wakati akimtetea mteja wake ambaye ni wakili Boniface Mwabukusi aliyekuwa anakabiliwa na makosa ya kukiuka maadili katika utendaji wake wa kazi ya uwakili.

Mwabukusi alikuwa anakabiliwa na kesi ya kukiuka maadili namba 10 ya mwaka 2023, iliyofunguliwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kuiwasilisha mbele ya Kamati ya Maadili ya Mawakili kujibu tuhuma zinazomkabili.

Katika kesi hiyo, Wakili Mpoki alikuwa kiongozi wa jopo la mawakili sita waliokuwa wanamtetea Mwabukusi, ambapo pamoja na mambo mengine aliwasilisha mapingamizi saba dhidi ya uhalali wa madai hayo, mbele ya kamati hiyo.

Akiziungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi, Novemba 23, 2023, makao makuu ya TLS, wakili Mpoki amesema hajaridhika na uamuzi huo uliotolewa na kamati hiyo  kutokana na kutoridhika huko ameamua kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kufungua kesi ya kikatiba kupinga uamuzi huo.

Pia, ameteua jopo la mawakili 26, akiwemo Dk Rugemeleza Nshalla na Dk Ringo Tenga kusimamia kesi hizo.

“Nakusudia kukata rufaa Mahakama Kuu kupiga uamuzi wa kamati wa Novemba 20, 2023. Tayari tumeshapeleka mbele ya kamati barua ya kusudio la kukata rufaa Mahakama Kuu na tumeandika barua kuomba nakala ya uamuzi huo na zinachukua muda wa siku saba kutolewa,” amesema.

Amefafanua endapo nakala hizo hatazipata ndani ya siku 10 tangu oka iku ya barua hiyo, watawajibika kuomba amri ya “Mandamus” kumlazimisha mwenyekiti awapatie nakala hizo mapema iwezekanavyo.

“Natarajia kupeleka haraka iwezekanavyo malalamiko yangu mbele ya Tume ya Maadili ya utendaji wa Majaji iliyoundwa chini ya sheria 4 ya mwaka 2011, juu ya mwenendo wa mwenyekiti wa tume hiyo ambaye kwa sababu anazozijua ameamua kunisimamisha uwakili kwa kipindi hicho bila kufuata sheria na bila kufuata utaratibu unaotakiwa,” amesema.

Pia, anakusudia kufungua kesi ya kikatiba Mahakama Kuu ya Tanzania dhidi ya mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Maadili, kwani kitendo cha kumsimamisha imempokonya haki yake ya kufanya kazi ambayo Katiba imempa chini ya Ibara ya 21(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano na haki ya kuishi kinyume cha Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Vile vile, anakusudia kufungua kesi nyingine ya kikatiba kupinga baadhi ya vifungu kadhaa vilivyomo ndani ya sheria ya mawakili vinavyopingana na haki ya asili ya kusikilizwa na kukinzana na ibara kadhaa za Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

“Nakusudia pia kufungua shauri katika Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki kwa kitendo cha kusimamishwa uwakili hakiendani na misingi ya mkataba wa ushirikiano wa Afrika Mashariki kama inavyoamrishwa kwenye ibara 6(d) kuhusiana na nchi husika kukuza na kulinda haki za watu kama ilivyoainishwa katika tamko la Afrika la Haki za Binadamu,” amesema wakili Mpoki.

“Pia, nakusudia kuwashawishi wanachama wa chama cha Sheria cha Tanganyika (TLS) kuitisha mkutano mkuu maalumu wa chama ili kujadili mwenendo wa uonevu uliofanywa dhidi yangu na “kamati” na mawakili wengine waliopita mbele ya kamati hiyo kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita” amesema wakili Mpoki.

Pamoja na hayo, amesema ameandika barua kwa mwangalizi wa umoja wa mataifa maalumu “Special Rapporteur on the Independence of Judges and Lawyers”, Margeret Salterthwale, juu ya kuporomoka kwa hali ya juu ya uhuru wa mawakili nchini inayotokana na sheria mbaya na kandamizi ya mawakili.