Wakili Madeleka afutiwa kesi ya ‘plea bargaining’, akamatwa tena

Wakili Peter Madeleka (kulia) akiwa anajadiliana na Wakili wake, Simon Mbwambo (kushoto) katika kumbi ya Mahakama Kuu Arusha, muda mfupi kabla ya kukamatwa na polisi. Picha Mussa Juma.
Muktasari:
- Jeshi la Polisi mkoani Arusha limemkamata Wakili wa kujitegemea, Peter Madeleka mara baada ya kufutiwa kesi yake ya kupinga makubaliano ya kukiri kosa.
Arusha. Wakili wa kujitegemea nchini, Peter Madeleka amekamatwa na Jeshi la Polisi katika Kituo Jumuishi cha utoaji haki baada ya kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.
Madeleka kabla ya kukamatwa alilazimika kung'ang'ania kwa zaidi ya dakika 30 katika chumba cha Mahakama cha Jaji Aisha Bade ambaye awali ndiye alitoa maamuzi katika kesi yake ya kupinga makubaliano ya kukiri kosa ‘Plea bargaining.’
Wakili Madeleka aliwasilisha maombi namba 80 ya mwaka 2021 kutokana na kesi aliyokuwa amefunguliwa ya uhujumu uchumi namba 40/2020.
Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi iliyotolea uamuzi Aprili 27 mwaka huu, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, wakili Madeleka alikuhukumiwa kulipa faini ya Sh200,000 au kutumikia kifungo cha nje cha miaka mitatu.
Katika uamuzi huo, pia alilipa Sh2 milioni kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) ili kuondolewa shauri hilo baada ya kulazimika kukiri makosa.
Hata hivyo wakili huyo alifungua kesi Mahakama Kuu, kupinga uamuzi wa Hakimu Mkazi Arusha, kumtia hatiani katika kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Wakili Madeleka pia aliiomba Mahakama Kuu itoe amri ya kurejeshewe faini ya Sh200,000 aliyolipa kwa sababu mchakato mzima ulikuwa ni kinyume cha sheria.
Amesema baada ya hukumu hiyo, alilazimishwa kufanya makubaliano ya kukiri kosa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) na baada ya kuachiwa alikata rufaa.
Leo mara baada ya kusomwa kwa hukumu yake na wakili huyo alibakia kwenye chumba cha mahakama hadi alipofika Wakili wake, Simon Mbwambo na wanahabari ndipo alipotoka kwenye chumba hicho na kukamatwa na polisi.
Awali Madeleka amesema kuwa Jaji Bade amekubaliana na hoja yake kuwa upande wa mashtaka kabla ya kuingia katika makubaliano ya kukiri makosa ulipaswa kuwa na ushahidi wa kosa alilotenda
“Hata hivyo, Jaji Bade ameagiza kesi hiyo kuanza upya kusikilizwa katokana na baadhi ya upungufu katika shauri hilo” amesema
Akizungumzia kuhusu kukamatwa kwa mteja wake, Wakili Simon Mbwambo, amesema hajui kosa analokabiliwa nalo wakili Madeleka.
"Sijui kosa naona polisi wamemkata na wanampeleka Ofisi ya RCO (Mkuu wa Upelelezi Mkoa Arusha) kwa mahojiano, labda wanataka kuanza upya kusikiliza kesi hii ya leo," amesema.
Polisi waliomkamata wakili Madeleka hata hivyo hawakuwa tayari kuelezea tuhuma zake na kuwataka wanahabari kufuata taratibu za kupata habari kwa kuzungumza na viongozi wa juu wa polisi.
Wakili Madeleka katika siku za karibuni amekuwa katika harakati za kupinga Makubaliano ya uwekezaji wa bandari kati ya Tanzania na Dubai na wiki iliyopita alikuwa jijini Dar es Salaam katika mkutano ulioandaliwa na Balozi mstaafu Dk Wilibroad Slaa na Wakili Boniface Mwabukusi wakielezea ubovu wa makubaliano hayo.