Wakazi 22,000 Butiama kunufaika na kituo cha afya cha Sh740 milioni
Kiongozi wa Kitaifa wa mbio za mwenge, Ismail Ussi akizungumza kabla ya kuweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa kituo cha afya cha Wegero wilayani Butiama. Picha na Beldina Nyakeke
Butiama. Zaidi ya wakazi 22,000 wa Kata ya Buswahili wilayani Butiama, Mkoa wa Mara wanatarajiwa kunufaika na mradi wa ujenzi wa kituo cha afya cha Wegero kinachotekelezwa kwa ushirikiano kati ya wananchi na Serikali Kuu.
Kituo hicho cha afya kimewekewa jiwe la msingi leo Jumatatu Agosti 18, 2025 na Kiongozi wa Kitaifa wa mbio za Mwenge wa Uhuru, Ismail Ussi, ikiwa ni sehemu ya mbio hizo ambazo leo zimeingia siku ya nne mkoani Mara, ambapo pia zinatarajiwa kuwasha Mwenge wa Mwitongo nyumbani kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Akitoa taarifa ya mradi huo, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Dk Nangi Nangi amesema ujenzi huo ulioanza Januari mwaka huu upo katika hatua ya asilimia 92 na unatarajiwa kugharimu zaidi ya Sh740 milioni.
“Baada ya kuibua mradi huu, wananchi walichangia zaidi ya Sh56.3 milioni na Serikali Kuu ikatoa zaidi ya Sh684.3 milioni. Kituo hiki kitahudumia vijiji vinne vya kata hii na kitasaidia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga,” amesema Dk Nangi.
Baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Wegero wamesema mradi huo utakuwa mkombozi mkubwa kwao kutokana na changamoto za upatikanaji wa huduma za afya.
Felister Magere amesema wamekuwa wakitumia gharama kubwa na muda mrefu kufuata huduma Kiagata, kilichopo umbali wa zaidi ya kilomita 20.
“Hapa pikipiki tunakodi kwa zaidi ya Sh20,000 kwenda Kiagata na tunatumia zaidi ya saa mbili kufika. Ukitembea ni zaidi ya saa sita kufika kule,” amesema.
Mary Wegoro amesema wananchi wamekuwa wakipoteza muda mwingi kutafuta huduma za afya hivyo kushindwa kushiriki ipasavyo kwenye shughuli za maendeleo.
Hata hivyo, Maswi Machela amesimulia mkasa wa kumpoteza mtoto baada ya mke wake kujifungulia njiani kwa kukosa usafiri wa haraka usiku.
“Mke wangu aliumwa uchungu usiku tukahangaika kupata usafiri kwenda Kiagata. Matokeo yake akajifungulia njiani, mtoto akafariki na yeye aliponea chupuchupu. Kituo hiki ni muhimu sana, tunataka kikamilike haraka,” amesema Machela.
Kwa upande wake, mkazi mwingine, Juma Waitaro alisema kata hiyo yenye vijiji vinne vya Wegero, Buswahili, Kongoto na Baranga ina zahanati mbili pekee, hali inayowalazimu wengine kutegemea maduka ya dawa.
Akizungumza kabla ya kuweka jiwe la msingi, Kiongozi wa Kitaifa wa mbio za mwenge, Ismail Ussi amesema mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa maono ya Serikali ya kusogeza huduma muhimu kwa wananchi.
“Nimeambiwa wakazi wa hapa mnalazimika kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya, jambo ambalo limehuzunisha sana. Lakini kwa kuwa mradi huu umekaribia kukamilika, sina mashaka kuwa sasa mtaanza kunufaika na huduma bora za afya,” amesema.
Amesema kituo hicho kitakuwa na huduma za uzazi salama, uzazi wa mpango na upasuaji wa dharura, na kitakuwa na ubora sawa na vituo vingine vinavyojengwa sehemu tofauti nchini.
“Serikali inatekeleza kwa vitendo dhamira yake ya kuboresha huduma za kijamii. Ubora wa kituo hiki ni sawa na ubora wa kituo kingine chochote iwe Dodoma au Dar es Salaam. Hii ina maana kuwa Serikali inatuthamini sote na kutoa huduma sawa kwa Watanzania wote,” amesema.