Musoma Vijijini yapokea Sh208 milioni mradi wa maji
Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka (mwenye fulana ya bluu), akikabidhiwa Mwenge wa Uhuru na Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Aswege Kaminyoge, kwa ajili ya kuanza mbio zake katika Halmashauri ya Musoma Vijijini. Picha na Beldina Nyakeke, Mwananchi.
Muktasari:
- Fedha hizo zimetolewa na serikali ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa uchimbaji wa visima 900 vya maji unaotekelezwa nchi nzima.
Musoma. Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Vijijini Mkoani Kara imepokea zaidi ya Sh208 milioni kwa ajili ya ujenzi wa vituo vitano vya kuchotea maji katika vijiji vinne mradi ambao ukikamilika unaelezwa utasaidia kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama katika vijiji hivyo.
Fedha hizo zimetolewa na Serikali ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa uchimbaji wa visima 900 vya maji unaotekelezwa nchi nzima.
Akitoa taarifa ya mradi huo leo Jumamosi Agosti 16,2025 kwa kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa, Meneja wa Wakala wa Maji safi Vijijini (Ruwasa) Wilaya ya Musoma, Edward Sironga amesema utekelezaji wa miradi hiyo umeanza tangu Januari mwaka huu na unatarajiwa kukamilika kabla ya mwisho wa mwaka huu.
Sironga amevitaja vijiji vitakavyonufaika na mradi huo wa ujenzi wa vituo vya kuchotea maji kuwa ni pamoja na Muhoji, Masinono, Kiriba na Bugwema.
Akizungumzia mradi huo katika Kijiji cha Muhoji, Sironga amesema mradi umefika asilimia 75 ya utekelezaji wake.
Amefafanua kuwa mradi huo ukikamilika utawanufaisha zaidi ya wakazi 1,200 wa kijiji hicho cha Muhoji pamoja na vijiji vya jirani.
"Faida za mradi huu ni pamoja na kupunguza muda mrefu waliokuwa wakitumia wakazi hawa kwenda kutafuta maji kwenye vijiji jirani," amesema.
Wakizungumzia mradi huo baadhi ya wakazi wa kijiji cha Muhoji wamesema kukamilika kwa mradi huo kutawaondolea adha waliyokuwa wakikutana nayo katika kutafuta maji kwaajili ya matumizi ya nyumbani.
Eliud Nyaubwa amesema wanawake kijijini hapo wanalazimika kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 10 kwenda na kurudi kufuata maji kwenye visima vya asili vilivyopo vijiji vya jirani.
"Wengine walikuwa wanalazimika kutumia maji ya kwenye madimbwi ambayo sio safi wala salama na hii ilikuwa ina hatarisha maisha yetu," amesema.
Lucia Munema amesema walikuwa wakilazimika kutumia maji pamoja na mifugo yao kutokana na kukosekana kwa maji safi na salama katika kijiji hicho hali ambayo pamoja na mambo mengine ilikuwa ikisababisha uwepo wa magonjwa ya mlipuko ikiwepo ugonjwa wa kuhara.
"Hapa kwetu tulikuwa tunasumbuliwa sana na magonjwa ya tumbo na yalikuwa yakisababishwa na matumizi ya maji yasiyokuwa salama naishukuru serikali kwa mradi huu sasa tumepona yale maradhi," amesema
Akizungumza baada ya kukagua mradi huo, Mkimbiza Mwenge kitaifa, Ismail Ussi amesema Serikali inalenga kuboresha huduma za kijamii ikiwepo huduma ya upatikanaji wa maji kwa wananchi wote wakiwepo waliopo maeneo ya vijijini.
Amesema ili kuhakikisha wakazi wa vijijini wanapata huduma ya maji safi na salama serikali iliamua kuanzisha wakala wa maji vijijini (Ruwasa) na kwamba hivi sasa miradi mingi inatekelezwa ili kufikia malengo hayo.
"Upatikanaji wa maji safi na salama mbali na kuondoa changamoto ya maji kwa wananchi lakini pia kunasababisha wananchi wapate muda mwingi wa kushiriki kwenye shughuli zao za maendeleo kwani maendeleo ya wananchi yanategemea ushiriki wao kikamilifu kwenye shughuli hizo," amesema.
Amesema kukosekana kwa maji kulikuwa kunasababisha wananchi wengi kutumia muda mwingi kutafuta maji na kushindwa kufanya shughuli zao za maendeleo.
Awali, akizungumza kwenye mapokezi ya mwenge huo leo, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka amesema mwenge huo unatarajia kuzindua, kukagua na kutembelea miradi minane yenye thamani ya zaidi ya Sh2.5 bilioni.
"Katika halmashauri ya wilaya ya Musoma vijijini mwenge utafikia miradi maendeleo ya vijana, elimu, afya, ustawi wa jamii na sekta nyingi na imegharimu zaidi ya Sh2.5 bilioni," amesema Chikoka.