Wadau wataja mbinu kumaliza kero ya maji

Muktasari:
- Wakati wataalamu wa uhandisi wa maji wakieleza matumizi ya Mto Rufiji, uchimbaji wa mabwawa na uvunaji wa mvua kuwa suluhisho la uhaba wa huduma hiyo, Chama cha ACT Wazalendo kimeishauri Serikali kukopa Sh10 trilioni kumaliza changamoto hiyo.
Dar es Salaam. Wakati wataalamu wa uhandisi wa maji wakieleza matumizi ya Mto Rufiji, uchimbaji wa mabwawa na uvunaji wa mvua kuwa suluhisho la uhaba wa huduma hiyo, Chama cha ACT Wazalendo kimeishauri Serikali kukopa Sh10 trilioni kumaliza changamoto hiyo.
Hatua hiyo inakuja wakati tayari Serikali ikitangaza kuwepo kwa mgawo wa maji katika baadhi ya mikoa kutokana na ukosefu wa mvua.
Jana Mwananchi ilimtafuta Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kwa simu kujibu changamoto za uhaba wa maji nchini, lakini alikata simu na kutuma ujumbe kwa mwandishi akisema “samahani nitumie message”, hata hivyo alipotumiwa ujumbe huo, hakujibu.
Vilevile, Naibu Waziri wa Maji, Maryprisca Mahundi alipatikana kwa njia ya simu lakini akajibu “siko kwenye nafasi ya kuzungumzia suala hilo.”
Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa alikata simu alipopigiwa na hakujibu ujumbe aliotumiwa.
Wanasiasa
Akizungumza na vyombo vya jana, msemaji wa sekta ya maji wa ACT Wazalendo, Esther Thomas alisema ni wakati sasa Serikali ikatafuta fedha hizo na kuzielekeza kwenye miradi ya maji nchi nzima ili wananchi wote wa mijini na vijijini wapate majisafi na salama.
Alisema mkopo huo wa muda mrefu utalipwa kwa makato ya tozo kwenye mafuta hadi utakapomalizika.
“Serikali ichukue mkopo nafuu wa muda mrefu wa Sh10 trilioni kutoka Benki za Maendeleo ili kutekeleza mradi mara moja na mapato ya fuel levy (tozo ya mafuta) yatahudumia mkopo huo mpaka utakapomalizika kulipwa,” alisema msemaji huyo.
Thomas alisema tatizo la maji nchini, siyo janga la asili, ni uzembe wa Serikali katika kumaliza changamoto hizo.
Alisema kuna miradi mingi iliyoanzishwa, lakini hadi sasa haijakamilika.
Aliutaja mradi wa maji wa Same - Mwanga - Korogwe wenye uwezo wa kuzalisha maji lita million 103.7 na wenye kipande cha tatu cha kusambaza maji katika mji wa Mwanga kinachogharimu Dola 36.70 milioni za Marekani (Sh84 bilioni).
Alitaja pia, kipande kingine cha nne cha ujenzi wa miundombinu ya kusambaza maji katika Mji wa Same kinachotekelezwa kwa thamani ya Dola 35.25 milioni za Marekani (Sh81.6 bilioni).
“Mradi huu utekelezaji wake ulianza mwaka 2014, miaka nane iliyopita hadi sasa haujakamilika,” alisema Thomas wakati akizungumza na vyombo vya habari.
Mradi mwingine alisema ni wa uboreshaji wa huduma ya majisafi na usafi wa mazingira katika Jiji la Mwanza na miji ya Magu, Misungwi na Lamadi kwa gharama ya Euro 104.5 milioni(Sh241.8 bilioni).
“Licha ya kuanza kwa mradi, baadhi ya maeneo bado watu wa Misungwi, Magu, Mkolani na Lamadi wanalia hawana majisafi yaliyo wafikia katika maeneo yao kama ilivyotarajiwa. Katika hili ni aibu kuona Jiji la Mwanza ambalo asilimia 53.2 ya eneo lake limezungukwa na maji baridi, watu wake hawana maji,” alisema Thomas.
Chama hicho kilipendekeza pia Serikali iharakishe kutafuta fedha kwa ajili ya kukamilisha mradi ya ujenzi wa Bwawa la Kidunda na mradi wa visima virefu 20 vya Mpera na Kimbiji vilivyopo Kigamboni.
Vilevile, kiliitaka Serikali kushughulikia tatizo la upotevu wa maji unaotokana na uchakavu wa miundombinu ya kusambaza maji.
Kwa upande wao, Chama cha Democratic (DP) kimeishauri Serikali kugeukia vyanzo vingine vya maji kama vile kuvuna maji ya mvua na kuchimba visima virefu hasa kwa maeneo kama Dar es Salaam ambako maji yako karibu.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdul Mluya alisema inashangaza kuona Serikali kuendelea kutegemea chanzo kimoja cha maji, miaka 60 tangu Tanzania ipate uhuru.
“Hii ni aibu, miaka 60 tunategemea chanzo kimoja cha Ruvu, Mkoa wa Dar es Salaam ni eneo tepetepe maji hayako mbali, Serikali inaweza kuchimba visima vya dharura maeneo mbalimbali vitakavyosaidia wakati kama huu,” alisema Mluya.
Aliongeza kuwa yapo maeneo kama ya Mto Msimbazi ambayo kipindi cha mvua inafurika, alisema maji hayo yanaweza kuvunwa na kuhifadhiwa kipindi cha masika, yakatumika wakati wa ukame.
“Yapo maeneo ya mabondeni, teknolojia inaweza kutumika kuvuna maji ya mvua, lakini kwa mikoa ya kanda ya Ziwa, kunaweza kufanyika uboreshaji, maji ya Ziwa Victoria yakawa sehemu ya utatuzi wa kero ya upatikanaji wa maji,” alisema.
Wataalamu washauri
Akizungumza kwa simu jana na Mwananchi, Vitalis Kitime kutoka Kampuni KTM Investment Ltd ya Dar es Salaam, alishauri kutotegemea moja kwa moja Mto Ruvu, kwa kuwa hautoshelezi mahitaji yaliyopo.
“Viongozi wa Serikali wanasema sababu ya uhaba wa maji mvua ni chache. Ni sawa, lakini miaka yote 60 ya uhuru bado tunategemea tu mvua?” alihoji Kitime.
Alisema zipo juhudi zinazoweza kufanyika, ikiwa pamoja na kujenga visima na mabwawa ya akiba kwa ajili ya Dar es Salaam maalumu kwa ajili ya wakati wa shida.
“Tanzania ina maziwa na mito mingapi? Leo ukizunguka kwenye mikoa yenye maziwa kama Kigoma, Geita, Mwanza, Kagera na kwingineko, kuna vijiji havina maji na ziwa liko pale,” alisema.
Kitime, ambaye ni mtaalamu wa uhandisi wa maji, alisema inawezekana kutumia teknolojia rahisi kusukuma maji kutoka kwenye vyanzo, hasa mito na maziwa na kusambaza kwenye miji na vijiji.
“Mfano nimesanifu floating intake (mtambo unaoelea), ambayo tunatoa maji bwawa la mto Mtera na tangi limejengwa pembeni maji yanaingia na yanahudumia watu wa eneo lile.
“Ifike mahali, tutumie hizi teknolojia kuhudumia maeneo yenye mito na maziwa yasiyo na huduma ya maji,” alisema.
Kwa Dar es Salaam, alisema suluhisho la haraka ni kutoa maji Mto Rufiji na uchimbaji wa visima.
Maoni hayo yameungwa mkono na Rashid Abdallah, ambaye pia ni mtaalamu wa maji aliyeshauri kuwepo na mikakati ya uvunaji na uhifadhi wa maji ya mvua.
“Kama tukiwekeza kwenye uvunaji wa maji itasaidia sana.
“Pia tunahitaji kutumia mito iliyopo karibu, hasa Rufiji kuliko kutumia Mto Ruvu pekee na kufanya utafiti wa kina kuhusu maji ya chini ya ardhi, hata kama ni nje ya Dar es Saaam litasaidia,” alisema.
Suala la kutumia maji ya Mto Rufiji pia limeshauriwa na Dk Lawi Yohana kutoka Chuo Kikuu Huria Tanzania, akisema japo itagharimu fedha nyingi, ndiyo suluhisho la kudumu.
“Tumekuwa na uhaba wa maji kwa sababu ya kutegemea tu chanzo kimoja cha mto Ruvu, suluhisho ni kuchukua maji ya mto Rufiji.
“Inawezekana isiwe leo wala kesho kwa sababu ya bajeti na muda, lakini pia kuna mikakati ya haraka nayo ni kuchimba visima na kuhifadhi maji,” alisema.