Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Maumivu ya kusaka maji yanavyoathiri familia

Mkazi wa Kisaarawe, Jirani Athumani akisaidia kubeba maji katika kisima kilichopo kijiji cha Kisopwa, kwa ajili ya matumizi ya nyumbani. Picha na Nasra Abdallah

Muktasari:

  • Wakati baadhi ya wakazi wa miji mikubwa, likiwamo Jiji la Dar es Salaam hawaamini kama wanaweza kukosa huduma ya maji kwa zaidi ya wiki, kwingineko wapo wanaoitafuta huduma kwa miaka nenda rudi.

Kisarawe. Wakati baadhi ya wakazi wa miji mikubwa, likiwamo Jiji la Dar es Salaam hawaamini kama wanaweza kukosa huduma ya maji kwa zaidi ya wiki, kwingineko wapo wanaoitafuta huduma kwa miaka nenda rudi.

Kwa mfano, ni miaka 18 sasa, kijiji cha Kisopwa kilichopo Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani hawana huduma ya maji, hali inayowafanya wakazi wa eneo hilo kuamka saa nane za usiku kusaka huduma hiyo.

Hali hiyo imeiathiri moja kwa moja familia ya Juma Said, ambaye sasa ameachana na mkewe Mwanjala Kimoko kutokana na ugomvi uliotokana na shida ya maji.

Akielezea mkasa huo, Mwanjala, aliyeoana na mumewe miaka saba iliyopita, anasema ni kama mwezi umepita tangu walipotengana na mume wake na sababu ilikuwa kuchelewa kurudi kuteka maji.

Mwanjala anasema hiyo siku anakumbuka alirudi nyumba saa 11 kasoro asubuhi, tena akiwa hoi na uchovu wa kusubiria maji tangu saa sita usiku na ndoo yake ya maji kichwani.

“Pamoja na kuchoka huko, mume wangu bila ya huruma alitoka nje akaanza kugomba na hatimaye akanifukuza na kuniambia nirudi nilipotoka bila huruma.

“Hata pale nilipomuelewesha kuwa nilikuwa katika kusaka maji, alizidi kupandisha hasira zake na kuniambia hataki kuniona machoni mwake.

Mwanjala ambaye ni mama wa watoto wanne, anasema kwa kuwa bado kulikuwa na giza, aliomba hifadhi jikoni kwa jirani yake akalala hapo mpaka kukakucha na kisha akaenda kwa wazazi kuwaeleza jambo hilo.

Baada ya kutoa taarifa hiyo anasema mama yake alipokwenda kumuuliza mume wake huyo kulikoni, aliambulia matusi.

“Nililala kwa muda wa kama siku nne katika jiko la jirani na baadaye kilipatikana chumba ambacho ni nyumba ya mtu haijaisha na kuipaua ili nipate kujihifadhi na watoto kwa kuwa bado ni wadogo nisingeweza kuwaacha wenyewe,” anasema Mwanjala.

Mume wa Mwanjala, alikiri kumfukuza mke wake na kueleza kuwa licha ya kutambua kuwepo kwa changamoto ya maji katika eneo lao, ukweli ni kwamba wakati mwingine wivu humuingia.

“Ni kweli tuna changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji, hivyo wanawake zetu wanavyokaa zaidi ya saa tano kisimani, wakati mwingine imani zinatutoka wanaume, kwani nasi tuna roho jamani,” anasema.

Hata hivyo, Said alisema baada ya kumfukuza mwanamke huyo, ndipo alipogundua kwamba ni kweli maji hayo wanayapata kwa shida kwa kuwa naye ilibidi kuanza kuamka saa sita za usiku kwenda kuweka foleni.

Alisema hali hiyo ilimuathiri hata katika kwenda kutafuta kipato, kwa kuwa sasa ilibidi kwanza apate uhakika kuwa ana maji ya kutumia atakaporudi ndio aondoke.

“Nilijionea hali mwenyewe, ndio yakanifanya nirudishe moyo nyuma na kumrudia mke wangu kama siku tatu zilizopita. Pia ilichangiwa na vikao na wazazi wa pande zote mbili kukaa na kutuelewesha.

“Lakini kama na mimi nisingejionea kwa macho haya aliyekuwa anapitia mke wangu huenda tusingerudiana naye maisha,” anasema Said.

Alipoulizwa ni kwa nini hamsindikizi mkewe kwenye maji, alisema ni kutokana na utafutaji wa maisha ambapo yeye kutwa nzima anakuwa kazini akibeba matofali, anaporudi nyumbani ni usiku mwingi anakuwa amechoka huku akitakiwa kuondoka asubuhi sana.

Aliiomba Serikali kuwatafutia ufumbuzi wa tatizo hilo na kueleza kuwa kwa yeye alivumilia kumfukuza mke wake hata bila kumkata kibao, lakini kwa wengine wanaweza kuchukua maamuzi mengine hata ya kuuana kutokana na wivu katika mapenzi.

“Viongozi wetu waelewe tu kwamba changamoto ya maji inaleta madhara makubwa kwetu, ikiwemo kuvunjika kwa ndoa na kukosekana kwa amani.

“Pia suala zima la usalama wa watoto wetu ambao wakati mwingine wanaachwa wenyewe nyumbani na mama zao wanapokwenda kusaka huduma hiyo na kama hivyo kwa sasa dunia ilivyoharibika kuna vitendo vya ulawiti na ubakaji kwa watoto wetu, Serikali itusaidie katika hili,” amesema.

Said anasema kwa sasa ili kupata maji safi yasiyo na chumvi inawalazimu kutumia Sh1,500, maji ambayo wanayapata Maramba Mawili Mbezi, ambayo kwa miasha yao hawayamudu, wakati yale ya kisima yanayochimbwa na baadhi ya watu anasema yana chumvi ambayo hayafai hata kupikia chai na kwao bora kutumia hayo ya kisima.



Wananchi wafunguka

Hali hiyo ya shida ya maji inaelezwa na wakazi wa eneo hilo, akiwemo Mwajuma Hussein, ambaye anasema kwa wao wenye watoto wadogo, inabidi waende nao kisimani usiku kwa kuwa hawana watu wa kuwaachia, jambo ambalo sio zuri kwa afya zao.

Ukiachilia hilo, pia huwashindisha na njaa kwa muda mrefu, kwa kuwa mpaka watoke huko kisimani ndio wakawakorogee uji, huku akionyesha kuhofia kuweza kupata maradhi ya utapiamlo.

Sada Habibu anasema hali hiyo ni ngumu, kwani wanaume zao wamekuwa wakiwahisi wanaenda kwenye mchepuko, lakini ukweli ni kwamba muda mwingi wanautumia katika kusaka maji.

Kauli hiyo iliungwa mkono na Alice Mhando, aliyesema maji yamekuwa kero kubwa kwao, kwani kutokana na uchafu wake wanawake wamekuwa hawaishi kupata maambukizi katika njia ya mkojo (UTI).

Jirani Athumani, anasema maji hayo wanayotumia ni hatari hata kumpa ng’ombe, lakini leo wao ndio wanayatumia binadamu kupika, kunywa na kuoga na kuiomba Serikali iwajali katika hilo.

Asha Seleman, anasema tabu nyingine wanaipata kwa watoto wao ni mashati yao ya shule, kwani ndani ya wiki moja tu yanakuwa yamebadilika rangi kuwa kama chai ya maziwa.

“Shati zinafubaa ndani ya muda mfupi na sisi hatuna uwezo huo wa kununua sare za shule kila siku. Kwa hiyo tunaomba tusaidiwe maji jamani, maji hatuna,” anasema Asha.

Naye Rahim Lyema, aliyehamia huko tangu mwaka 2010, anasema maji mengi wanayoyatumia ni ya kuchimba mashimo ambayo ni machache ukilinganisha na idadi ya watu waliomo humo.

Lyema anasema anachoona suala la maji katika eneo hilo linawezekana, kwani maji hayako mbali, kwa kuwa kuna kisima kipo Pugu na kingine kipo Kisarawe ambapo ni kilomita chache kufika hapo walipo, na kueleza kuwa ni kiasi cha viongozi kulipa suala hilo kipaumbele.

Akizungumzia changamoto hiyo, Diwani wa Kiluvya kilipo kitongoji hicho, Aidan Kitale anasema taarifa aliyonayo ni kwamba kuanzia Januari mwakani ujenzi wa miundombinu ya maji utaanza na kuwaomba wananchi kuwa na subira katika hilo.


Dawasa

Akizungumzia kero hiyo, Mkurugenzi Mawasiliano wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa), kupitia msemaji wake Nelly Msuya alisema eneo hilo lipo katika mradi wa usambazaji wa miundombinu ya maji maeneo ya Gongo la Mboto, Pugu na Majohe, ambapo mradi mzima unatarajiwa kukamilika na kukabidhiwa ifikapo Februari mwakani.

“Niwaombe tu wananchi wa Kisopwa wavute subira,” anasema Nelly. Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kisopwa, Penmaen Samson, anasema wiki moja iliyopita watu wa Dawasa walipita kupima wakiwa na mkandarasi, hivyo hayo ni matumaini tosha kuwa maji yatafika.

Amesema wamekuwa kwenye adha hiyo kwa muda mrefu, licha ya kuwapo bomba la maji kutoka Ruvu yanayoenda kwenye visima vya Kisarawe.