Prime
Wadau wamtwisha zigo Rais Samia akikutana na vigogo Polisi

Rais Samia Suluhu Hassan
Muktasari:
- Kesho Jumanne, Amri Jeshi Mkuu wa Tanzania, Rais Samia Suluhu Hassan atakuwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya Jeshi la Polisi. Wadau waliozungumza na Mwananchi wameeleza matamanio yao wanayotarajia kusikia akiyasema mbele ya askari hao.
Moshi. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu kesho Jumanne, Septemba 17, 2024 anakutana na maofisa wa juu wa Jeshi la Polisi, huku wanasheria, wanaharakati, viongozi wa dini na wananchi wakitamani atoe kauli thabiti juu ya masuala 10 muhimu yakiwamo matukio ya utekaji na mauaji.
Masuala hayo yanahusiana na utekaji watu, kupotea kwa watu, kuteswa, mauaji, ubambikiaji kesi, rushwa ndani ya Jeshi la Polisi, matumizi ya nguvu kupita kiasi, uundwaji Tume ya Kijaji, haki za raia, uchaguzi na nani wanahusika na utekaji.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Tanzania (LHRC), kimetamani Rais azungumzie na kukemea matukio ya utekaji, kupotea kwa watu na mauaji ambayo yanakiuka Katiba, Sheria na mikataba ya kimataifa.
Mkazi wa Njoro katika Manispaa ya Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro, Emiliana Johnson, amesema anamatani maofisa hao wamweleze Rais uchunguzi wao wa awali wa matukio ya utekaji, kupotea kwa watu na mauaji ni genge gani linafanya uhalifu huo.
“Lakini si hivyo tu, ninatamani waeleze mbele ya Rais je ile orodha ya watu 83 iliyotolewa na TLS (Chama cha Wanasheria Tanganyika) ina ukweli au uongo na kama ina uongo kwa nini hatujasikia hao TLS wamehojiwa kwa uchochezi,” amesema.
Rais anakutana na maofisa hao wakati atakapokuwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya Jeshi la Polisi, katika Shule ya Polisi Tanzania mjini Moshi, ambayo zamani ilijulikana kama Chuo cha Polisi Moshi au kwa kifupo CCP.
Katika kipindi cha saa 24 hadi kufikia leo mchana, ukurasa wa X (Twitter) wa Jeshi la Polisi, umesheheni matangazo ya kuhamasisha tukio hilo litakaloanza saa 2:00 asubuhi.
Itakumbukwa Rais anakutana nao akiwamo Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Camilius Wambura na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Ramadhan Kingai, ikiwa ni siku 10 tangu aagize uchunguzi wa mauaji ya aliyekuwa kada wa Chadema, Ali Kibao.
Septemba 8, 2024 kupitia ukurasa wake wa X, Rais Samia alionyesha masikitiko yake makubwa baada ya kupokea taarifa za mauaji ya Kibao aliyekuwa mjumbe wa Sekretarieti ya Chadema.
Kibao alitekwa na genge la watu wenye silaha Ijumaa ya Septemba 6,2024 eneo la Kibo Complex Tegeta, jijini Dar es Salaam, ambao walimshusha kwenye basi la Tashriff na siku iliyofuata mwili wake ulipatikana akiwa ameuawa eneo la Ununio, Dar es Salaam.
Kupitia ujumbe wake huo, Rais Samia aliviagiza vyombo vya uchunguzi kumpelekea taarifa ya kina kuhusu tukio hilo aliloliita ‘baya kabisa’ na mengine ya namna hiyo akisisitiza taarifa hiyo ya uchunguzi ifikishwe kwake haraka.
“Nchi yetu ni ya kidemokrasia na kila raia ana haki ya kuishi. Serikali ninayoiongoza haivumilii vitendo vya kikatili vya namna hii,” alisisitiza Rais, kauli ambayo bado ilipokelewa kwa hisia tofauti na umma, wakitaka uwajibikaji wenye dhamana.
Tukio hilo sio tu limelaaniwa na viongozi na wanachama wa Chadema, lakini pia limelaaniwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), viongozi wa dini, mabalozi zaidi ya 15 wanaowakilisha mataifa yao Tanzania, wanaharakati na wananchi, wakitaka hatua za haraka zichukuliwe dhidi ya waliohusika.
Kauli ya LHRC
Wakizungumza na Mwananchi, Mkurugenzi Mtendaji LHRC, Dk Anna Henga amesema angependa Rais Samia awaeleze maofisa wa Polisi umuhimu wa kulinda haki za bindamu na kuheshimu sheria katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
“Polisi wanapaswa kuhakikisha wanatekeleza majukumu kwa kuzingatia sheria bila kuvunja haki za msingi kama vile uhuru wa kujieleza na haki ya kukusanyika kwa amani.
“Matukio ya utekaji na kupotea kwa watu yameathiri haki za binadamu nchini na Polisi wana nafasi kubwa ya kuyazuia. Rais anapaswa kusisitiza Polisi kushirikiana na taasisi nyingine kuhakikisha vitendo vya aina hiyo vinakomeshwa,” amesema Henga.
Mkurugenzi huyo amesema: “Polisi wakichukua hatua stahiki, wanaweza kudhibiti na kuzuia matukio haya. Lakini kuelekea uchaguzi mkuu, Polisi wanapaswa kujiepusha kuwa na upande wowote wa kisiasa ili kulinda usalama wa raia bila upendeleo.”
“Rais awahimize viongozi wa Polisi kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa haki na salama kwa kutoa ulinzi kwa pande zote. Mafunzo ya haki za binadamu kwa Polisi ni muhimu ili wahakikishe wanatimiza wajibu wao kwa ufanisi na weledi,” amesema.
Mkurugenzi wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Bob Wangwe ambaye ni mwanasheria, amesema: “Matamanio yangu ni kumsikia Rais akiwasihi askari Polisi kuondokana na vitendo vibaya kama utekaji, mauaji, kubambikia watu kesi.
“Rushwa, matumizi ya nguvu kupita kiasi, kutofuata sheria ambavyo vimebainishwa na Ripoti ya Haki Jinai na malalamiko ya wananchi. Jeshi la Polisi linapaswa kujifananisha na mke wa Kaisali ambalo halipaswi hata kutuhumiwa.”
Matarajio ya wananchi
Mkazi wa Njoro katika Manispaa ya Moshi, Emiliana Johnson, amesema anamatani maofisa hao wamweleze Rais uchunguzi wao wa awali wa matukio ya utekaji, kupotea kwa watu na mauaji ni genge gani linafanya uhalifu huo.
“Lakini si hivyo tu, ninatamani waeleze mbele ya Rais je ile orodha ya watu 83 iliyotolewa na TLS (Chama cha Mawakili Tanganyika) ina ukweli au uongo na kama ina uongo, kwanini hatujasikia hao TLS wamehojiwa kwa uchochezi,” amesema.
Mwananchi huyo alikwenda mbali na kueleza kuwa anatamani kusikia uchunguzi wa awali wa Polisi unaonyesha ni nani waliomteka na kumuua mzee Kibao na nani wanawashikilia Deusdedith Soka na wenzake na wengine ambao wamepotea.
Ally Ramadhan, mkazi wa Shabaha Wilaya ya Moshi, amesema anatamani kumsikia Rais akitumia kofia yake ya kuwa mfariji mkuu, kuwatuliza wananchi na taharuki waliyonayo kutokana na watu kutekwa, kupotea na wengine kutoonekana.
Viongozi wa dini
Akizungumza na Mwananchi, Askofu mstaafu wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Stephen Munga, amesema roho ya mtu mmoja ikipotea, inaleta mahangaiko kwa wapenda amani.
“Tunatamani kesho (Rais atuthibitishie kwamba pamoja na matukio haya ya utekaji, watu kupotezwa na mauaji, ana mkakati dhabiti wa kuyakomesha haya na waliohusika wanatafutwa, kupatikana na kushtakiwa mahakamani.
“Hapo (CCP) ni mahali pake haswa. Tutaumia tusipomsikia akituthibitishia hili roho za watu zitulie maana uhai wa mtu mmoja tu ukipotea tunaumia na kupata mahangaiko kwa sababu roho ya mtu mmoja ina thamani sawa na wengi,” amesema.
Askofu mstaafu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) Kilimanjaro, ambaye sasa ni Mchungaji kiongozi wa Kilimanjaro International Christian Centre (KICC), Dk Glorious Shoo, amesema anatamani Rais awaambie wasimamie haki.
“Yaani natamani awaambie simamieni haki na alirudie hilo neno hata mara 100. Kwa sababu nchi inapita kipindi kigumu. Ubambikiaji kesi, utekaji, watu kupotea, mauaji na hili la utekaji limepigiwa kelele duniani kote na kila mtu,” amesema.
Mchungaji Shoo amesema suala la ukiukwaji wa haki za binadamu za kiraia lisiposhughulikiwa vizuri linaweza kuathiri sifa nzuri ya Tanzania kimataifa na kuathiri imani ya wawekezaji na kuiona Tanzania kama nchi ambayo si salama.