Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chadema, ACT-Wazalendo waibana Serikali

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe (kushoto) na Makamu Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo (Bara), Isihaka Mchinjita.

Muktasari:

  • Chadema imeipa Serikali muda wa siku 10 hadi Septemba 21 kueleza walipo waliotekwa, vinginevyo wataandamana.



Dar es Salaam. Vyama vya Chadema na ACT- Wazalendo vimeibana Serikali, vikitaka hatua kuchukuliwa kushughulikia na kukomesha vitendo vya utekaji au watu kupotea katika mazingira ya kutatanisha.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema iwapo hakuna hatua zitakazochukuliwa dhidi ya wakuu wa taasisi zinazosimamia ulinzi na usalama wa raia, wafuasi na wanachama wa chama hicho watainga barabarani kuanzia Septemba 23, 2024 kudai haki za watu wao waliopotezwa.

Mbowe amesema hayo leo Jumatano Septemba 11, 2024 jijini Dar es Salaam alipohutubia viongozi wa chama hicho wa Dar es Salaam na Pwani, juu ya maazimio ya vikao vilivyofanyika leo.

Amesema katika vikao hivyo wamekubaliana kuipa Serikali muda hadi Septemba 21, ieleze walipo wanachama wake waliopotea au iwakabidhi wakiwa wafu.

Amesema hadi siku hiyo Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Camilius Wambura na Mkurugenzi wa Idara wa Usalama wa Taifa wawe wamewajibika kwa kujiuzulu.

Amewataka viongozi wa Chadema mikoa yote nchini kwa siku 12 kuanzia leo Septemba 11, waanze kujipanga kwa safari ya Dar es Salaam.

“Tutakutana Dar kwa utaratibu ambao tutapeana,” amesema Mbowe.


Maazimio ya vikao

Mbowe amesema vikao vimeazimia kuitisha kikao cha Kamati Kuu maalumu Septemba 16 na 17, 2024 kujadili suala la utekaji, mauaji na kupotea kwa viongozi.

“Dhamira ni kuhakikisha yote yanayoamuliwa katika kikao hicho yapate uhalali wa kikatiba, kanuni na kiutendaji,” amesema.

“Tunatambua uwepo wa Watanzania wengi waliotekwa na vikao vimesema lazima jambo hili lifike mwisho. Kwa sababu wao wamekataa kufika mwisho, sisi tutawalazimisha walifikishe mwisho,” amesema.


Tume ya kimataifa

Katika mkutano huo, Mbowe amesema badala ya kuundwa kwa tume ya kijaji, hitaji lao ni taasisi za kimataifa ndizo zichunguze matukio ya utekaji na mauaji nchini.

Uamuzi huo, unatokana na kile alichoeleza, hawana imani kuwa tume ya kijaji katika mazingira yaliyopo, inaweza kuleta matokeo wanayotarajia.

Awali, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu amesema mkutano huo, unahusisha kuelezana mambo magumu.

“Ni wakati sasa wa kuelezana mambo magumu kwa sababu tunapelekwa mahali ambapo tusipofanya maamuzi magumu kuhusu hali yetu kama chama kama wanachama na kama wananchi mambo yetu yatakuwa mabaya sana,” amesema.


Kauli ya ACT

Kwa upande wake, Chama cha ACT- Wazalendo, kimetaja hatua nne zinazopaswa kuchukuliwa na Serikali, ikiwemo kushughulikia mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai kuhusu utendaji kazi wa polisi, ili kukomesha vitendo vya utekaji au watu kupotea katika mazingira ya kutatanisha.

Mbali na hilo, imemtaka Rais Samia Suluhu Hassan kuwafuta kazi Masauni na IGP Wambura, ikidai wameshindwa kutimiza majukumu yao ya kusimamia usalama wa raia.

Kauli hiyo imetolewa na Makamu Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo (Bara), Isihaka Mchinjita alipohutubia mkutano wa hadhara, eneo la  Mbagala Kizuiani wilayani Temeke, ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara yake ya siku 10 katika mikoa ya Dar es Salaam na Morogoro.

Viongozi wa chama hicho wameanza ziara ya awamu pili ya siku 21 kutembelea mikoa 22 kuimarisha chama hicho.

Mchinjita amesema hatua nyingine ni Serikali kuupeleka upya bungeni Muswada wa Sheria ya Usalama wa Taifa ya mwaka 2023, ili kufanyiwa marekebisho baadhi ya vipengele akidai si rafiki.

"Tanzania ina historia ya kuwa na amani na utulivu, lakini sasa hivi inaingia doa kutokana na vitendo vya utekaji, hivyo Rais Samia ana wajibu wa kukomesha vitendo hivi kwa kuyafanyia kazi mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai, ili kurejesha imani ya wananchi kwa Jeshi la Polisi.

"Hatupaswi kuendelea na hali hii, maisha ya Watanzania yamejawa hofu na mashaka kiasi kwamba ndugu yako akiondoka ghafla hujui kama atarudi au la? Tumtake Masauni ajiuzulu mwenyewe, akishindwa Rais Samia amfute kazi kwa kushindwa kusimamia usalama wa wananchi," amesema.

Pia ametaka Rais Samia kumfuta kazi IGP Wambura kutokana na vitendo vya utekaji, likiwemo tukio la mjumbe wa sekretarieti ya Chadema, Ali Kibao aliyetekwa Septemba 6, 2024 maaneo ya Tegeta Kibo Complex kwa kushushwa kwenye basi alipokuwa akielekea mkoani Tanga na Septemba 7, mwili wake kukutwa Ununio akiwa ameuawa.

Mchinjita amesema tukio la Kibao halileti taswira nzuri ndani ya Taifa, akisisitiza linazidisha hofu na mashaka kwa Watanzania wakiwemo wakosoaji ambao hawajui kesho yao itakuaje.

Akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika Kibaha mkoani Pwani, Kiongozi wa ACT- Wazalendo, Dorothy Semu amesema, "hali ya utekaji inaleta hofu na kuzua maswali kwa jamii, ingawa Rais Samia ameagiza uchunguzi ufanyike.

"Sisi wanasiasa tunahitaji majibu, Rais Samia alete majibu ya uchunguzi kwa sababu Watanzania wanastahili kuishi bila hofu."