Wadau wa demokrasia wataka tume huru, mgombea binafsi

Muktasari:
- Kikao cha wadau kuhusu hali ya demokrasia nchini kimeazimia mabadiliko madogo ya Katiba badala ya kuifumua yote.
Dar es Salaam. Wadau wa demokrasia kupitia Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), wapendekeza kufanyika kwa mabadiliko madogo kwenye Katiba iliyopo sasa kabla ya mchakato wa Katiba mpya kuendelea.
Mapendekezo hayo, kwa mujibu wa Mwenyekiti TCD, Profesa Ibrahim Lipumba, ni kutokana na kukaribia kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024 na Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Profesa Lipumba ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam leo, Jumatano Agosti 23, 2023 akitoa maazimio ya mkutano huo ulioandaliwa na TCD.
"Mkutano ulipendekeza kufanyika mabadiliko muhimu katika Katiba iliyopo sasa ili kupanua uwepo wa demokrasia na kupatikana tume huru ya uchaguzi kuelekea uchaguzi wa 2024 na 2025," amesema.
Katika maazimio hayo, amesema washiriki wameona kusubiri Katiba Mpya ipatikane kabla ya chaguzi zijazo ni sawa na kujidanganya.
"Mkutano ulipendekeza kufanyika mabadiliko muhimu katika Katiba iliyopo sasa ili kupanua uwepo wa demokrasia na kupatikana tume huru ya uchaguzi kuelekea uchaguzi wa 2024 na 2025," amesema.
Mbali na tume huru ya uchanguzi, Profesa Lipumba ametaja mabadiliko mengine kuwa ni uwepo wa mgombea binafsi ili kuwapa mwanya wasio na vyama kushirikia kama wagombea lakini pia wanataka uchaguzi wa Rais kuhojiwa mahakamani endapo kutakuwa na tatizo.
Kingine amesema Rais atangazwe mshindi endapo akipata asilimia 50 ya kura ambapo kwa sasa ni asilimia 15 tu zinazompa ushindi Rais.
Maazimio mengine ameyataja ni mabadiliko ya sheria ya utumishi wa umma ili kuruhusu wagombea ambao ni watumishi wa umma wa wawe na fursa ya kurejea kwenye nafasi zao iwapo watashindwa uchaguzi.
"Hili linawakwaza wengi hasa wanawake ambao wengi ni watumishi wanaogopa kwenda kugombea wakikosa watakuwa wamepoteza ushindi na kazi," amesema.
Kingine walichoazimia ni kuondolewa kwa gharama za uchukuaji na urudishaji fomu za kugombea uchaguzi.
"Nakumbuka kwenye urais, inahitajika ukirudisha fomu upeleke na Sh1 milioni, sasa kuna watu wanataka kugombea urais, lakini hawana hiyo hela.
"Unaweza kuwa huna Sh1 milioni lakini una mawazo mazuri ya kuwaletea Watanzania, kwa hiyo kiondolewe kikwazo hicho," amesema.