Profesa Lipumba alia na ucheleweshwaji tume huru ya uchaguzi

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi CUF, Ibrahim Lipumba akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Jumatatu Novemba 28, 2022.Picha na Michael Matemanga
Muktasari:
Profesa Lipumba amesema amejawa na wasiwasi kuona hata maazimio waliyokubalina kwenye mkutano wa wadau wa demokrasia uliofanyika jijini Dodoma Desemba, 2021 kama yatafanyiwa kazi.
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amesema kupata tume huru ya uchaguzi imekuwa ni kitendawili licha ya jitihada za maridhiano zianzofanyika.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 28, 2022 jijini hapa, Profesa Lipumba amesema amejawa na wasiwasi kuona hata maazimio waliyokubalina kwenye mkutano wa wadau wa demokrasia uliofanyika jijini Dodoma Desemba, 2021 kama yatafanyiwa kazi.
"Nina wasiwasi mkubwa kwani sioni maandalizi ya kupata tume turu.
“Pamoja na dhamira ya Rais Samia (Suluhu Hassan) na falsafa yake ya 4R yaani ‘Reconciliation, Resilience, Reforms and Rebuilding (Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Kujenga upya).
Akikumbusha maazimio waliyokubaliana katika mkutano wa wadau wa demokrasia ya vyama vya siasa jijini Dodoma, amesema suala la kupatikana kwa tume huru ya uchaguzi lilijadiliwa.
“Tume huru isimamie chaguzi zote zikiwemo za serikali za mitaa," amesema.
Amesema ni muhimu tume huru ya uchaguzi ipatikane kwa haraka ili iwe na muda wa kuandaa uchaguzi huru na wa haki wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025.