Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Viongozi wa dini wasisitiza Tume huru ya uchaguzi

Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Bakwata, Sheikh Hamis Mataka

Muktasari:

Viongozi wa dini wamesisitiza umuhimu wa kuwa na Tume huru ya uchaguzi wakati wakitoa mapendekezo yao mbele ya Kikosi Kazi cha kuratibu maoni ya wadau wa demokrasia, ikiwa ni sehemu ya maeneo tisa yaliyochambuliwa na kikosi hicho.

Dar es Salaam. Viongozi wa dini wamesisitiza umuhimu wa kuwa na Tume huru ya uchaguzi wakati wakitoa mapendekezo yao mbele ya Kikosi Kazi cha kuratibu maoni ya wadau wa demokrasia, ikiwa ni sehemu ya maeneo tisa yaliyochambuliwa na kikosi hicho.

Mchakato wa kukusanya maoni kutoka kwa wadau na taasisi mbalimbali jana uliingia siku ya pili ambapo uwakilishi wa Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata), Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC) na Kanisa la Waadventisa Wasabato Tanzania, walitoa mapendekezo katika maeneo hayo.

Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Bakwata, Sheikh Hamis Mataka alisema wamependekeza kuwepo kwa Tume huru ya uchaguzi itakayolindwa kisheria na kutekeleza majukumu yake bila kuwa na hofu. Pia alisema tume hiyo itatoa uamuzi wake kwa haki na uadilifu kuwa inalindwa kisheria.

“Tunapendekeza kuwepo kwa Tume huru ya uchaguzi itakayokubalika na kuridhiwa, maana yake itakuwa shirikishi hata watu na wanajamii wakiwaona wajumbe wake hawatakuwa na mashaka nao,” alisema Mataka.

Kuhusu ushirikishwaji wa umma katika suala la Bunge, Mataka alisema Bakwata imependekeza kuwepo kwa viti maalumu vitakavyotolewa kwa vyama vyote vya siasa vitakavyoshiriki uchaguzi mkuu.

“Pia tunapendekeza kuwepo kwa mkutano wa maridhiano wa vyama vyote baada ya kumalizika uchaguzi mkuu utakaosimamiwa na viongozi wa dini. Lengo ni kuponya majeraha yaliyotokana na uchaguzi mkuu. Pia mikutano ya hadhara ni muhimu kwa sababu vyama vya siasa vinapata fursa ya kujitangaza.

Kwa upande wake, Camillius Kassala ambaye ni mkurugenzi wa Uadilifu na Binadamu wa TEC alisema wamependekeza kuwepo kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambayo watendaji na viongozi wake wataongozwa kwa kusimamia ukweli na uadilifu katika utendaji wao.

“TEC inapendekeza kuwepo kwa uwakilishi wa viongozi wa dini katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Kwa sababu viongozi wa dini wanatufundisha maadili na kusema ukweli ni mojawapo nguzo ya maadili. Ukweli ndio utakaofanya tume ya uchaguzi kuwa huru,” alisema Kassara.

Mbali na hilo, TEC ilipendekeza kuwepo chuo cha uongozi kitakachofundisha masomo ya uraia na siasa, ili wanasiasa wanaojiunga na vyama vya siasa wajengewa uelewa kuhusu tasnia hiyo, badala ya kuingia na kutafuta masilahi.

“Ndio maana hadi leo baadhi yao wanatafuta masilahi badala ya itikadi na falsafa za chama husika, jambo linalosababisha matatizo na hama hama ya wanasiasa,” alisema Kassala.

Naye Askofu Mkuu, Jimbo Kuu la Kusini mwa Tanzania Kanisa la Waadventista Wasabato Tanzania, Mark Malekana alizungumzia suala la Katiba, akisema, “Katiba ipo ndio maana Taifa linaongozwa ila kinachotakiwa ni kufanyiwa maboresho na marekebisho.

“Wanaosema Katiba mpya wapo sahihi, lakini kinachotakiwa ni maboresho na marekebisho.

Kiundwe chombo kitakachokutanisha wadau mbalimbali, wakiwemo wanasiasa, taasisi na asasi za kiraia ili kubaini maeneo yanayohitaji maboresho katika Katiba ya sasa,” alisema Askofu Malekana.

Maeneo mengine yanayotolewa maoni mbele ya kikosi kazi hicho ni mikutano ya hadhara ya ndani ya vyama vya siasa, uchaguzi, mfumo wa maridhiano ili kudumisha haki, amani, utulivu na umoja wa kitaifa, ushiriki wa wanawake na makundi maalumu katika siasa na demokrasia ya vyama vingi.

Maeneo mengine ni pamoja na elimu ya uraia, rushwa na maadili katika siasa na uchaguzi, ruzuku ya Serikali kwa vyama vya siasa, uhusiano wa siasa na mawasiliano kwa umma na Katiba mpya.