Wabunge walia na madeni ya makandarasi, fidia

Muktasari:
- Wabunge wamejadili makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka 2025/26 huku wakilalamikia madeni ya makandarasi na fidia kwa wananchi wanaopisha miradi ya ujenzi.
Dodoma. Wabunge wameitaka Serikali kuandaa mkakati maalumu wa kulipa madeni ya makandarasi na wahandisi washauri, huku Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu ikisema hadi kufikia Februari 2025 deni limefikia Sh1.29 trilioni.
Wameyasema hayo wakati wakichangia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi wa wizara hiyo kwa mwaka 2025/26 bungeni leo Jumatatu Mei 5, 2025.
Katika mwaka wa fedha 2025/26 Wizara ya Ujenzi inaomba kuidhinishiwa Sh2.28 trilioni kati ya hizo, Sh2.18 trilioni zinakwenda katika shughuli za miradi ya maendeleo huku Sh90.46 bilioni zikienda katika matumizi ya kawaida ya wizara na taasisi zake.
Wakati kukiwa na ongezeko la bajeti, mwaka 2024/25, Bunge liliidhinishia wizara hiyo, Sh1.77 trilioni huku Sh1.68 trilioni zikienda katika shughuli za miradi ya maendeleo.
Akiwasilisha maoni ya kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, mjumbe wa kamati hiyo, Ally Jumbe amesema kamati imebaini kuwa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) imekosa uwezo wa kulipa madeni ya makandarasi na wahandisi washauri wa ndani na nje ya nchi.
Amesema hadi kufikia Februari, 2025, Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) ilikuwa na jumla ya deni lililozalishwa la Sh1.299 trilioni na kuwa kati ya deni hilo, Sh187.605 bilioni ni la makandarasi na wahandisi washauri wa ndani katika miradi ya barabara kuu.
Jumbe amesema pia kati ya Sh974.589 bilioni ni deni la makandarasi na wahandisi washauri wa nje na Sh136.983 bilioni ni riba.

Mbunge Iringa Mjini akichangia katika Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2025/26.
Amesema katika deni hilo, miradi inayoendelea ilikuwa inajumuisha jumla ya Sh507.759 bilioni na Sh652.213 bilioni ni deni la miradi iliyokamilika.
“Kwa deni hilo kuendelea kutolipwa, riba inazidi kuongezeka na inaathiri uchumi wa makandarasi hasa wa ndani na vilevile kuathiri maendeleo ya miradi ya barabara nchini,” amesema Jumbe.
Amesema Serikali imekuwa ikisuasua katika kulipa madai na madeni ya makandarasi na wahandisi washauri katika miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara na vivuko.
Jumbe amesema kwa sababu hizo, kamati inaishauri Serikali kuwa na mkakati madhubuti na wa kudumu ili kulipa madeni kwa wakati lakini pia kuwajengea uwezo makandarasi wa ndani ili watekeleze miradi mingi zaidi.
Fidia kwa wananchi
Jumbe amesema kamati imebaini kuwepo na changamoto ya muda mrefu ambapo Serikali haijalipa fidia kwa wananchi ambao wameachia ardhi yao kupisha miradi mbalimbali nchini.
Amesema inakadiriwa hadi kufikia Februari, 2025 kiasi cha fedha kilichokuwa kinachodaiwa kama fidia ni jumla ya Sh123.64 bilioni.
“Kamati haikuridhishwa na mwenendo wa Serikali kushughulika fidia hizo, ambazo kadri siku zinavyozidi kwenda, kiwango kinaongezeka,” amesema Jumbe.
Akichangia mjadala huo, Mbunge wa Viti Maalumu, Halima Mdee amesema Bunge limekuwa likitunga sheria ili fedha zinazokusanywa kutokana na tozo mbalimbali ziwafikie wananchi lakini hazipelekwi kunakotakiwa.
“Fedha zinakusanywa na TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) anabaki nazo Mwigulu Nchemba (Waziri wa Fedha) anafanya nazo nini labda mtuambie kama kuna matumizi mengine ya ziada labda Bunge halijui,” amesema.
“Kwa sababu kama Bunge tunasema tunakusanya Sh46 trilioni ama Sh47 trilioni mnatuambia kuwa mmekusanya ikija katika utekelezaji mnatuambia asilimia 20, mnapeleka wapi. Tusiwe tunapoteza muda hapa fedha zinakusanywa zinaishia katika mifuko ya watu. Mtupe majibu ya mantiki,” amehoji.
Aidha, Mdee ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) ameshauri kuwepo kwa mpango mahususi wa kusaidia makandarasi wazawa nchini ili waweze kupata zabuni za miradi yenye fedha nyingi.

Mbunge wa Viti Maalumu, Halima Mdee akizungumza bungeni alipokuwa akichangia mjadala wa kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2025 / 2026, jijini Dodoma jana. Picha na Hamis Mniha
Amesema Tanzania kuna makandarasi 13,000 lakini mfuko wa kuwasaidia umetengewa Sh4 bilioni.
Naye Mbunge wa Kilindi (CCM) Omary Kigua amesema ameona jitihada za kulipa madeni ya makandarasi lakini alishauri kasi iongezwe.
Amesema kwa kufanya hivyo kutawapa nguvu wazawa ambao wanaijenga nchi yao.
Naye Mbunge wa Iringa Mjini (CCM), Jesca Msambatavangu amesema kazi na utu ni pamoja na kuhakikisha kuwa makandarasi wanalipwa fedha zao wanazodai kwa sababu wana mtandao mkubwa wa watu wanaowategemea.
“Huku kuna watu wanaouza nondo, wao nao wameajiri watu, wana watoto wanaowasomesha kwa hiyo usipowalipa makandarasi kuna mnyororo mkubwa wa watu wanaowategemea,” amesema.