Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wabunge wahoji hatua wanaodhalilisha mitandaoni, Serikali yajibu


Muktasari:

  • Baadhi ya wabunge wameibua maswali mbalimbali ya udhalilishaji mitandaoni na hatua zinazochukuliwa. Serikali imeyajibu na kubainisha mikakati.

Dodoma. Serikali ya Tanzania imesema zaidi ya asilimia 50 ya makosa udhalilishaji mtandaoni yamefanyiwa kazi na hatua zimechukuliwa.

Hayo yamesemwa leo Jumatano, Mei 14, 2025 na Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Maryprisca Mahundi wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Dk Christina Mzava.

Katika swali la nyongeza, Dk Christina amesema kumekuwa na matukio mbalimbali katika mitandao ya kijamii ikiwamo baadhi ya wanafunzi wakionyesha matukio ya kinyume cha sheria na udhalilishaji, ambapo amehoji Serikali imechukua hatua gani.

Amesema pia kumekuwa na matukio mengi ya udhalilishaji katika mitandao ya kijamii na kuhoji Serikali imeshachukua hatua kwa kiasi gani kwa wale wanaofanya uhalifu huo.

Akijibu swali hilo, Maryprisca amesema matukio hayo mengi yanashughulikiwa na Jeshi la Polisi na hatua zimeshachukuliwa kwa waliofanya na sheria inafuata mkondo wake.

“Zaidi ya asilimia 50 ya makosa yaliyojitokeza yamefanyiwa kazi na taratibu mbalimbali za kisheria zimechukuliwa dhidi yao,”amesema.

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Dk Christina Mzava, akiuliza swali la nyongeza kwa Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Maryprisca Mahundi leo Jumatano Mei 14, 2025 bungeni jijini Dodoma. Picha na Hamis Mniha

Naye Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Fatma Toufiq amesema baadhi ya waathirika wa udhalilishaji mtandaoni wamekuwa wakitolewa picha zao bila ridhaa zao.

“Je, Serikali inatoa kauli gani kuhusiana na jambo hilo,” amehoji Fatma ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii.

Akijibu swali hilo, MaryPrisca amewataka wataalamu wao kuendelea kutoa elimu hasa wale wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na polisi,  kwa sababu kutumia taarifa za mtu bila idhini yake ni kosa la jinai.

“Na tunamshukuru mheshimiwa Rais ameunda taasisi maalumu inayolinda taarifa za mtu binafsi hivyo sheria itachukua mkondo wake bila kumuonea aibu mtu yoyote,” amesema.

Katika swali la msingi, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Tauhida Galloss amehoji kuna mpango gani wa kudhibiti udhalilishaji na ukatili kwa wanawake unaofanywa kupitia mitandao ya kijamii.

Akijibu swali hilo, Maryprisca amesema Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendesha kampeni za kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii.

Amesema elimu hii imetolewa kwa makundi mbalimbali yaliyojumuisha wanafunzi wa shule za sekondari pamoja na wanawake.

“Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum na wadau wengine wamefanya majadiliano kuhusu njia za kuimarisha usalama wa mitandao na kupambana na uhalifu mtandaoni, ikiwa ni pamoja na unyanyasaji dhidi ya wanawake,” amesema.

Amesema pia wizara inasimamia utekelezaji wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 na Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ya mwaka 2022 zilizotungwa mahsusi kwa ajili ya kulinda watumiaji wa mtandao, hasa wanawake, dhidi ya unyanyasaji na ukatili wa mtandaoni.