Wabunge tisa walivyombana Waziri Mwigulu

Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba akijibu maswali ya wabunge katika kikao cha 44 cha mkutano wa bunge la bajeti jijini Dodoma, Juni 10, 2024. Picha na Hamis Mniha
Muktasari:
- Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba amelazimika kujibu maswali ya nyongeza zaidi ya tisa ya wabunge yaliyojitokeza baada mbunge wa Tabora Mjini, Emmanuel Mwakasaka kuuliza swali la msingi.
Dodoma. Wabunge tisa wamembana Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba baada ya kumuuliza maswali bungeni kuhusu fidia kwa wanaopisha maeneo pamoja na malipo kwa wastaafu kikiwamo kikokotoo cha mafao ya mkupuo.
Wabunge waliomuhoji maswali hayo leo Jumatatu Juni 10, 2024 wakati wa kipindi cha maswali na majibu ni Rita Kabati, Hawa Mwaifunga, Agnes Hokororo (viti maalumu), Rehema Migila (Ulyankulu), Priscus Tarimo (Moshi Mjini), Hassan Mtenga (Mtwara Mjini).
Wengine ni Zacharia Issay (Mbulu Mjini), Richard Maboto (Bunda Mjini) na Emmanuel Mwakasaka (Tabora Mjini.
Akiuliza swali, Kabati amehoji Serikali imefikia wapi kurekebisha suala la kikokotoo cha mafao ya mkupuo kwa kuwa wastaafu wamekuwa wakilalamika na hata wabunge wakienda katika majimbo yao bado suala hilo linaulizwa.
Akijibu swali hilo, Dk Mwigulu amesema Serikali na vyama vya wafanyakazi nchini, walishakubaliana maeneo wanayoendelea kufanya kazi ndani ya Serikali na kwamba muda muafaka watakapoyakamilisha watayasema.
Naye, Rehema amesema kwa mujibu wa tafiti zinaonyesha kuwa muda wa kuishi kwa Mtanzania hivi sasa umeshuka sana.
Amesema katika kipindi cha kustaafu ambacho ni miaka 60 na kuendelea, wastaafu wamekuwa wakikumbana na magonjwa na ugumu wa maisha hali inayowafanya wapate msongo wa mawazo.
“Je Serikali ina mpango gani wa kuwaongezea kile kiwango cha mafao ya mkupuo asilimia 33 hadi 80 ili wafurahie mafao yao kipindi chote ambacho kimebakia,” amehoji Rehema.
Akijibu Dk Mwigulu amemuomba mbunge huyo kupokea sehemu ya mwisho ya swali hilo kwa sababu ni miongoni mwa mambo wanayoendelea kufanyia kazi na wizara ya kisekta.
“Lakini kipengele cha kwanza alichosema lifespan (muda wa kuishi), umepungua na nadhani sasa umeongezeka na hata sasa wanaume tunaishi sana, tumesogea sogea kwa hiyo lifespan imeongezeka,” amesema.
Dk Mwigulu amesema kwa sehemu ya pili ya swali lake, ni mambo wanayoendelea kuyafanyia kazi na wataendelea kuwasiliana na vyama vya wafanyakazi kuhusu Serikali inasema nini juu ya suala hilo.
Naye, Mtenga amesema katika jimbo lake la Mtwara Mjini kuna watu wanadai katika Mfuko wa Pride zaidi Sh600 milioni na Dk Mwigulu aliahidi tangu 2021 kuwa watawalipa fedha zao.
“Ni lini mtakwenda kuwalipa wananchi wao wanaotaabika na hawaelewi wapi waende wapate fedha zao ambazo tayari ziliingizwa katika Mfuko wa pride,” amehoji Mtenga.
Akijibu swali hilo, Dk Mwigulu amekiri ni kweli mbunge huyo amekwenda wakati kadhaa, kufuatilia madai ya wananchi wake na wanaendelea kukamilisha taratibu zinazotakiwa.
“Nimuombe tukishamaliza maswali tukae ili mimi na yeye, tukae na wataalamu wangu ili aweze kupata hatua ambayo imefikiwa na Serikali,” amesema Dk Mwigulu.
Kwa upande wake, Tarimo amehoji ni lini Serikali itapeleka bungeni muswada wa sheria, itakayorekebisha pensheni ya waliostaafu muda mrefu ili iendane na wastaafu wa sasa hivi.
Akijibu Dk Mwigulu amesema wameipokea hoja ya mbunge huyo na kwamba waijumlisha katika masuala wanayoendelea kuyafanyia kazi, lengo likiwa ni kuboresha malipo kwa wastaafu.
Naye Issay amesema mwaka 1985, Serikali iliwastaafisha watumishi wa umma kwa mkupuo na kuwa hadi sasa watumishi hao wapo hai.
“Je, Serikali haioni ni wakati muafaka wa kuangalia upya waliostaafishwa kwa mkupuo ili waweze kulipwa pesheni kwa kiasi kinachowezekana,” amehoji Issay.
Akijibu swali hilo, Dk Mwigulu amesema jambo la ulipaji wa mafao ni jambo lenye fomula kutokana na uchangiaji.
Hata hivyo, amesema wamelipokea na wataendelea kulifanyia kazi kama alivyosema mbunge huyo kwamba waangalie uwezekano.
Kwa upande wake, Hokororo amehoji Serikali ina mpango gani wa kulipa mafao ama madai ya wazee waliopigana wa vita vikuu vya pili vya dunia wanaoendelea kudai hadi sasa.
Akijibu swali hilo, Dk Mwigulu amesema suala hilo lina historia ndefu kwa wale ambao kumbukumbu zao zilisadiki kulipwa, walishalipwa na kama kuna ambao madai yao ni uhakika (genuine) na hawajalipwa anadhani taratibu za masuala ya malipo zitafuatwa.
Hata hivyo, amesema katika kumbukumbu alizonazo wale ambao kumbukumbu zao zilisadiki kulipwa wameshalipwa.
“Kama mheshimiwa mbunge ana maeneo mahususi ama kumbukumbu mahususi zinazohusiana na suala hilo basi tutawasiliana naye ili tuweze kuzipokea,” amesema Dk Mwigulu.
Aidha, Maboto amehoji Serikali inalipa lini watu wa Kata ya Nyatwali wanaohamishwa kutoka maeneo yao.
Akijibu swali hilo, Dk Mwigulu amesema pamoja ya kuwa ni swali jipya kwa kuwa swali la msingi lilihusiana na hili ni fidia, jambo hili lilishafika mezani mwao.
“Ni moja ya eneo linafanyiwa kazi kwa karibu, kwa hiyo eneo la Nyatwari na Kipunguni jijini Dar es Salaam pamoja na maeneo yanayohusiana na masuala ya fidia. Kwa hiyo tumepokea mheshimiwa mwenyekiti tunayafanyia kazi na punde hali fedha itakaporuhusu tutaendelea kulipa,” amesema.
Naye Mwaifunga amehoji Serikali ina mpango gani wa kuwalipa waliokuwa wafanyakazi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki waliokuwa wakifanya kazi vyuo vikuu.
Akijibu swali hilo, Dk Mwigulu amesema wale wote ambao kumbukumbu zinaafiki na kusadikiki wanatakiwa walipwe, Serikali italipa lakini kwa wale waliowahi kufanya kazi katika maeneo mengine wengi wao walishalipwa.
“Wengine ambao uhakiki utaonyesha kuwa wanafaa kulipwa, watalipwa. Serikali italipa kufuatana na upatikanaji wa fedha, lakini kumbukumbu tulizonazo maeneo hayo ambayo mheshimiwa mbunge ameyasemea malipo yameshafanyika,” amesema.
Katika swali la msingi, Mwakasaka amehoji Serikali ina mpango gani wa kuwalipa wastaafu kwa wakati mafao yao.
Akijibu swali hilo, Dk Mwigulu amesema Serikali imeishasimika Mfumo wa Malipo ya Pensheni - TPPS kwa waajiri wanaolipwa mafao na Hazina pamoja na kuskani majalada yote ya wastaafu na kuyahifadhi katika Mfumo wa Malipo ya Pensheni.
“Hii imesaidia mstaafu kupata taarifa na majibu yake kwa haraka pindi wanapotembelea ofisi za Hazina Ndogo zilizopo mikoa yote,” amesema.
Amesema Serikali inaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusiana na mafao ya hitimisho ili mstaafu ajue mfuko sahihi anaopaswa kulipiwa na aina ya mafao atakayostahili kulipwa.
Katika maswali ya nyongeza Mwakasaka bado kuna matatizo mengi sana kwa wastaafu hasa katika kufuatilia haki zao, jambo ambalo hadi wengine kufa kabla hawajapata mafao yao.
Amehoji Serikali ina mpango gani wa kuboresha mfumo ili wastaafu waweze kupata fedha zao kwa wakati.
“Kuna tabia ya kutopeleka mafao ya wastaafu, kitu ambacho wanapofuatilia wanakuta baadhi ya mafao hayajafika sehemu yake. Je Serikali inawachukulia hatua gani wastaafu hao wale wasiopeleka makato ya wastaafu,” amehoji Mwakasaka.
Akijibu swali hilo Dk Mwigulu amesema kama alivyosema katika swali la msingi kuwa wameweka mfumo hiyo yote, lengo ni kupunguza urasimu uliokuwa unahusisha kufanya vitu kwa njia ya kianalojia.
Amesema wanaamini kwa utaratibu huo, jambo hilo litakuwa limeisha. “Jambo hili lilishachukuliwa na mheshimiwa waziri anayeshughulikia hii.”
Kuhusu kutopelekwa kwa michango na waajiri, Dk Mwigulu amesema sekta inayohusika na jambo hilo (Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) ililitolea kauli na huo ndio msimamo wa Serikali.
Amesema wataendelea kulifuatilia kwa karibu sana jambo hilo na endapo kutatokea ucheleweshaji wa makusudi wa aina hiyo basi hatua makusudi zichukuliwe.