Wabunge Geita ‘wamlilia’ Rais Samia ujenzi barabara Geita-Kahama

Rais Samia Suluhu Hassan akiwasalimia wananchi wa Katoro mkoani Geita wakati alipowasili mkoani humo kufanya ziara ya kikazi ya siku moja leo Jumamosi Oktoba 15, 2022.
Muktasari:
Wabunge wa mkoa wa Geita wametoa kilio cha ujenzi wa barabara inayounganisha mkoa huo na ule wa Shinyanga yenye urefu wa kilomita 58 na kumuomba Rais Samia Suluhu Hassan kusaidia ili iweze kujengwa kwa kiwango cha lami.
Geita. Wabunge wa mkoa wa Geita wametoa kilio cha ujenzi wa barabara inayounganisha mkoa huo na ule wa Shinyanga yenye urefu wa kilomita 58 na kumuomba Rais Samia Suluhu Hassan kusaidia ili iweze kujengwa kwa kiwango cha lami.
Wakizungumza leo Jumamosi, Oktoba 15, 2022 kwa nyakati tofauti mbele ya Rais Samia katika viwanja vya Kalangalala mjini Geita, Mbunge wa Geita Mjini (CCM), Constantine Kanyasu, Joseph Msukuma (Geita Vijijini) na Tumaini Magesa wa Busanda wamesema barabara hiyo imekuwa ikiwekwa kwenye ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa awamu mbili sasa lakini bado haijajengwa.
Kanyasu amesema barabara ya Geita-Kahama ni barabara inayobeba uchumi wa mkoa huo wenye rasilimali kubwa ya madini ya dhahabu.
Kauli hiyo imeungwa mkono Magesa aliyedai barabara hiyo imewekwa kwenye ilani awamu mbili tofauti lakini hadi sasa haijaanza kutekelezwa.
Mbali na kilio cha barabara, Kanyasu amemuomba Rais Samia kupandisha hadhi mji huo na kuupa sifa ya kuwa manispaa kwa kuwa unakidhi vigezo vyote kuanzia mapato na idadi ya watu.
Aidha, Magesa na Msukuma wamemuomba Rais kuigawa halmashauri ya Geita ambayo wananchi wajimbo la Busanda wanalazimika kutembea zaidi ya kilomita zaidi 100 kufuata huduma makao makuu ya halmashauri yaliyoko Nzera.
Wabunge hao wamemshukuru Rais Samia kuwezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali kwenye mkoa huo ikiwemo miradi ya elimu, afya, maji na barabara