Musukuma: Watu wanashindana kuzaa wakajaze madarasa

Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Kasheku Msukuma
Muktasari:
- Musukuma amesema wakazi wa eneo la Buseresere Katoro mkoani Geita, wanalazimika kutembea zaidi ya Kilometa 107 kwenda ilipo halmashauri yao ya Nzera kufuata huduma za kijamii jambo ambalo amesema litakomeshwa kwa kuanzishwa halmashauri katika eneo hilo.
Mwanza. Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Kasheku Musukuma amesema wakazi wa mji mdogo wa Katoro mkoani Geita wanashindana kuzaa ili wakajaze madarasa yaliyojengwa kupitia mradi wa Uviko-19, ambapo kwa Busanda pekee zaidi ya madarasa 70 yamejengwa na serikali katika eneo hilo.
Pia, amesema katika eneo hilo linalokadiliwa kuwa na Kaya zaidi ya 140, 000, watoto 3, 000 huzaliwa kwenye kituo kimoja cha afya kila baada ya miezi mitatu huku akisema kuna umuhimu wa kuanzishwa Halmashauri mpya ili kusogeza huduma za kijamii kwa wananchi hao.
Mbunge huyo ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Oktoba 15, 2022 wakati Rais Samia Suluhu aliposimama katika eneo la Buseresere kuzungumza na wananchi, ambapo amemuomba atangaze eneo hilo kuwa wilaya ili kusogeza huduma kwa wananchi hao.
Amesema wakazi wa eneo hilo wanalazimika kutembea zaidi ya Kilometa 107 kwenda ilipo halmashauri yao ya Nzera kufuata huduma za kijamii jambo ambalo amesema litakomeshwa kwa kuanzishwa halmashauri ya Busanda ili kusogeza huduma hizo.
"Busanda peke yake ina wakazi zaidi ya 800,000 na Geita Vijijini ina wakazi 500,000...yani kila baada ya miezi mitatu hapa tunazaa shule ya msingi, tuna shule zaidi ya 20, pia ikikupendeza kwa vile Waziri wa Afya yuko hapa atupatie DMO (Mganga Mkuu wa Wilaya)," amesema Msukuma
Ameongeza; "Huku tuko vizuri hatuna tatizo la afya ya akili au siyo (Wananchi wanashangilia) na mama kazi umeipiga tukienda uwanjani tutakueleza.....wasukuma kwa kuzaa wako vizuri lakini sasahivi watu wanashindana kuzaa ili wakajaze madarasa,"
Awali, Mbunge wa Busanda (CCM), Tumaini Magesa alimuomba Rais Samia kulipatia eneo hilo wilaya ya Busanda mara uchumi utakapoimarika huku akisema uboreshaji wa miundombinu ya eneo hilo unaendelea ili kufanikisha lengo hilo.
Amesema; "Eneo hili lina Kaya 140,000, kwenye kila kituo kimoja cha afya watoto zaidi ya 1,000 huzaliwa kwa mwezi, tuna vituo vitano unaweza kujua wangapi watazaliwa kwa mwaka kwa kuanzisha wilaya tutaweza kuwa na eneo ambayo linajitawala kiwilaya," amesema.
Hata hivyo, Rais Samia Suluhu Hassan bila kujibu maombi ya wabunge hao amewataka wakazi wa eneo hilo kufanya kazi, kutunza usalama, ulinzi na amani ya nchi kwa kuwa watulivu.
"Mapokezi haya yananipa picha kwamba Geita ni mkoa ambao unahitaji maendeleo, tufanye kazi, tuzalishe mpunga kwa wingi sana tule mwingine tusafirishe nje twendeni tukachape kazi," amesema
Rais Samia anaendelea na ziara yake ya siku moja mkoani Geita ambapo leo Saa 10:00 jioni anatarajiwa kuzungumza na wananchi wa mkoa huo katika viwanja vya Kalangalala Geita.