Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Huu hapa ugonjwa unaomtesa Bwege

Muktasari:

  • Itakumbukwa Bwege aliwahi kuumwa sukari, ugonjwa uliosababisha akatwe mguu wake wa kushoto miezi kadhaa iliyopita.

Dar es Salaam. Aliyewahi kuwa mbunge wa Kilwa Kusini, Seleman Bungara (Bwege) ameeleza magumu anayopitia kwenye ugonjwa wa figo unaomsumbua hivi sasa.

Itakumbukwa Bwege aliwahi kuumwa sukari, ugonjwa uliosababisha akatwe mguu wake wa kushoto miezi kadhaa iliyopita.

Akizungumza na Mwananchi jijini Dar es Salaam leo Alhamisi Aprili 17, 2025, mwanasiasa huyo aliyevuma kwa vionjo vyake vya ulisikia wapi?, inawezekanje? na uliona wapi? akiwa bungeni amesema baada ya tatizo la sukari lililopelekea akatwe mguu, hivi sasa anasumbuliwa na figo.

"Nimeambiwa figo zangu zimefeli, njia pekee ni kufanyiwa oparesheni na kubadilisha figo," amesema Bwege kwa unyonge alipozungumza na Mwananchi Kigamboni anakoishi hivi sasa.

Mbunge Bwege

Amesema daktari wake amemueleza njia pekee ya yeye kupona na kurudi kwenye hali ya kawaida ni kufanyiwa oparesheni na kuwekewa figo nyingine.

Akizungumzia ugonjwa huo ulivyomuanza hadi kugundulika, Bwege amesema akiwa Kilwa, aliugua BP kali.

"Nilienda hospitali kule kule Kilwa, walishindwa kuona tatizo, wakanishauri nije Mloganzila," amesema Bwege.

Hata hivyo, anasema Mloganzila baada ya vipimo ikaonekana ana tatizo la figo.

"Ilionekana zimefeli ikabidi nisafishwe, nimekuwa kwenye tiba hiyo kwa miezi kadhaa sasa na kila wiki nasafishwa mara mbili.”

"Daktari wangu alinishauri nikiweza nifanyiwe  oparesheni, kwa sababu kusafishwa ni muda mrefu na si tiba, inapunguza tu sumu," amesema Bwege.

Amesema matamanio yake ni kutibu kwa kuondoa figo zilizofeli na kuwekewa nyingine, na matibabu yake, daktari wake anayemtibu Mloganzila amemueleza gharama yake si chini ya Sh35 milioni.

"Kati ya hizo, Sh5 milioni ni tiba ya mwanzo, kujua vipimo vinataka nini, yule atakayenipa figo naye apimwe na Sh30 milioni ni za matibabu,” amesema Bwege.

Hata hivyo, anasema ameambiwa kuna Mfuko wa Mama Samia ambao unasaidia gharama za matibabu kwa wagonjwa kama yeye, unaweza kumchangia Sh15 milioni, hivyo anatakiwa atafute Sh20 milioni.

Bwege amesema kwa mujibu wa madaktari, oparesheni hiyo anatakiwa kufanyiwa Julai, mwaka huu.

"Siwezi kukosa mtu wa kunitolea figo, huyo nitapata, kikubwa nipone nirudi katika hali yangu ya kawaida, nikishindwa kufanyiwa oparesheni, basi itabidi niendelee kusafisha.

"Kinachonisikitisha maisha yangu yote tangu nizaliwe mwaka wa 64, naishi Kilwa, hii tiba ya kusafishwa inabidi kila wiki ifanyike mara mbili, Kilwa haipo ni hadi Dar es Salaam. Hii maana yake nihame Kilwa, kitu ambacho ni kigumu sana kwa mazingira yangu, lakini kama nitashindwa kutibiwa, kwa kuwa nipo tayari kufanyiwa oparesheni, sitakuwa na namna nyingine zaidi ya kuhamia Dar es Salaam,” amesema.


Alivyoanza kuumwa

Akizungumzia ugonjwa huo, Bwege amesema ilianza dalili ya kushindwa kula.

"Sikuhisi ladha kwenye chakula pia nilikuwa natema mate sana na kukojoa sana, hasa usiku, nikaenda kupima ndipo nikaambiwa tumboni kuna maji,” amesema.

Hata hivyo, amesema hospitali iliyobaini ugonjwa wake wa kufeli kwa figo ni ya Mloganzila.

"Sikuwa naweza kula chakula kabisa, nashkuru Mungu baada ya kusafishwa hivi sasa nakula, mate hayatoki tena, ingawa ninachokitamani sasa ni oparesheni.


Kuhusu sukari

Miezi kadhaa iliyopita Bwege alikatwa mguu wake wa kushoto kutokana na changamoto ya sukari.

Lakini anasema kwa sasa hana tena changamoto ya sukari iko sawa.

"Hata madakatari wamenishauri nisinywe dawa za sukari, kwa sasa namshukuru Mungu, imepungua, sielewi kwa nini imepungua, kwani ilifikia hatua ya kujichoma mwenyewe sindano za insulini. Lakini sasa madaktari wameniambie nisitumie kabisa dawa za sukari na wala haipandi tena,” amesema.

Bwege anasema awali sukari ndiyo iliyosababisha apoteze mguu wa kushoto, ambao ulikuwa na kidonda kilishindikana kutibika .


Hatogombea mwaka huu

Akizungumzia harakati zake za siasa, Bwege amesema kutokana na afya yake hatogombea ubunge wa Kilwa mwaka huu wa uchaguzi.

"Mwaka huu  kwa afya yangu sitoweza kugombea, afya ni muhimu na kazi ya kuwatumikia wananchi ni muhimu pia ila sina namna,” amesema.

Lakini amesema ugonjwa hauwezi kumzuia kukitumikia chama chake cha ACT Wazalendo.

“Najua mwaka huu ni wa uchaguzi, kwa hiyo na mimi ni miongoni mwa wanachama watiifu tunaopaswa kuzipigia kasoro tulizozibaini ili zirekebishwe,” amesema Bwege.